Mahakama yaitaka Jamhuri kukamilisha upelelezi kesi ya Mange Kimambi

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeitaka Jamhuri kukamilisha upelelezi wa kesi ya uhujumu uchumi iliyomfungulia mwanaharakati maarufu kwenye mitandao ya kijamii ya X na Instagram anayeishi Marekani, Mange Kimambi.

Maelekezo hayo yametolewa leo Alhamisi Desemba 4, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu, Hassan Makube anayesikiliza kesi hiyo ilipotajwa mbele yake kuangalia mwenendo wa upelelezi.

“Mheshimiwa hakimu upelelezi wa kesi hii bado haujakamilika. Kwa hiyo, tunaomba tarehe nyingine ya kutajwa,” amesema mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Clemence Kato.

Kato ameeleza hayo baada ya hakimu Makube kuutaka upande wa Jamhuri kueleza hatua iliyofikiwa.

Kutokana na majibu hayo Makube ameelekeza upelelezi ukamilishwe haraka ili kesi ianze kusikilizwa.

“Upande wa Jamhuri hebu kamilisheni haraka taratibu za upelelezi ili kesi hii ianze kusikilizwa,” amesema.

Hakimu Makube ameipanga kesi hiyo kwa ajili ya kutajwa Januari 28, 2026.

Shauri hilo lilipoitwa mahakamani, upande wa mshtakiwa haukuwa na mwakilishi.

Katika kesi hiyo, Mange anakabiliwa na shtaka moja akidaiwa kujihusisha na utakatishaji wa fedha haramu. Shauri hilo lilifunguliwa na upande wa Jamhuri Agosti 28, 2025.

Mange kupitia mitandao ya kijamii, asubuhi ya Desemba 2, 2025 alionekana kwenye video iliyosambaa akithibitisha kupewa taarifa kuhusu kufunguliwa kwa kesi hiyo, akisema Serikali ya Tanzania imedhamiria kumrejesha nchini.

Sheria ya kurejeshwa kwa mtuhumiwa (Extradition Act Chapter 368) ya mwaka 2019, kosa la utakatishaji wa fedha ni miongoni mwa makosa ambayo yanaipa nguvu Tanzania kuomba kurejeshwa nchini mtuhumiwa wa kosa la jinai.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 000021172 ya 2025, kosa analodaiwa kutenda linaangukia kifungu 12(1)(d) na 13(a) cha Sheria ya Utakatishaji Fedha sura 423 ya 2019 ikisomwa kwa pamoja na Sheria ya Uhujumu Uchumi.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Jamhuri inadai katika tarehe mbalimbali kati ya Machi Mosi, 2022 na Machi 31, 2022, kwenye maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, alijipatia Sh138.5 milioni akifahamu fedha hizo ni zao la uhalifu.

Katika hati hiyo, inadaiwa Mange alijipatia fedha hizo kwa kufanya kazi ya uandishi wa habari bila kuwa na ithibati, pia kudai fedha hizo kwa vitisho.