Tutuba: Wahasibu nguzo muhimu kufanikisha dira 2050

Dar es Salaam. Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, amewataka wahasibu na wakaguzi wa hesabu nchini kuchukua nafasi ya kipekee katika kuiwezesha Tanzania kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ya kujenga uchumi wa dola trilioni moja, akisema taaluma ya uhasibu kisasa ndiyo injini ya uendelevu, uwajibikaji na ushindani wa Taifa kwa muda mrefu.

Akizungumza leo Desemba 3,2025 wakati akifungua mkutano mkuu wa wahasibu, Tutuba amesema taaluma hiyo imepanuka zaidi ya kazi za kihasibu za jadi na sasa imekuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya uchumi wa taifa.

Amesema wahasibu na wakaguzi wa hesabu ni wanazuoni wa takwimu, washauri wa kimkakati na walinzi wa uwajibikaji ambao uamuzi wao unaathiri uthabiti wa uchumi na kuimarisha imani ya wawekezaji.

Akitoa mwelekeo wa mwenendo wa uchumi wa Taifa, Tutuba amesema Tanzania inaendelea kufanya vizuri na iko katika nafasi nzuri kusonga mbele kuelekea malengo yake ya muda mrefu.

Kwa mujibu wake pato la Taifa (GDP) limeongezeka kutoka asilimia 4.7 mwaka 2022 hadi 5.5 mwaka 2024, mfumuko wa bei ulishuka kutoka asilimia 4.6 (2022) hadi 3.2 (2024), chini ya wastani wa dunia wa 4.7, mikopo chechefu (NPLs) imeshuka kutoka asilimia 8 (2022) hadi 3.5 (2024) hadi 3.3 kufikia Septemba 2025.

Akiba ya fedha za kigeni imeongezeka kutoka dola bilioni 4.8 (2022) hadi dola bilioni 5.7 (2024) na kufikia dola bilioni 6.7 kufikia Septemba 2025.

Akiba ya dhahabu imefikia tani 15.2, hatua inayochangia uthabiti wa shilingi na kuimarisha imani ya wawekezaji.

Riba za mikopo ya kibiashara zimepungua kutoka asilimia 17.5 (2022) hadi 15.8 kufikia Septemba 2025.

“Viashiria hivi vinaonyesha mazingira thabiti ya uchumi yanayowezesha sekta binafsi kukua. Ni jukumu la wahasibu kutafsiri takwimu hizi na kuiwezesha nchi kubadilika kuelekea uchumi imara, wa kisasa na unaotumia teknolojia,” Amesema.

Akizungumza kwenye mkutano huo Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), Profesa Sylvia Temu, amesema taaluma hiyo inapaswa kuongoza kwa ubunifu, uongozi madhubuti na viwango vya juu vya maadili wakati Taifa likiingia katika awamu mpya ya mageuzi ya kimfumo.

Amesema wahasibu wana nafasi ya kuongoza utekelezaji wa malengo ya Dira ya Taifa 2050 kwa kusimamia uwazi na uwajibikaji katika taasisi za umma na binafsi.

“Kwa ushiriki hai na ubadilishanaji maarifa, taaluma ya uhasibu itaendelea kuielekeza nchi kwenye mustakabali jumuishi na imara,” amesema.

Profesa Temu amesema mkutano huo unajadili mabadiliko na fursa katika taaluma hiyo, ikiwemo maendeleo ya teknolojia, akili mnemba (AI) na ongezeko la umuhimu wa taarifa za uendelevu.

Aliongeza kuwa athari za Covid-19 zilionyesha umuhimu wa mifumo ya kisasa inayotumia teknolojia na kwa kutambua hilo NBAA imewekeza katika mageuzi ya kidijitali, ikiwa ni pamoja na kuboresha mfumo wa usajili, kutoa leseni na mafunzo endelevu mtandaoni, pamoja na kuimarisha maktaba mtandaoni inayowezesha upatikanaji wa maarifa kwa wakati.

Katika mkutano huo, NBAA na BoT walisaini hati ya makubaliano (MoU) ya miaka mitano, kuanzia  Desemba 3, 2025 hadi  Desemba 2, 2030, yenye lengo la kuimarisha ushirikiano katika kubadilishana taarifa, kujenga uwezo na kukuza maendeleo ya kitaaluma.

Taasisi hizo zimekuwa zikishirikiana kwa muda mrefu katika kutoa mafunzo kwa wahasibu, wakaguzi, wataalamu wa kodi na masuala ya fedha. Makubaliano hayo mapya yanapanua wigo hadi maeneo mapya kama taarifa za uendelevu na ujumuishaji wa mifumo ya kidijitali.

Makubaliano hayo pia yanaunga mkono utekelezaji wa mfumo mpya wa NBAAVN, unaotoa namba maalum za utambuzi kwa taarifa za kifedha  hatua muhimu ya kutokomeza wahasibu vishoka na kuimarisha uadilifu wa taarifa za fedha.

Zaidi ya washiriki 4,500 wanahudhuria mkutano huo wa siku tatu, unaotarajiwa kufikia tamati Desemba 5, ambapo washiriki watatembelea vivutio vya utalii Pugu na Kazimzumbwi na kupanda zaidi ya miti 600 kama sehemu ya kuchochea uendelevu wa mazingira.