Kocha Singida Black Stars achekelea pointi moja

BAADA ya kuambulia suluhu dhidi ya Azam FC ugenini, kocha mkuu wa Singida Black Stars, Miguel Gamondi amesema kupata pointi moja mbele ya mshindani waliyenaye kwenye malengo sawa siyo haba.

Gamondi alifunguka hayo huku akiwapongeza wachezaji wa timu hiyo walikuwa na mchezo mzuri kipindi cha pili tofauti na kipindi cha kwanza na  walicheza chini ya kiwango.

“Haukuwa mchezo rahisi tumekutana na timu bora na shindani kwani tumo nayo kwenye malengo sawa msimu huu kuhakikisha tunawania nafasi nne za juu ili kurudi kwenye michuano ambayo tunaishiriki sasa,” amesema Gamondi na kuongeza;

“Ubora wa wapinzani wetu ulikuwa kipindi cha kwanza kama ambavyo sisipia tulikuwa bora kipindi cha kwanza licha ya kushindwa kupata matokeo ambayo yangetupa pointi tatu muhimu tukiwa ugenini hata moja tuliyoipata siyo haba.”

Akizungumzia pambano hilo kwa jumla, Gamondi amesema wachezaji wa timu hiyo walifanya makosa mengi kikosi cha kwanza hawakufanya vizuri wapinzani wao Azam FC kama wangekuwa makini basi walikuwa na nafasi nzuri za kufunga mabao zaidi ya mawili kipindi cha kwanza.

GAMO 01

“Wachezaji wangu hawakuwa vizuri kipindi cha kwanza walifanya makosa mawili hadi matatu makubwa kama Azam FC wangekuwa watulivu basi wangefunga, hivyo hivyo upande wetu kipindi cha pili tulibadilika na kutengeneza nafasi, pia hatukuzitumia.”

Gamondi amesema kupata kwao pointi moja wakiwa ugenini sio haba lakini sio matokeo ya kuyafurahia kwani huo haukuwa mpango wao walijiandaa kukusanya pointi zote tatu.

Sare waliyoipata Singida Black Stars imeifanya timu hiyo kufikisha pointi nane kwenye mechi nne walizocheza hadi sasa wakishinda michezo miwili na sare mbili hawajapoteza mchezo hata mmoja, wamefunga mabao matatu na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara moja.