Dar es Salaam. Serikali imewataka vijana kuwa makini pindi wanapopata fursa za kazi nje ya nchini huku ikibainisha kuwapo kwa taarifa za baadhi yao kutumika kufanya kazi za uhalifu wa mtandaoni au vitendo vya uhalifu kupitia magenge yenye silaha.
Ofisa Uchunguzi Mkuu wa Sekretarieti ya Kuzuia Biashara Haramu ya Binadamu chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Selestine Makoba ametoa kauli hiyo leo Desemba 3, 2025 katika mkutano wa wadau unaolenga kujadili kwa pamoja namna ya kudhibiti usafirishaji haramu wa binadamu.
Alitumia nafasi hiyo kutoa wito kwa vijana kuhakikisha kuwa fursa zote za kwenda kufanya kazi nje ya nchi zihakikiwe na taasisi husika kabla ya utaratibu wowote kufanyika.
“Kuna nchi ambayo tunaijua vijana wanatumika kufanya uhalifu wa kimtandao, magenge ya uhalifu wa kutumia silaha na makundi mengine ya uhalifu hivyo nawaasa vijana kutumia nafasi ya kwenda kwenye taasisi au mamlaka husika kujiridhisha kuwa kule wanapokwenda au walipopata fursa ya kujitafutia riziki zao, kwani usafirishaji haramu wa binadamu bado unaendelea na sisi tumezidisha juhudi za kupambana nao,” amesema.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili kwa maofisa wa sheria, waendesha mashtaka na mahakimu amesema elimu zaidi kwa umma inahitajika haraka ili kuimarisha vita dhidi ya biashara haramu ya binadamu.
“Ili kukabiliana na changamoto hizi, Serikali imechukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kuanzisha kitengo mahususi cha Kupambana na biashara haramu ya binadamu ndani ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.”
“Pia tumefanya marekebisho ya sheria ya kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu hivi karibuni ambayo yanaleta adhabu kali zaidi kwa wakosaji na kutambua waajiri, wakiwemo watumishi wa umma, kama wahusika wanaowajibika wakati ulanguzi unafanyika chini ya ulinzi wao,” amesema.
Amesema kupitia marekebisho ya sheria yaliyofanyika yameondoa kipengele cha mtu kulipa faini kukwepa kifungo na badala yake mtu atapewa adhabu ya kifungo huku faini ikiwa ni kama nyongeza.
Ili kukomesha biashara hiyo pia Serikali imeandaa mipango kazi ya kitaifa ya miaka mitatu wa mwaka 2025 hadi 2028 ikiwa ni baada ya mpango wa mwaka 2021–2024 kukamilika.
“Maandalizi yake yameshakamilika, unatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni,” amesema.
Katika kuunga mkono jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali, Mkurugenzi wa Mpango wa Misaada Tanzania (TRI), Edwin Mugambila amesema tangu mwaka 2014 wamekuwa wakiisaidia serikali kubaini mapungufu ya kisheria na kupendekeza marekebisho ili kupunguza mianya ya sheria ya kuzuia usafirishaji haramu wa binadamu.
“Sheria imepitiwa upya na sasa ni imara na inaendana na viwango vya kimataifa. Suala la usafirishaji haramu wa binadamu linaingia katika sekta zote na linahitaji hatua za Pamoja,” amesema Rugimbana.
Amesema ili kufikia malengo ya Pamoja ni muhimu kujenga uwezo na kubadilishana uzoefu ili kuongeza mwitikio wa kitaifa kwani Tanzania inabaki kuwa chanzo na njia ya kupitia waathirika wa usafirishaji haramu wa binadamu.
“Jamii za vijijini na kaya maskini ambako elimu ni ndogo ndizo zilizo hatarini zaidi na kudanganywa kwa urahisi na ahadi za uongo,” amesema.
Amesema takwimu za sasa zinaonyesha kuwa mikoa kadhaa ya Kanda ya Mashariki ikiwemo Morogoro na Dar es Salaam ni chanzo kikuu huku Kanda ya Ziwa inayojumuisha mikoa ya Kagera, Mwanza, Geita na Mara ikiwa njia za kupita na maeneo ya lango na imeathirika kwa kiasi kikubwa.
Pia Kanda ya Kusini yenye mikoa ya Mbeya na Songwe na Mikoa ya Mipaka kama Tanga, Horohoro, Kilimanjaro na Arusha zote zina sehemu nyingi za mipaka hivyo kuweka urahisi wa biashara hiyo kufanyika.
Licha ya hali kuwa hivyo amesema mashtaka bado ni kikwazo kikubwa kwani ni kesi chache hufika kortini na zinapofika wahalifu mara nyingi hushtakiwa kwa makosa madogo au kutozwa faini kati ya Sh200,000 na Sh500,000 kabla ya kuachiliwa.
“Lazima tujifunze kutokana na mapungufu yetu ili kusambaratisha mitandao inayowalenga vijana wetu wengine wenye umri wa miaka 12,” amesema.