Pacome, Dube waizima Fountain Gate

MABAO mawili yaliyofungwa kila moja katika kipindi cha mechi ya Ligi Kuu Bara leo la Prince Dube na Pacome Zouzoua yalitosha kuipa Yanga ushindi wa nne wa Ligi Kuu Bara na kuendeleza ubabe mbele ya Fountain Gate.

Ushindi huo umeifanya Yanga kufikisha pointi 13 na kuchupa kutoka nafasi ya tano hadi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo, ikiishusha Mashujaa inayolinga nao pointi ila ikiizidi uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Yanga ina mabao 11 na kufungwa moja, wakati Mashujaa ina matano na kufungwa manne ikiwa imecheza mechi tisa tofauti na watetezi waliocheza mechi tano hadi sasa.

NAB 01

Katika pambano hilo la tatu la Ligi Kuu kwa Pedro Goncalves, kocha huyo Mreno alifanya mabadiliko kadhaa ya wachezaji waliocheza mechi mbili zilizopota za Caf akimpumzisha kabisa kipa Diarra Djigui na Mudathir Yahya, huku Pacome, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ wakianzia benchi.

Beki Frank Assinki alianzisha sambamba na Dickon Job, ilihali Offen Chikola akianzishwa na kushirikiana na kina Maxi Nzengeli, Duke Abuya, Mohamed Doumbia, Celestin Ecua na Duke Abuya na kuisumbua Fountain Gate.

Dube ndiye alikuwa wa kwanza kuifungia Yanga bao la kuongoza dakika ya 29 kwa penalti na la pili lilipachikwa na Pacome dakika ya 82 akipokea pasi nzuri kutoka kwa Duke Abuya.

Fountain iliingia uwanjani kwa kujilinda zaidi, lakini haikuizuia Yanga kuendeleza ubabe kwani tangu timu hiyo ipande daraja, haijawahi kutamba mbele ya watetezi hao, kwani haikutengeneza nafasi za kumtia kashkash Abutwalib Mshery aliyeanza langoni leo kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge.

NAB 03

Katika kipindi cha kwanza ilichonga kona mbili lakini hazikuwa na faida kwao kutokana na kutokuwa na madhara langoni kwa Fountain Gate.

Kipindi cha pili Yanga ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Maxi Nzengeli nafasi yake ilichukuliwa na Pacome Zouzoua, Offen Chikola alitoka nafasi yake ilichukuliwa na Lassine Kouma, alitoka Chadrack Boka akaingia Mohammed Tshabalala.

Mabadiliko yaliyoisaidia Yanga kupata bao la pili la Pacome na kumfanya nyota huyo kufikisha bao la pili msimu huu katika Ligi Kuu.