Dar es Salaam. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imewakamata watuhumiwa wawili wakiwa na dawa mpya za kulevya zinazodaiwa kutumika kwenye matukio ya uhalifu kutokana na uwezo wake wa kusababisha usingizi ndani ya muda mfupi, kufuta kumbukumbu na kusisimua mwili.
Hii ni mara ya kwanza nchini kukamatwa dawa hizo aina ya 3,4 Methylenedioxymethamphetamine (MDMA) vidonge 738, vyenye uzito wa gramu 177.78, pamoja na dawa za tiba zenye asili ya kulevya aina ya Rohypnol (flunitrazepam) vidonge 24, vyenye uzito wa gramu 10.03.
Watuhumiwa hao, Cuthbert Kalokola (34) na Murath Abdallah (19), ambao ni wapenzi, walikamatwa na dawa hizo eneo la Sinza D, jijini Dar es Salaam katika operesheni iliyofanywa na DCEA, baada ya kupata taarifa kuhusu uwepo wa dawa hizo za kulevya.
Akizungumza na Mwananchi leo, Jumatano, Desemba 3, 2025, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema baada ya kupata taarifa hizo, uchunguzi ulianza na walifanikiwa kumkamata Kalokola ambaye alimtaja Murath.
“Kalokola alitupeleka hadi kwenye nyumba aliyekuwemo Murath, ambaye baada ya kumkamata na kumhoji, ikaonekana mzigo huo ni wa Kalokola, lakini kwa sababu tuliwakuta wakiishi pamoja, wote wanawajibika katika hili.
“Huyu binti, baada ya kumhoji, alisema hafahamu chochote kuhusu dawa hizo kuwa za kulevya, kwa kile alichokuwa akielezwa na mpenzi wake, ni za maumivu,” amesema na kuongeza;
“Hapa kuna funzo kubwa kwa wanawake: usijiingize kwenye uhusiano na mtu ambaye hujui anafanya nini. Huyu ni binti mdogo, alikuwa anatoroka kwao, anaenda kwa mpenzi bila kujua anafanya biashara ya dawa za kulevya.”
Kamishna Jenerali Lyimo amesema baada ya kuhojiwa Kalokola, alikiri kuingiza dawa hizo nchini kutokea Uingereza, akizipitisha Kampala, Uganda, kabla ya kuziingiza kwa njia za panya.
“Huyu alikuwa anaishi Uingereza na ndiko alikoingia kwenye mtandao wa matumizi na biashara ya dawa hizo. Sasa alivyokuja nchini, alikuja nazo chache, lakini akaona kuna watu wengi wanaozihitaji, hivyo akaanza kuziingiza kibiashara, akizipitisha nchi jirani.
“Akawa anazishusha Kampala, zinasafiri hadi mpakani ambapo hazipiti kwenye ukaguzi, anayezibeba anampa bodaboda ambaye atazipitisha njia za panya, kisha yeye anavuka na kuupokea mzigo huo. Hapo zinakuwa zimeshaingia nchini,” amesema.
Kwanini dawa hizi ni hatari
Akizungumzia namna ya kukabiliana na dawa hizo zinapoingia mwilini, Dk Peter Mfisi ambaye pia ni Kamishna wa Kinga na Tiba wa DCEA amesema kuna dawa mpya za kulevya zinazodhibitiwa na methadone, lakini nyingine hadi sasa hakuna dawa ya kuzidhibiti.
“Hizi dawa inategemea zinatoa mwitiko gani kwenye mwili zinapotumika, kuna zile ambazo zina vichangamshi na zipo zinazolegeza mwili sasa kwa sababu dawa hizi zinatengenezwa kwa kuchanganywa zipo ambazo hadi sasa hazijapata tiba ya kuzipoza hasa zikitumika mara kwa mara na kutengeza uraibu.
“Hizo ambazo hulaza mfano MDMA mara nyingi mhusika anaweza kuamka baada ya saa kadhaa na akawa na kiwewe kidogo lakini baadaye akarudi katika hali ya kawaida,” amesema Dk Mfisi.
Tovuti ya Drugs.com inazitaja MDMA na Rohypnol kuwa ni miongoni mwa dawa hatari zaidi kwa vijana kwa sababu ya athari za haraka na za muda mrefu zinazoambatana na matumizi yake.
MDMA inatajwa kuongeza joto la mwili kupita kiasi (hyperthermia) na kusababisha figo kushindwa kufanya kazi au moyo kusimama ghafla.
Dawa hiyo pia huathiri mfumo wa fahamu kwa kuharibu kemikali za ubongo, hivyo kusababisha msongo wa mawazo, wasiwasi, kupoteza kumbukumbu na kushuka kwa uwezo wa kufanya maamuzi.
Kwa upande wa Rohypnol, hii ni dawa ya usingizi yenye nguvu kubwa ambayo imepigwa marufuku katika nchi nyingi kutokana na matumizi mabaya.
Pia, matumizi kupita kiasi ya dawa hizo husababisha kupooza kwa mfumo wa kupumua, jambo linaloweza kusababisha kifo.
Kamishna Jenerali Lyimo amesema matumizi ya dawa hizo huweza kuongeza hatari ya shinikizo la damu na mshtuko wa moyo, na ikitokea dozi imetumika kubwa, husababisha vifo vya ghafla.
“Dawa hizi pia husababisha usingizi mzito, kupoteza fahamu na kukosa kumbukumbu ya matukio, inasababisha uraibu ndani ya muda baada ya kutumiwa. Pia wapo wanaotumia kuchangamsha mwili kwa kile wanachoaminishwa kwamba zinaongeza nguvu za kiume.
“Tulipomhoji mtuhumiwa amesema wateja wake ni wengi, anawapata kwenye hoteli kubwa. Wapo wanaotumia dawa hizi kufanya uhalifu, ikiwemo matukio ya utapeli na ubakaji, hivyo watu wanapaswa kuchukua tahadhari,” amesema.
“Inaweza kutokea umepanga kukutana na mtu kwa ajili ya biashara, akifanikiwa kukuwekea kidogo tu kwenye kinywaji, utapoteza fahamu. Wanawake wapo hatarini zaidi kwa sababu unaweza kufanyiwa ukatili wa kingono na usiwe na kumbukumbu za aliyekufanyia hivyo,” amesema.
Katika operesheni iliyofanyika eneo la Mbezi Maramba Mawili, watuhumiwa Jaribu Tindwa (38), Ally Meshe (39), Juma Mfamo (20), Rahim Nampanda (28), Abubakari Ally (20), Nurdin Rashid (36) na Farid Rashid (33) walikamatwa wakiwa na kilogramu 90 za dawa za kulevya aina ya skanka, zikiwa zimefichwa ndani ya matanki ya solar panel zilizokuwa zimepakiwa kwenye basi linalofanya safari zake kati ya Tanzania na Malawi.
Vilevile, mkoani Rukwa katika mpaka wa Kasesya, alikamatwa Godwin Andrew (26), mkazi wa Mbalizi, Mbeya, akiwa na dawa za kulevya aina ya skanka zenye uzito wa kilogramu 244.3.
Dawa hizo zilikuwa zimefichwa ndani ya spika, mashine za kupooza hewa, mashine za kukatia majani na vifaa vya kompyuta (CPU).
Vifaa hivyo vilikuwa vikisafirishwa katika gari aina ya Iveco Van, yenye namba za usajili wa nchi ya Afrika Kusini CN 85 FN GP, mali ya kampuni ya usafirishaji ya Makamua Logistics Limited, lililokuwa likitokea nchini Afrika Kusini kuja Dar es Salaam.
Mali za Sh3.3 bilioni zataifishwa
Katika hatua ya kukabiliana na uhalifu wa dawa za kulevya, Mahakama Kuu, divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, imetoa uamuzi wa kutaifishwa kwa mali zenye thamani ya Sh3.3 bilioni.
Mali hizo, ambazo ni nyumba nne, viwanja sita na magari 11, zilithibika kupatikana kutokana na biashara ya dawa za kulevya zikimilikiwa na Saleh Basleman na Gawar Fakir.
Utafishaji wa mali hizo umefanyika chini ya Sheria ya Mazao ya Uhalifu, Sura ya 256, pamoja na Sheria ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa, Sura ya 200, na Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Namba 5 ya mwaka 2015.
Akizungumzia hilo, Kamishna Jenerali Lyimo amesema maombi ya kutaifishwa kwa mali hizo yaliwasilishwa mahakamani kufuatia uchunguzi uliofanyika na kubainika kuwa mali hizo zilipatikana kwa njia ya uhalifu ya dawa za kulevya.
“Utaifishaji huu umefanyika kisheria ili kuifundisha jamii kuwa uhalifu hauna faida, na adhabu za kifungo hazitoshezeli hasa katika makosa ya kupanga, ikiwemo yanayohusisha dawa za kulevya. Huu ni mkakati wa kuzuia uhalifu kuendelea na kuondoa matamanio ya kufanya uhalifu,” amesema Lyimo.
