Mtandao wa kufuatilia matokeo ya tafiti Afrika wazinduliwa Arusha

Arusha. Wataalamu wa utafiti barani Afrika wamezindua mtandao mpya wa bara zima unaolenga kuimarisha ushirikiano wa kisayansi na kuhakikisha kuwa matokeo ya tafiti yanatoa manufaa halisi kwa jamii katika maeneo mbalimbali ya Afrika.

Mtandao huo, unaojulikana kama ‘Continental-Wide Research Networks’, unakusudia kuziunganisha taasisi za elimu ya juu, vituo vya utafiti na watafiti kutoka nchi mbalimbali za Afrika ili kuwezesha kubadilishana data, kufanya tafiti za pamoja na kutoa suluhisho la pamoja kwa changamoto zinazolikabili bara.

Uzinduzi huo umefanyika kwenye Mkutano wa watafiti Afrika 2025 ulioandaliwa na Chuo cha Usimamizi cha Afrika Mashariki na Kusini (ESAMI) na kuwaleta pamoja washiriki zaidi ya 500, wakiwemo watafiti, wasomi wa vyuo vikuu, wawakilishi wa sekta binafsi, watunga sera na wabunifu kutoka Afrika na mataifa mengine.

Mbali na mtandao huo, mkutano huo pia umezindua Jukwaa la Utendaji za Mandhari za Utafiti za Kimataifa za Esami (EGRETA-CP) litakalowaunganisha watafiti wanaofanya kazi kwenye sekta mbalimbali kwa lengo la kushirikiana katika tafiti za kikanda na kimataifa.

Jukwaa hilo linakusudia kuwaunganisha watafiti, wataalam wa kiufundi na watunga sera ili kubadilishana maarifa, mbinu bora na kusambaza matokeo ya tafiti yatakayoweza kuchangia ajenda ya maendeleo barani Afrika.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Esami, Dk Peter Kiuluku amesema taasisi hizo mpya zimeanzishwa ili kuongeza ubunifu, kuimarisha ushirikiano na kukuza matumizi ya matokeo ya tafiti katika utungaji sera na katika kutatua changamoto za Afrika.

Amesema toleo la kwanza la mkutano huo limewakutanisha zaidi ya watu 500, wakiwemo wataalamu 300 wenye shahada za uzamivu (PhD) na wawakilishi kutoka vyuo 63 barani Afrika, Ulaya na Marekani.

Aidha, amesema kuwa mkutano huo umehusisha uwasilishaji wa makala nane za kisayansi pamoja na mihadhara miwili ya umma.

“Kaulimbiu ya mkutano wa mwaka huu ni  “Ekosistimu za utafiti barani Afrika: utawala, matokeo na athari kwa jamii’ inajikita katika kuboresha mazingira ya utafiti kupitia kuimarisha mifumo ya utawala, kuboresha ubora wa matokeo ya tafiti na kuhakikisha kwamba tafiti za Afrika zinatoa athari chanya kwa jamii,” amesema.

Dk Kiuluku ameongeza kuwa majadiliano pia yameangazia changamoto sugu zinazokwamisha utafiti barani Afrika, ikiwemo uhaba wa rasilimali, uwezo mdogo wa kiufundi na ukosefu wa ufadhili wa kutosha.

“Changamoto nyingine ni pamoja na haja ya kuongeza ushirikiano wa kikanda, kuunganisha utafiti moja kwa moja na utungaji sera, na kutoa maarifa yanayoweza kutekelezwa moja kwa moja kuboresha ustawi wa jamii” amesema

“Hizi ndizo sababu za kuanzisha mitandao hii na majukwaa haya ili tufanye kazi kwa pamoja na kuhakikisha manufaa ya tafiti yanawafikia wananchi,” amesema.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Esami, Dk David Kalaba, amesisitiza kuwa mitandao mipya inalenga kujenga mfumo wa utafiti uliokomaa, jumuishi na unaojibu mahitaji ya Afrika.

“Hatua hii pia itawezesha bara kushiriki kikamilifu katika uchumi wa maarifa na katika maendeleo endelevu ya dunia,” amesema.

“Tunapoadhimisha miaka 50 ya Esami, tunathibitisha upya dhamira yetu ya kuimarisha ekosistimu ya utafiti barani Afrika na kuunganisha maarifa na vitendo ili kutoa matokeo halisi kwa maendeleo ya bara.”

Awali, Profesa Kazhila Chinsembu, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu ya Juu ya Zambia, amesema kuwa utafiti una thamani tu pale unapofikishwa kwa matumizi na unapoweza kuboresha maisha ya watu.

“Afrika inahitaji utafiti unaoiwezesha kushiriki kikamilifu na kunufaika na maendeleo endelevu ya dunia. Hiyo ndiyo sababu majukwaa haya ni muhimu,” amesema.