Kanuni mpya zao la korosho zaibua hofu kufikia malengo ya ubanguaji wa ndani

Zao la korosho nchini limeingia katika msimu wa 2025/2026 ikiwa na sura mpya ya kanuni na masharti yaliyowekwa na Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), hatua ambayo imezua hisia tofauti miongoni mwa wabanguaji wa ndani.

Wakati serikali ikisisitiza kuwa maboresho haya yanakusudia kuongeza uwazi, ufuatiliaji na thamani ya zao hilo, wabanguaji wanadai kuwa masharti mapya yameweka vikwazo katika kuwawezesha wabanguaji wa ndani kuhimili ushindani wao katika soko la kimataifa.

Katika mabadiliko ya hivi karibuni, kupitia nyongeza za Mwongozo Na.3, Bodi hiyo ya Korosho (CBT) imeweka mfumo mpya wa usafirishaji, ununuzi na malipo unaowalazimu wabanguaji kuwasilisha nyaraka za malipo kwa Chama cha Ushirika na Halmashauri kabla ya kupata Kibali cha Usafirishaji (PDN).

Licha ya kuwa mfumo huu unalenga kufuatilia mwenendo wa korosho kutoka shambani hadi kiwandani, lakini wabanguaji wanasema unachelewesha upatikanaji wa huduma muhimu ikiwemo muda wa kupata kibali cha kusafirisha korosho zao.

Akizungumzia mwongozo huo mpya, Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) Francis Alfred amesema Mwongozo huo uliandaliwa katika mazingira shirikishi ukilenga kuchochea ubanguaji wenye tija wa zao hilo kama ambavyo imekuwa ikielekezwa na serikali.

“Mwongozo huu uliandaliwa tangu mwezi wa kumi na wadau wote walishirikishwa, kama kuna mapungufu wabanguaji wanayaona tunawaomba tutakutana na wadau kwenye kikao cha tathmini badaye ili kuona changamoto zilizopo na kuzishughulikia, amesema.

Mkurugenzi huyo amesema Bodi ya Korosho inatumia vikao vyake maalumu katika kufanya mapitio ya tathmini na kufanya maboresho pale panapoonekana kuwa na uhitaji ili kukidhi matakwa ya wadau na kuchochea maendeleo ya zao la korosho nchini.

Katika mwongozo huo mpya, majukumu ya taasisi mbalimbali pia yamepangiliwa upya. Halmashauri zikipewa jukumu la kuwatambulisha wabanguaji kwa Vyama vya Union kwa AMCOS, huku CBT ndiyo hutoa kibali cha mwisho cha usafirishaji.

Alfred anasema Mwongozo uliandaliwa tangu mwezi wa kumi na wadau walishirikishwa, kama kuna mapungufu wabanguaji wanayaona tunawaomba tutakutana na wadau kwenye kikao cha tathmini badaye ili kuona changamoto zilizopo na kuzishughulikia.

Kwa upande wabanguaji, Katibu wa chama cha wabanguaji wa Korosho nchini, John Nkundwanabake anasema licha ya serikali kutoa matamko ya kutaka maboresho ya ubanguaji wa zao hilo ndani ya nchi, utekelezaji wake umekuwa mgumu kutokana na wanunuzi wengi bado hawaoneshi utayari kutokana na mazoea ya soko la wazi la awali.

“Korosho ni zao mtambuka ambalo lina wadau wengi kuanzia taasisi na vyama mbalimbali, wizara kadhaa za Serikali pia zinahusika moja kwa moja kupitia huduma zake mbalimbali zinazosimamia katika hatua tofauti za uendeshaji wa zao hili,” amesema.

Katibu huyo pamoja na kupongeza hatua za serikali kusisitiza ubanguaji wa ndani uimarishwe lakini amesema tamko hilo limebaki bila uhalisia, changamoto inabaki kuhusu namna ya kutekeleza.

“Kuanzia kwenye kibali cha kutoa gari moja unaweza kuomba leo ukasubiri siku nne hadi wiki moja kukipata, hii inafanya mfumo huu kubaki katika matamko bila utekelezaji kwani wadau wengi bado hawaoneshi utayari. Sisi kama chama tunaona haja ya wadau kukaa kuona namna bora ya kuwezesha wabanguaji wa ndani waweze kununua na kuuza bila vikwazo,

“Wadau washirikishwe katika maboresho ya miongozo ili kuondoa changamoto na kuendana na hali halisi hasa ikizingatiwa kuwa wenzetu kutoka nje wanakuja na mitaji mikubwa na wananunua korosho katika maeneo mengi sisi wabanguaji wa ndani hatuwezi kushindana nao, ni wajibu wa serikali kushirikiana na wadau wote kuona namna ya kuwezesha wabanguaji wa ndani,” ameongeza.

Kwa mujibu wake, kusafirisha korosho kwenda kubanguliwa nje hupoteza ajira nyingi kwani kubangua zao hilo huhusisha idadi kubwa ya watu, hivyo anasisitiza wito wake kwa mamlaka za zao hilo ikiwemo Bodi ya Korosho kuweka mazingira rafiki ya ubanguaji wa korosho ndani ya nchi.

“Sisi tunachosema wabanguaji wasizuiliwe kusafirisha korosho ghafi nje bali wawekewe mazingira rafiki waweze kubangua ndani kwani tunapobangua ndani tunatoa ajira nyingi sana. Kanuni za sasa ni kama wamezuiwa tu kwani taratibu za mwaka huu kwa wengi wanaona zimekuwa ngumu zaidi zikifanya mazingira ya ubanguaji wa ndani kutokuwa rafiki ” ameongeza.

Hata hivyo, wabanguaji wanadai kuwa adhabu kwa wanaokiuka utaratibu zimekuwa kali, ikiwemo faini ya Sh10 milioni na kusimamishwa leseni kwa miezi sita kwa atakayenunua korosho nje ya mfumo rasmi. Wabanguaji wanasema hatua hii inahitaji maandalizi makubwa ya mazingira ya uzalishaji kabla ya kuitekeleza.

Pia katika upande wa mauzo, mfumo mpya wa mnada, umeimarishwa kwa masharti mapya yanayomtaka mnunuzi kuwasilisha nyaraka za kodi, usajili wa kampuni, leseni ya mazao na malipo ya dhamana kulingana na kiasi cha korosho anachokusudia kununua.

Masharti hayo ya malipo yamewekewa muda mfupi wa siku tano tu kukamilisha miamala, na kushindwa kulipa ndani ya muda huo humaanisha kupoteza dhamana. Hii, kwa mujibu wa wabanguaji, inawaweka katika mazingira magumu ya kiuchumi wakati mikopo ya ndani ina riba ya asilimia 10 hadi 16 ikilinganishwa na washindani wao wa nje wanaopata mikopo ya asilimia 3 hadi 5.

Aidha, tozo mbalimbali zilizowekwa katika mfumo mpya pia zimekuwa gumzo. Wabanguaji hao wanasema, gharama hizi zinapunguza uwezo wa kubangua kwa tija na kuongeza thamani, licha ya matarajio makubwa ya serikali ya kuifikisha Tanzania kwenye ubanguaji wa kiwango cha kimataifa.

Hata hivyo, pamoja na malalamiko, sekta ya korosho inaendelea kubeba matumaini mapya. Kuanzishwa kwa soko la awali kumeondoa mianya ya kangomba, kuimarisha kukusanywa kwa ushuru na kuongeza uwekezaji kwenye viwanda vya ndani.

Serikali pia imeweka malengo makubwa ya kuongeza thamani ya korosho kwa ubanguaji wa ndani, ikiwemo kufikia ubanguaji wa tani 700,000 ifikapo 2026 na tani milioni moja ifikapo 2030. Lengo kuu ni kupunguza utegemezi wa kuuza korosho ghafi na kujenga uchumi wa viwanda wa kilimo unaohimili ushindani wa kimataifa.

Hata hivyo, kwa wabanguaji wa ndani, njia kuelekea malengo hayo bado ni ndefu. Wanasema mazingira ya sasa yanahitaji marekebisho ya kiuchumi, tozo rafiki na mifumo inayotambua uwezo halisi wa viwanda vya Tanzania, wanaonya kuwa ubanguaji wa ndani unaweza kushuka au kukwama, licha ya fursa kubwa zilizopo katika soko la kimataifa.