Maxime aibukia Mbeya City, kuanza kazi baada ya Simba

KOCHA Mecky Maxime ndiye mrithi rasmi wa Mbeya City ya Mbeya akichukua mikoba ya Malale Hamsini aliyeondolewa mwanzoni mwa wiki hii.

Maxime ambaye amewahi kuzinoa Kagera Sugar na Dodoma Jiji, ataanza rasmi kibarua cha kuinoa Mbeya City baada ya mechi ya leo Desemba 4, 2025 dhidi ya Simba.

Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti imezipata kutoka chanzo cha uhakika ndani ya Mbeya City, zimethibitisha kuwa timu hiyo imeshamalizana na Maxime.

“Mkataba umeshasainiwa na baada ya mchezo dhidi ya Simba ataanza majukumu yake. Kuhusu muda wa mkataba na mambo mengine, uongozi utatangaza rasmi.

“Maxime ni kocha mzuri na mwenye uzoefu, hivyo atakuwa na msaada mkubwa kwa Mbeya City,” kimesema chanzo hicho.

Msimu uliopita, Maxime aliinoa Dodoma Jiji FC ambayo aliiongoza kumaliza katika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mbeya City iliachana na Malale Hamsini muda mfupi baada ya kupoteza kwa bao 1-0 nyumbani dhidi ya Namungo, Novemba 30, 2025.

Maxime ameonekana jioni hii katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo kunakochezwa mechi kati ya Simba na Mbeya City