Trump apiga ‘stop’ maombi ya uhamiaji kwa raia wa nchi 19

Dar es Salaam. Serikali ya Rais Donald Trump imesimamisha kwa muda usiojulikana maombi yote ya uhamiaji kutoka nchi 19, hatua iliyoibua sintofahamu nchini Marekani na duniani kwa ujumla.

Hatua hiyo inajumuisha maombi ya ukaazi (green card) na uraia, kwa wahamiaji kutoka nchi 19 zilizowekewa marufuku ya kusafiri mapema mwaka huu.

Marufuku hiyo inawahusu raia wa Afghanistan, Myanmar, Chad, Jamhuri ya Congo (Congo-Brazzaville), Equatorial Guinea, Eritrea, Haiti, Iran, Libya, Somalia, Sudan na Yemen.

Raia wa Burundi, Cuba, Laos, Sierra Leone, Togo, Turkmenistan na Venezuela wanakabiliwa na vikwazo vya kupunguzwa au kuzuiwa upatikanaji wa huduma za uhamiaji nchini Marekani.

Hatua hii ni sehemu ya mabadiliko ya sera za uhamiaji kutokana na tukio la kupigwa risasi kwa wanajeshi wawili wa National Guard karibu na Ikulu ya White House wiki iliyopita.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Daily Mail na NPR, uamuzi huo pia umesababisha kufutwa kwa baadhi ya sherehe za viapo vya uraia kwa maelfu ya wahamiaji waliokuwa wakisubiri kukamilisha safari ya kupata uraia wa Marekani.

Vyombo vya habari nchini Marekani vinaeleza zaidi ya watu milioni 1.5 waliokuwa na maombi ya hifadhi na zaidi ya 50,000 waliopewa hifadhi awali chini ya utawala wa Joe Biden wanaweza kuathiriwa na hatua hiyo.

Katika zuio la awali lililotolewa Juni, wahamiaji waliokuwa tayari nchini Marekani hawakuathrika. Ilivyo sasa, hata waliowasili kabla ya marufuku waathiriwa.

Taarifa ya Ikulu imesema hatua hiyo imechukuliwa kutokana na tukio la wiki iliyopita la mashambulizi karibu na White House, ambako Rahmanullah Lakanwal, raia wa Afghanistan, alikamatwa kwa tuhuma za kumuua mwanajeshi wa National Guard na kumjeruhi mwingine.

Ikieleza inalinda usalama wa taifa, Serikali imezitaja nchi 19 ambazo raia wake hawataruhusiwa kuendelea na hatua yoyote ya uhamiaji.

Kwa mujibu wa Idara ya Usalama wa Ndani (DHS), watu kutoka nchi hizo hawatakamilisha maombi yao bila kufanyika ukaguzi mpya, ikiwa ni pamoja na mahojiano mapya ili kubaini iwapo wanaweza kuwa tishio kwa usalama.

Taarifa ya idara hiyo inasema: “Kutokana na changamoto zilizobainika na tishio kwa wananchi wa Marekani, tumedhamiria kufanya uchambuzi wa kina, mahojiano mapya au ya ziada kwa wahamiaji wote kutoka nchi hizi waliowasili nchini baada ya Januari 20, 2021.”

Maelekezo ya ndani ya Idara ya Uhamiaji yamesisitiza kusimamisha utoaji wa kadi za ukaazi (green cards), mahojiano ya uraia, mahojiano ya kubadilisha hadhi ya ukaazi na sherehe za viapo vya uraia.

Akizungumza kupitia mtandao wake wa Truth Social, Trump amesema Marekani inahitaji ‘kupumua’.

Amesema atachukua hatua zaidi ikiwa ni pamoja na kusimamisha kabisa uhamiaji kutoka nchi za dunia ya tatu.

Waziri wa Mambo ya Nje, Kristi Noem, ametangaza kuwa Serikali inapanga kupanua marufuku hiyo hadi mataifa zaidi ya 30.

Amesema baadhi ya nchi zinatuma wauaji, watu wanaotegemea kodi za Wamarekani na wanaojipenyeza kwa ajili ya kujipatia manufaa ya haraka.

Hata hivyo, mashirika ya kutetea haki za wahamiaji yamesema hatua hiyo ni ubaguzi unaoendeshwa kwa misingi ya utaifa, huku wengine wakisema itawazuia watu waliokuwa tayari wanachangia katika jamii.

Hatua hii imefikiwa wakati kukiwa na ongezeko la matamshi makali dhidi ya wahamiaji, hasa kutoka Afrika na Mashariki ya Kati, jambo linalozua hofu ya kuvuruga uhusiano na jamii mbalimbali nchini humo.

Kwa mtazamo wa wachambuzi, mabadiliko haya ya sera yanaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa watu wanaotoka mataifa yenye migogoro.

Baadhi ya wataalamu wanaonya kuwa, uamuzi huo unaweza kuleta kesi nyingi mahakamani na mgawanyiko zaidi katika jamii.