MANUNGA ACHAGULIWA TENA KUONGOZA HALMASHAURI YA CHATO

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Chato, Christian Manunga

Kushoto ni Mwenyekiti na msimamizi wa Uchaguzi wa Mwenyekiti halmashauri, Das Thomas Dimme.

Kushoto ni Hakimu wa wilaya na kulia ni diwani wa kata ya Bwera, Josephat Manyenye, akipata kiapo

 ………………….

CHATO 

SIKU Chache baada ya kutokea sintofahamu katika viapo na Uchaguzi wa mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Chato mkoani Geita, hatimaye Madiwani wateule wamepata viapo rasmi na kumchagua Christian Manunga kuwa mwenyekiti wa halmashauri hiyo.

Manunga ambaye ni Diwani wa kata ya Bwongera kwa kipindi cha miaka 15 amefanikiwa kutwaa kwa mara nyingine nafasi hiyo baada ya Chama Cha Mapinduzi!(CCM) kuwasilisha jina lake kugombea nafasi hiyo.

Aidha katika uchaguzi huo, makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo amechaguliwa Photunatus Jangole, ambaye ni diwani wa kata ya Ilemela Chato huku akiahidi kumshauri vyema mwenyekiti wa halmashauri hiyo na kuhakikisha miradi ya maendeleo inagusa kata zote.

Akitangaza matokeo hayo, Mwenyekiti na msimamizi wa Uchaguzi huo, ambaye pia ni Katibu tawala wa wilaya ya Chato (Das), Thomas Dimme, kwa mujibu wa kura zilizopigwa ni 32 ambapo kura za ndiyo ni 28, kura haribika ni kura 4, hivyo amemthibitisha Manunga kuwa mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti wa halmashauri hiyo baada ya kuvuka nusu kura zote zilizopigwa.

Aidha Makamu mwenyekiti ameshinda baada ya kupata kura za ndiyo 29 kati ya kura 32 zilizopigwa huku kura za haribika zikiwa 3, hivyo msimamizi wa Uchaguzi huo kuwathibitisha rasmi kuwa ndiyo viongozi wapya wa halmashauri hiyo.

Hata hivyo Uchaguzi huo umefanyika baada ya Madiwani hao kupata viapo vya kuthibitisha kupokea nafasi hiyo, na kuwa waaminifu katika kutetea na kuisimamia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kanuni za Baraza la Madiwani.

Viapo hivyo vimetolewa mbele ya Hakimu kazi mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Chato, Amalia L. Mushi, ikiwa ni uthibitisho wa kutambuliwa kisheria madiwani hao, ambao wameanza rasmi kazi ya kuisimamia halmashauri hiyo.

Akitoa shukrani baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Manunga ameahidi kuendelea kuisimamia vyema halmashauri hiyo ili iweze kutimiza wajibu wake wa kuwahudumia wananchi.

Amesema baada ya Uchaguzi huo kumalizika ni wakati wa kuungana pamoja ili kuendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato, kusimamia fedha zote za umma pamoja na kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi wote.

Halmashauri ya wilaya ya Chato mkoani Geita inao Madiwani wa kata 23, viti maalumu Madiwani 8, Wabunge wa majimbo wawili na viti maalumu mmoja.