Dar es Salaam. Ikiwa imepita miezi zaidi ya minne tangu Tanzania izindue nembo yake ya Made in Tanzania kwa ajili ya kutambulisha bidhaa zake katika masoko ya nje, imeshatoa nembo hiyo kwa bidhaa zaidi ya 30.
Hayo yameelezwa leo Alhamisi, Desemba 4, 2025, na Ofisa Uendelezaji Biashara wa Tantrade, Deo Shayo, alipozungumza na Mwananchi katika ofisi za Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) na kuongeza kuwa lengo ni kuzitambulisha hadi bidhaa 100 hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu.
Nembo hiyo ilizinduliwa Julai 7, 2025 na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, ambaye alitaja kuwa itaitambulisha Tanzania kama taifa lenye bidhaa zenye ubora, ubunifu na fahari ya kiafrika.
Amesema Made in Tanzania itasaidia kutatua matatizo ambayo yalikuwa yakitokea, ikiwemo bidhaa za Tanzania kuuzwa kimataifa bila kutambulika kama zimezalishwa Tanzania huku nchi nyingine zikinufaika zaidi.
Katika uchumi, itasaidia kutanua wigo wa uzalishaji bidhaa kwa ajili ya masoko ya nje, jambo litakalochochea ajira kwa vijana, kilimo na viwanda.
Uwepo wa nembo hiyo pia utatanua wigo wa ukusanyaji wa mapato, kwani kila bidhaa itakuwa imetambuliwa baada ya kuzalishwa, huku ikiongeza umaarufu wa Tanzania katika soko la nje.
“Hii inafanya Tanzania inapotajwa, watu kuanza kufikiria zile bidhaa tunazalisha, kama ni kahawa, chai, nondo, mabati tunatambulika na inafika hatua ikitajwa sehemu yoyote mtu anawatambua kupitia bidhaa zetu mnazozalisha,” amesema Shayo.
Alipozungumzia uzinduzi wa nembo hiyo, aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo, Julai 2 mwaka huu, alisema nembo hiyo itaweka alama katika eneo la biashara kwa kuwa Tanzania imekuwa ikifanya vizuri katika uzalishaji, lakini bidhaa zake hazitambuliki vizuri katika masoko ya nje.
Hiyo ni baada ya baadhi ya bidhaa zinazozalishwa nchini kuwa zaidi ya mahitaji yaliyopo, jambo linalohitaji masoko zaidi.
“Kwa mfano, saruji mahitaji yetu ni tani milioni nane na sasa tunazalisha tani milioni 10, mahitaji ya sukari ni tani 802,000 lakini sasa inapanda hadi mwaka 2027 tutakuwa tumejitosheleza, hivyo lazima kuwe na nembo ya Made in Tanzania,” amesema.
Hayo yanaelezwa wakati ambao mauzo ya bidhaa na huduma za Tanzania nje ya nchi yameongezeka hadi kufikia Sh42.128 trilioni katika mwaka ulioishia Septemba 2025 kutoka Sh36.712 trilioni katika kipindi kama hicho mwaka 2024, Ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaeleza.
Ripoti hiyo ya tathmini ya hali ya uchumi ya kila mwezi ya Oktoba mwaka huu inaonesha mauzo ya bidhaa pekee katika masoko ya nje ya nchi yalifikia Sh24.941 trilioni, kilinganisha na Sh20.028 trilioni mwaka uliopita.
Ongezeko hilo lilichangiwa zaidi na mauzo ya dhahabu, bidhaa za viwandani, korosho, nafaka na tumbaku.
Ili mtu apewe nembo hiyo, Shayo amesema ni lazima bidhaa yake iwe na uasilia kwa kutengenezwa nchini angalau kwa asilimia 35.
“Mfano, unaweza kutengeneza dirisha la nondo (grill), hii nondo unaweza kuwa umeitoa nje ya nchi, ukabuni muundo, ukakunja, ukapiga rangi, ukaweka alama zako, ukija kupiga jumla ya shughuli zilizofanyika na malighafi ukapata zaidi ya asilimia 35, ina vigezo vya kupewa nembo ya Made in Tanzania,” amesema.
Ubora wa bidhaa ni jambo lingine linaloangaliwa, kwa kila bidhaa kupitishwa na mamlaka inayoisimamia, kama ni chakula basi ithibitishwe na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) au Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
“Pia namba ya mlipakodi ni muhimu, kwani bidhaa yoyote au biashara yoyote lazima ilipiwe kodi. Mtu kuwa na nembo ya kisekta nayo inampa kigezo cha kupata nembo hiyo, kwani anakuwa amekidhi vigezo vingine muhimu,” amesema.
Pia suala la uadilifu huzingatiwa, ikiwemo kutotumia watoto katika uzalishaji wa bidhaa, uhalali wa bidhaa kwa ajili ya masoko yote, kwani hayo ni mambo yanayobeba heshima ya nchi.
“Tunafanya hivi kwa sababu kitu kikipewa nembo ya Made in Tanzania maana yake kama nchi tunajivunia kukizalisha, sasa lazima iwe na vigezo hivi ili tukutambue,” amesema.
Amesema nembo hiyo hutakiwa kurejewa (renew) kila baada ya mwaka mmoja, kwani wanaamini ndani ya kipindi hicho huwa yanafanyika maboresho mbalimbali katika bidhaa ambayo wazalishaji wangependa kuyataja.
“Lakini pia unatakiwa kuomba upya ili tuone kama bado unazingatia vigezo vyote vinavyotakiwa,” amesema.
Amesema mtu anayehitaji nembo hiyo hutuma maombi kupitia tovuti ya Tantrade, kufungua akaunti na kufuata maelekezo, hatua inayoweza kuchukua saa mbili kukamilika ikiwa mtu amekamilisha nyaraka zote, au hadi siku tatu ikiwa atahitaji kufanya marekebisho katika baadhi ya vitu kabla ya kupewa nembo kwa ajili ya bidhaa zake.
“Malipo ya awali ni Sh10,000 kwa ajili ya mchakato wote na anapokamilisha kila kitu anapewa nembo, QR Code na cheti ambapo atatakiwa kulipia Sh50,000,” amesema.
Amesema lengo lao ni kuhakikisha bidhaa zote zinazozalishwa Tanzania zinapewa nembo hiyo, hata nguo zinazotengenezwa nchini.
Amesema kupitia QR wanayoweka itasaidia kuwabaini wale wanaofanya udanganyifu, na watakaobainika kufanya hivyo ni faini ya kati ya Sh1 milioni hadi Sh20 milioni.
Kwa mujibu wa Shayo, kabla ya mtu kupewa nembo hiyo huelimishwa kwanini ni muhimu kuwa nayo, na utafika wakati maneno ya Made in Tanzania hayatakuwa yakitumika, bali nembo pekee.
“Ili kufikia watu wengi zaidi tumepanga kukutana na sekta binafsi na Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania ili wawajengee uelewa juu ya umuhimu wa kuwa na nembo hiyo katika bidhaa zao,” amesema.
Kwa upande wake, Shamimu Rashid, muuzaji wa bidhaa za viungo, ametaka elimu zaidi itolewe ili watu wajue namna wanavyopata nembo hiyo.
“Ukizungumzia kupata kitu, watu wanadhani hadi uende ofisini urudishwe ukalete hiki na kile, kama watu wangejua wanaweza kuomba mtandaoni, bidhaa nyingi zingekuwa zimepata nembo hiyo.
“Elimu itolewe zaidi na elimu hii iende sambamba na kuweka mazingira mepesi ili wajasiriamali wapata nembo za TBS kwa urahisi,” amesema.
Akijibu suala hilo, Shayo amesema wanaendelea na uelimishaji kupitia makundi mbalimbali yanayopangwa ili watu wengi waelewe umuhimu wake.