Marekani kutathimini uhusiano wake na Tanzania

Dar es Salaam. Serikali ya Marekani imesema inatathimini kwa kina uhusiano wake na Tanzania, kwa kile inachodai kutoridhishwa na matukio ya ukandamizwaji wa uhuru wa dini na uhuru wa kujieleza nchini unaofanywa na Serikali.

Mbali na hilo, Marekani imedai kwamba kumekuwapo na vikwazo vya mara kwa mara dhidi ya uwekezaji wa nchi hiyo na ukatili dhidi ya raia kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Taarifa kwa umma iliyotolewa leo Alhamisi Desemba 4, 2025 na Naibu Msemaji Mkuu wa Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, Tommy Pigott, imeeleza kuwa mambo hayo ndio yameifanya taifa hilo kutathimini upya uhusiano wake na Tanzania.

“Vitendo hivi vimewaweka raia wa Marekani, watalii na maslahi ya Marekani nchini Tanzania kuwa hatari na kutishia kudhoofisha ustawi na usalama wa pamoja uliokuwa alama ya ushirikiano wetu kwa miongo kadhaa,” amesema Pigott katika taarifa hiyo.

Kutokana na hilo, Pigott amesema Marekani haiwezi kufumbia macho vitendo vinavyohatarisha usalama wa raia wao au usalama na utulivu wa kanda, akisema mustakabali wa uhusiano wa kibalozi na Tanzania utategemea matendo yake.

“Marekani inathamini ushirikiano wake wa muda mrefu na watu wa Tanzania, ambao umeleta ustawi kwa wananchi na usalama katika kanda hii.

“Hata hivyo, hatua za hivi karibuni za Serikali ya Tanzania zimezua wasiwasi kuhusu mwelekeo wa uhusiano wetu rasmi wa kibalozi na kuaminika kwa Serikali ya Tanzania kama mbia,” amesema Pigott.                               

Jitihada za Mwananchi kumpata Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Mahmud Thabiti Kombo kuzungumzia hatua hiyo ya Marekani, hazijafanikiwa hata alipotafutwa kupitia simu yake ya mkononi.