Dk Migiro asisitiza mazungumzo kuleta Taifa pamoja

Dodoma. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dk Asha-Rose Migiro amesema huu ni wakati wa mazungumzo, kila mmoja anatakiwa kujiandaa kwa ajili ya mazungumzo.

Dk Migiro amesema mazungumzo ndiyo yatakayosaidia kuwepo amani, lakini mambo hayo yanawezekana kupitia wanawake kama wataamua.

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Desemba 4, 2025 wakati akifungua Jukwaa la Wanawake 2025 lililobeba kauli mbiu ya Mama ni Amani.

Jukwaa hilo limefanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma na kuwaleta pamoja wanawake kutoka mikoa mbalimbali na visiwani Zanzibar.

Kabla ya kufunguliwa kwa jukwaa hilo, ilioneshwa makala ya video kuhusu yaliyotokea Oktoba 29, 2025 na kutajwa kwa takwimu ya mali zilizoharibiwa.

Katika hotuba fupi aliyoitoa, Katibu Mkuu amesema huu ni wakati wa kuwa na mazungumzo yatakayosaidia utulivu na amani katika kuirejesha Tanzania kwenye sifa iliyozoeleka duniani kwa miaka mingi.

Dk Migiro amesema Taifa hili ni la vijana kwa kuwa,Β  asilimia kubwa ni vijana, lakini ifahamike kuwa wanatoka kwenye mikono ya wanawake, hivyo ni wajibu wao kuhakikisha vijana wanafahamu na kuelewa vema umuhimu wa amani.

Katibu mkuu amesema utamaduni wa Watanzania siku zote ni kuweka amani mbele akitaka utamaduni huo uendelee ukianzia kwa wanawake.

Mwanasiasa wa siku nyingi na mwanamke wa kwanza kuwa mbunge wa jimboΒ  mwaka 1980, Kate Kamba amesema mama ni mlezi wa kwanza na ndiyo mwalimu, hivyo haipaswi kukwepa wajibu wake yanapotokea hayo.

Kate amesema bila kuwekeza katika mambo yenye misingi mizuri, Taifa litapotea lakini wanawake wakiamua kulisimamia kupitia kwa vijana hao, Tanzania itaendelea kuwa mfano katika suala la amani.

Sifa Swai amesema ulinzi wa amani umehamia katika matumizi ya mitandao ambako mara nyingi taarifa potofu zinaanzia huko na mwisho wa siku watoto wanapoteza mwelekeo.

Swai ambaye ni mwanamke wa kwanza kuteuliwa kuwa mweka hazina wa CCM, amesema biashara za wanawake zikiyumba husababisha watoto kupoteza mwelekeo na matokeo yake ndiyo mambo yanayotokea sasa.