Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, imemuhukumu kunyongwa hadi kufa mvuvi, Gato Francis, aliyetiwa hatiani kwa mauaji ya mamalishe, Neema Julius, kwa kumkata kwa panga shingoni kisha kumwibia Sh250,000.
Kwa mujibu wa Jamhuri katika kesi hiyo, mwili wa marehemu ulikuwa na jeraha shingoni la kukatwa na kitu chenye ncha kali, ukiwa umefungwa mikono, uso ukiwa umefunikwa kwa kitambaa na kutelekezwa kando ya bwawa.
Jaji Evaristo Longopa katika hukumu aliyoitoa Desemba 2, 2025, amesema baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili, mahakama imemtia hatiani mshtakiwa baada ya kujiridhisha kuwa upande wa mashtaka umethibitisha kesi bila kuacha shaka.
Mahakama imezingatia ushahidi kuwa mshtakiwa amethibitika ndiye aliyekuwa wa mwisho kuonekana na Neema kabla kukutwa akiwa amefariki dunia. Katika maelezo ya onyo mshtakiwa amekiri kumuua Neema kisha kumwibia fedha alizozitumia kununua bidhaa.
Gato alishtakiwa kwa mauaji kinyume cha kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu. Alidaiwa kutenda kosa hilo Oktoba 3, 2023 katika Kijiji cha Ufana, Kata ya Mgungira, Tarafa ya Sepuka wilayani Ikungi.
Upande wa Jamhuri uliokuwa na mawakili wawili, uliwasilisha mahakamani mashahidi sita na vielelezo vitatu. Mshtakiwa aliwakilishwa na wakili mmoja akiwa shahidi pekee wa utetezi.
Shahidi wa kwanza, Julius Kiula, ambaye ni baba wa Neema alidai Oktoba 5, 2023 alipata taarifa kuwa mwili wa binti yake aliyekuwa amepotea kwa siku kadhaa umepatikana ukiwa jirani na bwawa.
Alidai walitoa taarifa kituo cha polisi na walipokwenda eneo la tukio walikuta wanakijiji wakiwa wamezingira eneo hilo.
Baada ya uchunguzi wa mwili ilielezwa Neema alishambuliwa na kitu chenye ncha kali shingoni ambako kulikuwa na jeraha kubwa.
Shahidi wa pili, Abdallah Bugohe, ambaye ni tabibu alieleza Oktoba 29, 2023 aliagizwa na Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ikungi aongozane na askari hadi Kijiji cha Ufana kwa ajili ya uchunguzi wa mwili wa marehemu.
Alidai mwili huo ulikuwa umelazwa, mikono ikiwa imefungwa na uso ukiwa umefunikwa kwa kitambaa.
Alieleza uchunguzi ulibaini uwepo wa jeraha upande wa kulia wa shingo lililotokana na kitu chenye ncha kali, hivyo chanzo cha kifo ni kutokwa damu nyingi kutokana na jeraha shingoni.
Shahidi wa nne aliyemuhoji mshtakiwa maelezo ya ziada, alidai alikamatwa Novemba 2, 2023, Mugumu wilayani Serengeti na alikiri katika maelezo aliyoyatoa kwa hiari polisi kuhusika na kifo hicho.
Alidai mshtakiwa alisimulia kuwa Oktoba 3, 2023, alimchukua Neema kwenye mtumbwi alipokuwa anakwenda kununua mboga kwa ajili ya biashara.
Shahidi alidai mshtakiwa alikiri kupata tamaa ya kumnyang’anya fedha, hivyo alimkata shingo kwa panga.
Alidai baada ya kuandika maelezo alimsomea mshtakiwa ambaye aliyathibitisha kuwa yalikuwa sahihi na hakuwa na la kuongeza wala kukataa. Maelezo yalipokewa mahakamani kama kielelezo.
Shahidi wa sita, Asha Ramadhan, ambaye ni mamalishe alidai akiwa Kilingeni, Neema alimweleza anakwenda Magungu kununua mboga, hivyo aliondoka na fedha.
Alidai Neema aliondoka kwa kutumia mtumbwi wa Gato, ambaye alikuwa akimfahamu kwani alikuwa mteja wake na siku ya tukio alipata kifungua kinywa kwenye mgahawa wake.
Shahidi alidai Neema alikuwa amevaa dera la rangi ya chungwa na nyeusi, suruali ya kahawia, skafu shingoni na kofia nyekundu na kwamba aliondoka na Gato ila hakurejea.
Alidai alimfahamisha mwenyekiti wa kambi ya wavuvi na wakawasiliana na jamaa wa Neema.
Shahidi alidai Oktoba 29, 2023 walishuhudia mwili wa Neema ukiwa umeanza kuharibika.
Gato alidai ni mkulima katika Kijiji cha Gusuhi, wilayani Serengeti na mvuvi ambaye alifanya shughuli kwenye mabwawa ya Mtera, Doromoni na Ufana.
Alidai alikwenda Kijiji cha Ufana Februari 2023 alikokaa hadi Septemba 13, 2023 alipoondoka kwa kuwa kambi ya wavuvi ilikuwa imeteketea kwa moto, huku bwawa na ziwa vikiwa vimekauka.
Alidai Oktoba 3, 2023 alikuwa kijijini Gusuhi wilayani Serengeti, mkoani Mara alikokamatwa akituhumiwa kwa kosa la mauaji ya Neema.
Alikaa hadi Oktoba 5, 2023 akidai aliteswa na kupigwa na polisi akilazimishwa kukiri kosa. Alidai Novemba 11, 2023 alilazimika kusaini karatasi ambazo hakujua kilichokuwa kimeandikwa na alifanya hivyo kwa kuhofia usalama wa maisha yake, akaomba mahakama imwachie huru kwa kuwa hakuhusika na mauaji.
Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote, jaji amesema ni wajibu wa mahakama kuamua kama kosa la mauaji lilithibitishwa dhidi ya mshtakiwa au vinginevyo.
Amesema ni wajibu wa upande wa mashtaka kuthibitisha kosa hilo la jinai bila kuacha shaka yoyote kama inavyoelekeza na sheria.
Jaji Longopa alinukuu sehemu ya maelezo ya mshtakiwa aliyekiri kuchukua uamuzi wa kumuua mwathirika ili achukue fedha zake.
“Nilimnyang’anya mtandio aliokuwa amejifunga shingoni nikamfunga uso kwa kumziba macho ili asiweze kunishuhudia nikiwa ninamuua. Alijipekua baada ya kujipapasa kwenye maziwa yake kifuani na kunikabidhi pesa taslimu Sh250,000, zilizokuwa kwenye ziwa la kushoto. Nilimnyang’anya tena sweta alilokuwa ameshikilia mkononi nikamuamuru anyoshe mikono mbele nikamfunga mikono kwa mbele kwa kutumia sweta hilo,” inaeleza sehemu ya maelezo hayo.
“Nilishika panga langu lenye mpini wa mpira mweusi kwa mikono miwili nikamkata shingo kwa nyuma upande wa kulia na kumsababishia jeraha kubwa sana shingoni akadondoka chini ndani ya Ngalawa akalala chali, huku damu nyingi zikiwa zinamtoka kwenye jeraha nililomkata nilimsogeza karibu na nchi kavu na kugeuza mtumbwi na kumwacha chini kwenye tope akiwa amelala kifudifudi,” inaeleza sehemu ya maelezo ya mshtakiwa.
Jaji amesema kimsingi katika kielelezo hicho cha tatu, yanatoa maelezo kamili juu ya namna ambayo kosa la mauaji lilitekelezwa ambapo mshitakiwa alikiri kumfunga mwathirika wa tukio hilo kwa kutumia kitambaa usoni na kumfunga mikono miwili na kumkata kwa panga upande wa kulia wa shingo, na kusababisha kupoteza damu nyingi na kumwacha mwathirika huyo amelala chini kifudifudi.
“Hakika, maungamo haya yanahusisha vipengele vyote vya kosa la mauaji, mshtakiwa alikiri kumjeruhi jeraha la kukatwa kwa panga shingoni mwa mwathiriwa, sababu ya kumuua ilikuwa ni kupora fedha za marehemu na ni wazi kuwa ili kukwepa kufuatwa na polisi aliamua kukatisha maisha. Kwa hivyo, nia mbaya iko wazi kwani mshtakiwa alimkata marehemu,” amesema.
Baada ya kupitia ushahidi, Jaji Longopa amesema kukiri kwa mshtakiwa katika vielelezo viwili vilivyopokewa mahakamani, ushahidi ambao mahakama umekuwa ukiita ni ushahidi bora kuliko ushahidi mwingine wowote, ikizingatiwa ushahidi wa utetezi haukuweza kuongeza shaka yoyote kwa kushindwa kwake kuhoji juu ya mambo muhimu.
“Upande wa utetezi umeshindwa kuibua shaka yoyote kuhusu kesi ya mwendesha mashtaka. Katika hali hiyo, ushahidi wa upande wa utetezi haujaharibu ushahidi thabiti, wa wazi na wa kueleza wa mashahidi wa upande wa mashtaka,” amesema.
Jaji alihitimisha kuwa Mahakama imeona upande wa mashtaka umetekeleza wajibu wake wa kuthibitisha kesi hiyo bila kuacha shaka yoyote na kumuhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.