KOCHA Mkuu wa Mtibwa Sugar, Yusuf Chipo amesema suluhu dhidi ya JKT Tanzania imechangiwa na nidhamu nzuri ya kiuchezaji kwa wachezaji pale ikiwa na mipira au inapoipoteza mbele ya maafande hao.
Ni suluhu ya pili kwa Chipo tangu ameanza kuisimamia Mtibwa Sugar alianza dhidi ya KMC, akaambulia pointi tatu dhidi ya TRA United kwa timu kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 na juzi suluhu na JKT Tanzania.
Akizungumza na Mwanaspoti, Chipo amesema timu hiyo inaendelea kuimarika kiuchezaji kadri inapopata mechi za ushindani nidhamu ya kulinda na kushambulia inaendelea kujengeka huku akisisitiza kuwa bado kutumia nafasi wanazotengeneza.
“Timu ili iwe bora inahitaji kuwa na nidhamu ya kiuchezaji naiona hiyo kwa wachezaji wangu wakiwa na mpira na hata mpira ukiwa kwa wapinzani nafikiri kilichobaki ni kutumia nafasi wanazotengeneza lakini kwenye uzuiaji wanawanya kile tunachoelezana uwanja wa mazoezi,” amesema kocha huyo raia wa Kenya na kuongeza;
“Safu ya ushambuliaji inapitia nyakati ngumu ni kitu ambacho kila mmoja anakiona timu imecheza dakika 180 hakijafunga bao hata moja hii sio sawa kwetu kutokana na kuwa na matarajio makubwa ya kumaliza nafasi nzuri kwenye msimamo tunatakiwa kuendana na ushindani wa wapinzani.”
Chipo amesema bado anaendelea kuiboresha timu hiyo ili iingii kwenye ushindani kulingana na aina ya mpinzani wanaekutana naye lengo kubwa ni kuhakikisha wanakuwa miongoni mwa timu bora na shindani.
Mtibwa Sugar hadi sasa imecheza mechi nane na kukusanya pointi 10 baada ya kushinda mbili, sare nne na kupoteza mbili, imefunga mabao manne na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara nne.
