Kiungo Tausi FC apata dili Sierra Leone

KIUNGO wa zamani wa Tausi FC, Zuwena Aziz ‘Zizou’ amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia Mogbwemo Queens inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake ya Sierra Leone.

Kiungo anajiunga na timu hiyo akitokea Tausi ambako alidumu msimu mmoja akiipandisha chama hilo zamani likiitwa Ukerewe Queens Ligi Kuu.

Kabla ya hapo aliwahi kuzitumikia Kigoma Sisters, Baobab Queens, Thika Queens ya Kenya, Lady Doves ya Uganda, Najah FC ya Morocco na Ceasiaa Queens ya Tanzania, akitumikia nafasi zote za ulinzi. 

Akizungumza na Mwanaspoti, Zizou amesema tayari amesaini dili hilo na jana alikuwa njiani kuelekea Sierra Leone tayari kwa kuanza kazi.

“Namshukuru Mungu kwanza kwa kufanikisha dili hilo lakini kwangu mchezaji inaongeza kitu kwenye karia yangu haikuwa rahisi kwa sababu nilikuwa nje muda mrefu kabla ya kujiunga na Tausi,” amesema Zizou na kuongeza;

“Naamini nitafanya vizuri kwa sababu nishacheza nje tena kwenye ligi kubwa kama Morocco, kikubwa kama nitapata nafasi basi nifuate maelekezo ya kocha nini anataka.”

Kwenye timu mbalimbali kiungo huyo alicheza nafasi tofauti kama kiungo mzuiaji, nafasi za beki wa pembeni, beki wa kati na kote alicheza kwa kiwango kikubwa.

Mogbwemo Queens ilianzishwa mwaka 2004 na msimu 2022/2023 ikashiriki rasmi Ligi Kuu ya Wanawake baada ya misimu kadhaa nyuma.

Mwaka 2023, klabu hiyo ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake ya Sierra Leone, ikiwa imepoteza mechi moja tu kati ya ishirini na mbili ilizocheza.

Ubingwa huo uliwapatia nafasi ya kushiriki kwa mara ya kwanza mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika hatua ya mchujo wa Kanda ya Afrika Magharibi Ukanda A, ambako walitolewa mapema.