DRC, Rwanda kusaini mkataba wa amani mbele ya Trump

Viongozi wa mataifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Rwanda wako Washington, Marekani kwa ajili ya kusaini makubaliano ya amani yanayolenga kumaliza mgogoro wa muda mrefu katika eneo la Mashariki ya DRC, kwa mwaliko wa Rais wa Marekani, Donald Trump.

Rais wa DRC, Félix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda, Paul Kagame wamekuwa wakirushiana maneno mara kwa mara katika miaka ya hivi karibuni, kila mmoja akimshutumu mwenzake kwa kuanzisha mzozo huo katika eneo hilo.

Siyo mara ya kwanza kwa viongozi hao kukutanishwa kwa lengo la kutafuta suluhisho katika mzozo huo, hata hivyo jitihada hizo hazijasaidia chochote kwani mapigano yameendelea kufanyika huko mashariki mwa DRC.

Juhudi za upatanishi zilianza kufanywa na Rais wa Angola, João Lourenço ambaye alikuwa akikutana na viongozi hao kwa nyakatio tofauti, hata hivyo hakufanikiwa. Jumuiya za kikanda, pia, zilifanya jitihada zao bila mafanikio.

Mkataba wa mwingine ulisainiwa huko Qatar kati ya Serikali ya DRC na waasi wa M23 ambao wameshikilia miji kadhaa ya Mashariki mwa DRC.

Tayari Tshisekedi na Kagame wako Marekani kuitikia wito wa Trump ambaye siku za nyuma alibainisha kwamba ana mpango utakaoleta amani ya kudumu nchini DRC na ukanda wa maziwa makuu.

Kuelekea mkutano huo, BBC imeripoti kwamba kumekuwa na ongezeko la mapigano katika eneo la mashariki mwa DRC lenye utajiri wa rasilimali, kati ya majeshi ya serikali na waasi wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda.

Jeshi la DRC liliwashutumu wapinzani wao kwa kujaribu kuhujumu mchakato wa amani, lakini waasi wa M23 walisema jeshi ndilo lililoanzisha mashambulizi kinyume na makubaliano ya kusitisha mapigano.

Mwanzoni mwa mwaka huu, waasi wa M23 waliteka maeneo ya mashariki mwa DRC katika mashambulizi yaliyosababisha maelfu ya watu kuuawa na wengine wengi kulazimika kuyakimbia makazi yao.

Tshisekedi na Kagame sasa watayathibitisha, huku viongozi wengine kadhaa wa Afrika na Kiarabu, wakiwemo wa Burundi na Qatar, wakitarajiwa kuhudhuria hafla ya utiaji saini.