Carter; Sokwe mkongwe mwenye hekima msituni

Mahale. Carter ni mmoja wa sokwe wakongwe wanaopatikana ndani ya Hifadhi ya Taifa Milima Mahale magharibi mwa Mkoa wa Kigoma, akiwa na umri wa miaka 40. Sokwe huyo ni mtoto wa sokwe jike maarufu kwa jina la Calliope, aliyefariki mwaka 2009 akiwa na miaka 51. 

Carter alikuwa na ndugu zake wawili, wa  kiume mmoja; Cadmas, aliyefariki mwaka 2010 akiwa na miaka 18 baada ya kushambuliwa na aliyekuwa kiongozi wa kundi wakati huo (Alpha Male) aitwaye Pimu, na ndugu wa kike mmoja aitwaye Carmen, ambaye aliamua kuhama familia baada ya kutimiza umri wa miaka 11. 

Kwa sasa Carter amezeeka na ni babu mlezi, mtulivu, mwema na anayependa kukaa karibu zaidi na watoto kuliko madume wenye nguvu wanaoongoza kundi lake la Sokwe wa Mahale. 

Wakati nyingi huonekana akitembea kwa utulivu ndani ya kundi kubwa la sokwe, akifurahia maisha ya amani anayoyaishi na jamii ya kundi lake. Na nyakati zingine hupendelea kupata utulivu wa kujitenga na vurugu ambazo husababishwa na madume wa kundi lake.

Kucheza na watoto wenye miaka kati ya minne ama mitano ndio kama sehemu ya tabia yake ya kila siku. 

Pia, hupenda kukaa na watoto, kuwatazama na kucheza nao huku akitengeneza uhusiano wa kipekee unaowafanya watoto kumpenda na kumfuata kila mara. 

Madume wengi wa Sokwe katika umri wa kati ya miaka 20 na 30 huepuka kucheza na watoto wakihofia kutoheshimiwa na watoto kwenye jamii ya koo zao.

Ingawa ni dume aliyewahi kufika nafasi ya tano katika uongozi wa ukoo wake, hajawahi kufika uongozi wa juu. Tangu akiwa kijana, Carter hajawahi kupenda mabishano, makabiliano au misuguano. 

Sokwe huyo hapendi ugomvi hali iliyomfanya kutokuwa na majeraha makubwa mwilini mwake ikiwa ni ishara  kuwa amekuwa na maisha ya kuepuka migogoro. 

Kitu pekee unachoweza kukiona kwa Carter ni makovu ya michubuko michache tu ambayo aliipata akiwa na umri wa miaka 30 kwenye jitihada zake za kupambania sokwe jike wakiwa katika kipindi cha kupandwa.

Nyakati pekee ambazo Carter huonyesha msimamo mkali ni pale anapozungukwa na kundi la majike watupu, ambapo hutoa ishara ya kuunguruma kama utambulisho wa uwezo wake, bila kuanzisha vita wala kumuumiza yeyote na baadaye hujituliza zake anapoona dume lingine limesogea eneo hilo.

Hali hiyo humsaidia kupata majike pindi yanapokuwa kwenye joto. Dume hufanya vurugu kwa majike wakiwa katika hali ya kawaida jambo ambalo humsaidia kufanikisha kuwapata majike kirahisi wakiwa kwenye hali ya joto.

Kwa sasa Carter ndio sokwe dume mwenye umri mkubwa kuliko wote walioko kundi la sokwe wa Mahale. Sokwe hufikia umri wa miaka 50 hadi 55 wakiwa mazingira yao asilia (msituni) na umri wa zaidi ya miaka 60 wakiwa maeneo ya bustani za wanyama. 
Sokwe mwenye umri mkubwa kuliko wote duniani ni Joao mwenye umri wa miaka 81, anayeishi kwenye Bustani ya Sokwe “Chimp Eden” iliyopo nchini Afrika Kusini. 

Sokwe wa Mahale ni hazina ya utalii ambayo inaleta mapato kwa Taifa, inaimarisha uchumi wa jamii zinazozunguka hifadhi na kuongeza ajira kwa Watanzania. 

Kwa kuhakikisha usalama wao leo, tunalinda urithi wa kisayansi, kitamaduni na kiuchumi utakaoendelea kunufaisha kizazi hiki na kijacho.

Milima ya Mahale ni milima ambyo ni moja ya hifadhi katika nchi ya Tanzania. Hifadhi hii iko magharibi mwa Tanzania ikiwa inapakana na Ziwa Tanganyika. Hifadhi hii inaundwa na vilima vilivyojipanga na kufunikwa na misitu minene ikiwa na jumla ya kilometa za mraba  takribani 1,613.