Mtanzania awa Mwafrika wa kwanza kushinda tuzo ya kimataifa ya moyo

Dar es Salaam. Mtafiti na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo, Dk Pedro Palangyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) anakua Mtanzania na Mwafrika wa kwanza katika historia baada ya kutunukiwa tuzo ya kimataifa ya Dr Jay Brown International Best Abstract.

Mbali na tuzo hiyo, Dk Pedro ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na Mafunzo wa JKCI pia ametunukiwa tuzo ya Paul Dudley White International Scholar ambayo haijawahi kutolewa kwa Mtanzania tangu ianzishwe.

Tuzo hizo zilitolewa katika mkutano wa American Heart Association (AHA) uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita mjini New Orleans, Jimbo la Louisiana nchini Marekani.

Akizungumzia tuzo hizo, Dk Pedro amesema kutambuliwa kwake kimataifa kumetokana na utafiti wa miaka 10 uliofanywa na taasisi hiyo kuhusu magonjwa ya moyo yanayoathiri uzazi, yanayojulikana kitaalamu kama Peripartum Cardiomyopathy (PPCM).

“Nimekuwa Mtanzania na Mwafrika wa kwanza na pekee kupata tuzo hizi mbili za heshima, baada ya utafiti wangu kutambulika kwa kiwango cha juu katika mkutano wa AHA. Hii ni kwa sababu ya ubora wa kisayansi, uvumbuzi, na athari za utafiti huu katika kuelewa magonjwa ya moyo yanayoathiri uzazi duniani,” amesema Dk Pedro.

Amefafanua ushindi wa tuzo hizo katika mwaka mmoja ni mafanikio makubwa na ya nadra, sio tu kwa JKCI bali pia kwa Taifa, hatua iliyowashangaza wataalamu na wanasayansi wa kimataifa waliokuwepo kwenye mkutano huo.

Dk Pedro amesema kuwa ugonjwa wa PPCM ni nadra lakini hatari, na huwapata wanawake katika kipindi cha mwisho cha ujauzito au muda mfupi baada ya kujifungua.

“Utafiti huu wa muda mrefu umebaini kundi kubwa zaidi la wagonjwa wa PPCM duniani na umeleta mwanga mpya katika utambuzi, usimamizi na matokeo ya ugonjwa huu,” ameongeza.

Mafanikio hayo amesema yanaiweka Tanzania na Afrika Mashariki katika ramani ya kimataifa ya sayansi, hasa katika eneo la afya ya mama na magonjwa ya moyo.