Pedro aachiwa zigo la Conte

KIKOSI cha Yanga kinajiandaa kushuka uwanjani leo kuvaana na Fountain Gate, lakini mapema mabosi wameamua kumuachia msala kocha Pedro Goncavales kuhusu kiungo mkabaji, Moussa Balla Conte wakimtaka asake mbadala wake kupitia dirisha dogo.

Mabosi wa Yanga ni kama hawajaridhishwa na uwezo wa Conte waliyemsajili kwa mbwembwe kutoka CS Sfaxien ya Tunisia na sasa wamemtaka Pedro kuanza mapema kusaka mbadala wa kiungo huyo raia wa Guinea.

Conte aliyetua Yanga mwanzoni mwa msimu huu kwa mkataba wa miaka miwili, amekuwa na wakati mgumu nafasi ndani ya kikosi, kwani ameanza mechi moja Ligi Kuu dhidi ya Pamba Jiji ambapo Yanga ilishinda  3-0 akiwa chini ya kocha Romain Folz.

Taarifa kutoka ndani ya Yanga ni kwamba mabosi wa klabu hiyo wamemmkabidhi Pedro jukumu la kutafuta kiungo mwingine baada ya kutoa taarifa za kutoridhishwa na kiwango cha Conte.

Upepo haujamwendea vizuri Conte ndani ya Yanga, kwani licha ya kuja kwa mbwembwe nyingi wakati wa usajili wake, lakini ameshindwa kuvutia makocha wote waliopita ndani ya kikosi hicho akipewa muda mchache tangu aanze kuvaa uzi wa njano na kijani.

Taarifa za ndani zimeliambia Mwanaspoti kuwa Pedro ameshaanza msako wa kiungo mkabaji, ambapo kama atapatikana haraka, basi timu hiyo inaweza kufanya uamuzi mgumu hata dirisha dogo la usajili.

Hadi sasa Yanga ina mambo mawili ikipambana kuchagua moja. Kwanza ni kama ikimpata kiungo mpya, basi itamtoa kwa mkopo Conte, lakini kuna uwezekano wa kuachana naye moja kwa moja.

Mwanaspoti linafahamu Yanga ilianza kitambo kutafuta mtu wa kuziba eneo la kiungo mkabaji ambalo kwa sasa wanachezwa Mudathir Yahya, Dube Abuya na Aziz Adambwile.

“Tunatafuta kiungo. Huyu Conte bado hasomeki kabisa unaweza kusema labda kachelewa kuzoea. Lakini kadri muda unavyokwenda unaona kabisa timu ni kubwa kwake,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:

“Kocha anatafuta kiungo. Unajua wakati anafika aliomba muda amuangalie kila mchezaji kabla ya kufanya uamuzi na ikifika anazungumzia watu wanaocheza eneo la Conte, haonyeshi kuwa na imani naye kubwa.

“Mliona katika mechi dhidi ya AS FAR Rabat tulilazimika kuongea na Mudathir, licha ya kwamba alikuwa hajapona sawasawa ili acheze kwa kuwa watu wana imani na ubora wake.”

Conte alicheza mechi moja ya kimataifa na mbili za ligi, huku akifikisha dakika 65, ilhali mechi zingine zote akisotea benchi.

Yanga ambao ni mabingwa wa Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA), kwa sasa ipo katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa na pointi nne sawa na vinara wa kundi B, Al Ahly na leo jioni inarejea katika Ligi Kuu Bara kuvaana na Fountain Gate kabla ya Jumapili kuifuata Coastal Union.