Dar es Salaam. Mauzo ya bidhaa na huduma za Tanzania nje ya nchi yameongezeka hadi kufikia Sh42.128 trilioni katika mwaka ulioishia Septemba 2025 kutoka Sh36.712 trilioni katika kipindi kama hicho mwaka 2024, Ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaeleza.
Wakati mauzo haya yakizidi kupaa, wadau wanashauri nchi kuendelea kuongeza nguvu katika kuzalisha bidhaa zake kwa kuongeza thamani mazao yanayozalishwa ili kuongeza kiasi cha fedha kinachopatikana.
Ripoti hii ya tathmini ya hali ya uchumi ya kila mwezi inaonyesha Oktoba mwaka huu mauzo ya bidhaa peke yake nje ya nchi yalifikia Sh24.941 trilioni ikilinganisha na Sh20.028 trilioni mwaka uliopita.
Ongezeko hili lilichangiwa zaidi na mauzo ya dhahabu, bidhaa za viwandani, korosho, nafaka na tumbaku.
Mauzo ya dhahabu yaliongezeka kwa asilimia 35.8 na kufikia Sh10.920 trilioni kutoka Sh8.043 trilioni mwezi uliotangulia, kutokana na kuongezeka kwa bei ya dhahabu katika soko la dunia.
Mauzo ya bidhaa za asili yalifikia Sh3.657 trilioni, sawa na ongezeko la asilimia 38.3. Ongezeko hili likichangiwa mauzo makubwa zaidi ya korosho na tumbaku sambamba na kuimarika kwa bei ya mazao hayo katika soko la dunia. Vilevile, mauzo ya nafaka yaliongezeka kutokana na ongezeko la mahitaji ya chakula kutoka nchi jirani.
Kwa kulinganisha Septemba 2025 na kipindi kama hicho mwaka 2024, mauzo ya bidhaa nje ya nchi yaliongezeka hadi Sh2.514 trilioni kutoka dola za Marekani 2.302 milioni. Ongezeko hili lilichangiwa na mauzo makubwa ya dhahabu na bidhaa za viwandani.
Licha ya ongezeko hilo, mtaalamu wa uchumi, Profesa Haji Semboja amesema ili kuona faida ya ukuaji wa biashara inayofanya ni lazima nchi iongeze umiliki wa vitu vinavyoendana sana masoko ya kimataifa, kusimamia na kuendesha.
Alitolea mfano wa dhahabu, akisema nchi ingekuwa inafanya shughuli zote yenyewe kuanzia uchimbaji migodini hadi uongezaji thamani, mapato ambayo yanayopatikana yangekuwa ni makubwa kuliko yale yanayoonekana sasa.
“Lakini sasa fedha zinazopatikana ni za watu wengine, wewe unabaki na kidogo na takwimu kuwa umeuza kiasi hiki, tofauti na iwapo ungekuwa unamiliki kila kitu wewe mwenyewe,” amesema Profesa Semboja.
Pia alitaka kuongezwa kwa wigo wa bidhaa zinazouzwa nje, mbali na mazao amesema dunia ya sasa wanauza sana bidhaa za kidijiti, hivyo ni vyema kuangalia namna ya kuendana na mabadiliko hayo ya kasi ya sayansi na teknolojia.
“Ukiangalia kampuni zinazopata faida sana sasa hivi sasa ni microsoft na wengine, dijitali inalipa si kama bidhaa tu tunazouza, hivyo ni vyema kuangalia namna ya kuwekeza,” amesema.
Hata hivyo, licha ya mapungufu hayo, mtaalamu mwingine wa uchumi kutoka Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Aurelia Kamuzora amesema kuongeza kwa mauzo ya nje maana yake uchumi wa Tanzania unazidi kukua.
Amesema kukua kwa mauzo kutaenda sambamba na kuchochea ulipaji kodi mzuri na kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni.
“Tuendelee kuwekeza katika soko la bidhaa, uwekezaji unapoongezwa ndiyo unavyozalisha kazi. Ukizalisha mihogo mingi maana yake kuna mkulima amepata kazi, magari yanayobeba mzigo maana yake dereva amepata kazi, viwandani watu wameajiriwa na kodi inaongezeka,” amesema Profesa Kamuzora ambaye pia ni mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa.
Kutokana na hilo, ameshauri kuendelea kufanyika kwa uwekezaji katika soko la bidhaa ili kusaidia kuongezeka kwa thamani ya fedha kwa kuwa ndiyo kitu nchi inahitaji.
“Tunapoongeza thamani ya bidhaa zetu tuhakikishe tunazingatia ubora unaotakiwa, ili tuweze kushindana katika masoko ya kimataifa na bidhaa zetu kutambulika kwa ubora wake,” amesema.
Wakati hayo yakielezwa, John Philip, mmoja wa wakulima nchini, amependekeza jitihada zaidi za kuwezesha kilimo kufanyika ili kuhakikisha kundi kubwa la Watanzania linalotegemea sekta hiyo linanufaika kikamilifu.
Amesema hilo liende sambamba na kuwekwa kwa mifumo bora ya mauzo ya bidhaa ambayo yatamnufaisha mkulima bila kujali yuko mkoa gani.
“Siku hizi tunanufaika sana na minada ya kidijitali inayofanywa, inafanyika kwa uwazi sana na tunapata bei nzuri lakini ili watu wanufaike ni lazima kuhakikisha uwezeshaji wa kutoka unafanyika. Tuwape watu mbolea ya kutosha, maofisa ugani wapite kwao kwa wakati kusikiliza kama kuna changamoto. Soko lipo, tuongeze uzalishaji ili tupate fedha zaidi,” amesema Philip.