Wananchi wapaza sauti changamoto ya daraja

Pemba. Wananchi wa vijiji vya Ng’wambwa na Vikunguni, Mkoa wa Kusini Pemba wameiomba Serikali kukamilisha ujenzi wa daraja ambalo limekuwa kero kwa wananchi, hususani kipindi cha mvua.

Kwa mujibu wa wananchi, daraja hilo linalounganisha mawasiliano ya vijiji hivyo viwili limekuwa hatarishi hasa nyakati za mvua, kwani huwawia vigumu kuvuka kupitia daraja hilo.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti leo Jumatano Desemba 3, 2025 wamesema wameanza ujenzi wa daraja hilo kwa nguvu zao kutokana na adha wanayopata wanafunzi, ambao kuna nyakati hukosa masomo.

Abdalla Juma Ali, Mkazi wa Kijiji cha Ng’wambwa, amesema baada ya kukabiliwa na adha hiyo, waliamua kushirikiana kujenga daraja hilo.

“Tumeamua kufanya hivyo baada ya kutafuta wafadhili wenye uwezo wa kutusaidia bila ya mafanikio, ndiyo sababu ya kuchangishana wanakijiji kuanza ujenzi kwani watoto wetu wanakosa masomo kipindi cha mvua, hawawezi kuvuka,” amesema.

Ameiomba Serikali kuwasaidia kukamilisha daraja hilo, akieleza hawana uwezo wa kuendelea kulijenga.

Amesema hatua waliyofikia ni nzuri, hivyo wanahitaji nguvu za wahisani kuwasaidia ili nguvu zao zisiende bure.

Kwa upande wake, Khamis Ali Juma, amesema baada ya kuona nguvu zao zimeishia njiani waliutafuta uongozi wa wilaya ili kuangalia namna ya kupata msaada na maelekezo yatakayosaidia kumaliza kero hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Chakechake, Mgeni Khatib Yahya, amesema Serikali ya wilaya itasaidia na kusimamia kwa karibu mradi huo ili ukamilike na kuwaondolea usumbufu wananchi.