Rais Samia Suluhu Hassan ameahidi kusimamia utawala wa sheria pamoja na kuhakikisha watumishi wa umma wanakuwa na uadilifu na uwajibikaji katika kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wananchi kote nchini.
Katika hotuba yake wakati akizindua Bunge la 13 jijini Dodoma, Novemba 14, 2025, Rais Samia alieleza kwamba katika miaka mitano ya Serikali ya awamu ya sita, kipindi cha pili, atasimamia masuala ya utawala wa sheria, uwajibikaji na uadilifu.
Alieleza kwamba Serikali yake inahakikisha inapambana na rushwa, ubadhirifu wa mali za umma na ufisadi, jambo ambalo limekuwa ni changamoto kubwa inayosababisha wananchi kukosa huduma za msingi.
Katika hotuba yake hiyo ya takribani saa 1 na dakika 32, Rais Samia alieleza mkakati wa Serikali kusimamia nidhamu na kudhibiti ukosefu wa maadili kwa watumishi hasa wanaoendekeza maslahi binafsi.
Wasomi na wachambuzi waliozungumza na Mwananchi wanaeleza wasiwasi wao kama mifumo iliyopo nchini itawezesha mafanikio katika kuhakikisha utawala wa sheria, uwajibikaji na uadilifu vinapatikana nchini.
Hata hivyo, baadhi yao wamepongeza hatua hiyo wakieleza kwamba kukosekana kwa uwajibikaji na utawala wa sheria kumekuwa ni tatizo linalosababisha wananchi kukosa huduma au haki zao kwa wakati.
Akizungumza katika hotuba yake wakati akizindua Bunge la 13, Rais Samia alisema ili kufikia malengo yote ya maendeleo waliyopanga kuyafanya katika miaka mitano ijayo, mafanikio yake ni kuwa na utawala wa sheria, uadilifu na uwajibikaji katika kila ngazi, kuanzia juu mpaka chini.
Ili kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali za nchi pamoja na kupata huduma wanazostahili, alisema wataelekeza jitihada zao kwenye mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi, ubadhirifu, uzembe, ukosefu wa nidhamu na ukosefu maadili.
“Ni lazima tudhibiti wachache wanaotaka kuturudisha nyuma kwa kuendekeza maslahi binafsi.
“Aidha, ili kuimarisha uwajibikaji Serikalini, tutaendelea kutekeleza programu za maboresho ya utumishi wa umma, ikiwemo matumizi ya mifumo ya upimaji wa utendaji kazi. Wajibu huenda na haki, au haki huambatana na wajibu,” amesema.
Vilevile, alisema wataimarisha uwajibikaji na utendaji wa mashirika ya umma. Alisema kuelekea 2030, watafanya mageuzi ya mashirika ya umma ili kuboresha ufanisi, uwazi na tija.
Msingi mwingine wa mafanikio hayo, alisema ni utawala wa sheria. Alisema ahadi ni kuwa Serikali itashirikiana kwa dhati na Mahakama ya Tanzania kuhakikisha haki inapatikana kwa watu wote na kwa wakati.
“Tutaendelea kuwezesha Mahakama kwa majengo, vitendea kazi, watumishi pamoja na kuimarisha matumizi ya Tehama. Tunachukua hatua zote hizi ili Mhimili huu uweze kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi.
“Tutasimamia utekelezaji kamili wa mapendekezo ya Tume ya Rais ya kuangalia namna ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai. Tutaendelea kufanya mageuzi na maboresho katika taasisi zote zinazoshughulikia masuala ya Haki Jinai ili ziweze kukabiliana na vitendo vyote vya uhalifu,” alisema.
Kwa upande mwingine, alisema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika sekta ya sheria, ikiwemo Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) pamoja na asasi zingine ili kuwezesha upatikanaji wa huduma na msaada wa kisheria kwa wananchi, kwani katika kipindi kilichopita wameona manufaa yake katika utatuzi wa changamoto zinazowakabili wananchi.
“Aidha, tutakamilisha tafsiri ya sheria zetu zote kwa lugha ya Kiswahili, ikiwa ni hatua muhimu kuhakikisha wananchi wetu wanaelewa kwa urahisi sheria za nchi,” alisema Rais Samia katika hotuba yake.
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Tumaini Munale anasema mambo aliyoahidi Rais ni muhimu lakini huenda utekelezaji wake ukawa si kama unavyotegemewa kutokana na mapokeo ya taasisi za Serikali.
“Msimamizi wa shughuli za Serikali ni Waziri Mkuu, huenda akafanikiwa kusimamia taaasisi zilizopo chini yake lakini je, kwa upande wa zile zilizopo Ofisi ya Rais itakuwaje, mapokeo ya watendaji wenyewe ngazi ya chini yapoje, wapo tayari kusimamia maelekezo haya? anahoji.
“Vipi mifumo ya chama tawala, inaruhusu mambo haya kufanyika? Serikali inaweza kuanza utekelezaji lakini mifumo ya chama nayo ikawa kikwazo, kwa hiyo jambo la muhimu ni kutengeneza mfumo bora wa uwajibikaji ambao hautamchagua mtu,” anahoji.
Munale anasema Serikali inayotanguliza uwazi, uadilifu na uwajibikaji huwa na nafasi kubwa ya kujenga utawala unaodumu, kwa kuwa misingi hiyo hutengeneza mazingira ya taasisi kufanya kazi bila upendeleo.
Kwa maana hiyo, anasema dhamira ya Rais Samia inawiana na kanuni za ujenzi wa utawala bora, hatua inayoweza kuimarisha imani ya wananchi na uwezo wa Serikali kutoa huduma kwa ufanisi.
“Historia ya nchi nyingi za Afrika imeonyesha kuwa vita dhidi ya rushwa mara nyingi hukwama pale ambapo taasisi kama Mahakama, vyombo vya uchunguzi na mashirika ya umma vinakuwa chini ya ushawishi wa kisiasa.
“Ikiwa maboresho yanayokusudiwa yataambatana na kuipa Mahakama uhuru wa kweli, kuimarisha vyombo vya haki jinai bila upendeleo na kuongeza uwazi katika bodi za mashirika ya umma, basi dhamira ya kujenga Serikali yenye uadilifu inaweza kufikiwa lakini bila uhuru huo, hatua hizo zinaweza kubaki ni ahadi nzuri zisizoleta matokeo ya mfumo,” anasema.
Kauli iambatane na mabadiliko
Mchambuzi wa siasa kutoka Chuo cha Taifa cha Zanzibar (Suza), Profesa Mohamed Makame anasema kauli ya Rais ya kudhibiti rushwa ni thabiti kama itachukuliwa kwa misingi ya kuleta mabadiliko.
Anasema mabadiliko hayo makubwa hasa katika wakati huu ambapo uchumi wa nchi utategemea rasilimali za ndani ni muhimu.
“Eneo ambalo lina fitina kubwa sana ni kwenye mapato na matumizi, bado hatujawa na nidhamu ya kutosha, mabadiliko ya kweli na maendeleo endelevu hayawezi kupatikana bila uwajibikaji.
Anasema katika mfumo wa utawala, viongozi wakuu ndiyo wasimamizi wakuu waliokabidhiwa mamlaka na dhamana ya kusaidia Serikali kufanikisha mipango yake.
Hata hivyo, anasema mafanikio ya mipango hiyo hutegemea kiwango ambacho watu waliopo kwenye mfumo wa utumishi wa umma wanaweza kuwajibika kwa uadilifu, uaminifu na weledi. Bila kuweka msingi wa uwajibikaji, hata sera nzuri hushindwa kuzaa matokeo.
“Kwa muda mrefu kumekuwapo changamoto kubwa katika utumishi wa umma ambapo uwajibikaji haujapewa uzito unaotakiwa,” anasema mwanazuoni huyo.
Baadhi ya watumishi wanafanya kazi kwa mazoea, kulindana na kutegemea mfumo usio na uwazi, hali ambayo imepunguza ufanisi na kuchelewesha utekelezaji wa majukumu muhimu.
Matokeo yake, anasema mambo yanayohitaji uangalizi wa karibu huachwa yakidhoofika na taswira ya taasisi za umma inaharibika mbele ya wananchi wanaotegemea huduma bora,” anasema.
Ikiwa kauli ya udhibiti na mageuzi itachukuliwa kwa misingi sahihi na kwa dhati ya kuleta mabadiliko, Profesa Makame anasema inaweza kuwa hatua muhimu kuelekea kujenga utawala bora.
Anasema nchi yoyote inayotaka kukua kiuchumi inategemea watumishi na viongozi wanaowajibika, wanaosimamia rasilimali kwa uadilifu na wanaofanya kazi kwa masilahi mapana ya taifa na si kwa masilahi binafsi.
Profesa huyo anasema kuimarisha uwajibikaji ni msingi ambao uchumi wa nchi yoyote, ikiwemo Tanzania, unategemea ili kufikia maendeleo yanayoonekana na yanayowagusa wananchi wote.
Kwa upande wake, Mwalimu Samson Sombi anasema rushwa imeendelea kuwa adui wa maendeleo, ikipunguza ufanisi wa taasisi za umma na kuondoa imani ya wananchi kwa serikali.
Anasema kauli ya Rais ya kuelekeza nguvu katika mapambano dhidi ya rushwa ni utayari wa Serikali kuzuia mianya inayosababisha upotevu wa rasilimali za umma.
Hata hivyo, anasema utekelezaji wa juhudi hizo utahitaji uthabiti, ufuatiliaji wa karibu na kuweka mifumo madhubuti ya uwazi ili kuhakikisha wahusika wote wanawajibishwa bila upendeleo.
“Changamoto ya uzembe na kufanya kazi kwa mazoea imekuwa ikidhoofisha utendaji katika idara nyingi za umma.
“Wafanyakazi wanaofanya kazi bila ubunifu, bila ufuatiliaji na bila kujali matokeo wanakwamisha dhamira ya Serikali ya kutoa huduma bora. Rais anawakumbusha watumishi wa umma kuwa wajibu wao kwa wananchi ni msingi wa utumishi wao,” anasema.
Mbali na hayo, Sombi anasema mageuzi ya mashirika ya umma kuelekea 2030 yanaonyesha dira pana ya Serikali ya kuongeza ufanisi, tija na ushindani.
Anasema mageuzi hayawezi kufanikiwa endapo utamaduni wa kufanya kazi kwa mazoea utaendelea.
Mtaalamu wa sayansi ya siasa ambaye hakutaka kutajwa jina, anasema kauli ya Rais kuhusu kudhibiti uzembe na rushwa ni yenye mwelekeo mzuri, lakini changamoto hizo zimejikita ndani ya mifumo ya utendaji wa Serikali, hivyo kunahitajika mbinu mahsusi za kimfumo ili kuzitatua kikamilifu.
Anasema watumishi wa Serikali kwa kawaida hupanda vyeo hatua kwa hatua kuanzia Mtendaji wa Kata, Tarafa hadi kufikia nafasi ya Mkurugenzi, hivyo ni rahisi kufahamu historia, maadili na mienendo yao.
“Lakini unapopata mtu ambaye ametokea nje ya mfumo, kwa mfano, mgombea ubunge aliyeshindwa kisha akateuliwa kuwa Mkurugenzi, unakuwa humfahamu vizuri. Ni vigumu kumdhibiti kwa sababu hujui maadili yake wala tabia zake,” anasema.
Mchambuzi huyo amesisitiza kuwa suluhisho la msingi ni kujenga mfumo madhubuti wa uwajibikaji kwa watumishi wa umma na kuweka utaratibu thabiti wa kuhakikisha kuwa watu wasiokuwa na rekodi wazi ya maadili hawaingii kwenye mifumo ya Serikali.
Anaongeza kuwa utekelezaji wa maagizo ya Rais unaweza kuwa mgumu iwapo hautaambatana na mabadiliko ya kimfumo ambayo yataweza kushughulikia kwa ufanisi mienendo na tabia za watumishi wote wanaoonyesha viashiria vya uzembe na rushwa.
Prince Mwaihojo, mchambuzi wa masuala ya utawala, anasema kauli ya Rais kuhusu kudhibiti rushwa na kurejesha nidhamu serikalini ni hatua muhimu inayodhihirisha dhamira ya kweli ya kuimarisha uadilifu na uwajibikaji katika utumishi wa umma.
Anasema uzembe utakomeshwa kupitia mabadiliko ya kimfumo yatakayofunga mianya ya upendeleo, ukosefu wa uwajibikaji na utaratibu usiozingatia maadili katika utoaji wa madaraka.
“Mabadiliko ya nidhamu serikalini yanahitaji mfumo madhubuti wa usimamizi wa watumishi, kuimarishwa kwa vyombo vya ufuatiliaji na kuweka mazingira salama kwa wanaotoa taarifa za vitendo vya rushwa,” anasema.
