Dar es Salaam. Kampuni ya Ulinzi ya SGA Security kwa mara nyingine imetajwa kuwa mtoa huduma za usalama anayeaminika zaidi Afrika na kutwaa tuzo ya chaguo la mtumiaji kwa mwaka 2025.
Tuzo hiyo ilitangazwa kwenye Tamasha la Tuzo ya Chaguo la Mtumiaji Afrika kwa mwaka 2025 jijini Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali na kampuni kutoka Afrika.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa SGA Tanzania, Dk Eric Sambu amesema kwa mara nyingine watumiaji wa huduma za kampuni yao wameonesha imani kwa kampuni kongwe ya ulinzi katika Bara la Afrika.
Tuzo hiyo ya SGA, Β imekuja baada ya tuzo nyingine ya awali kwa Kampuni Bora ya Ulinzi ya Mwaka Afrika katika Kundi la Huduma za Ulinzi.
Akieleza zaidi, Dk Sambu amesema SGA imewekeza katika kuwaridhisha wateja wake, hivyo imekuwa ikiboresha huduma zake ili kuhakikisha wateja wanapata thamani ya fedha katika mahusiano yenye manufaa kwa pande zote mbili.
Amesema tuzo hiyo ni kwa ajili ya wafanyakazi wote, ambao ni zaidi ya 18,000 katika Bara la Afrika, ambao kila mwaka huwahudumia wateja wao vizuri Β na kuongeza juhudi katika utoaji wa huduma.
“Tuna vyeti vinne vya Shirika la Kimataifa la Kusanifisha (ISO), ambavyo vimepatikana kwa miaka kadhaa, vikionesha matengenezo ya mifumo thabiti ya usimamizi ili kuhakikisha ubora wa huduma zetu kwa manufaa ya wateja wetu na kwa umma,” amesema.
Akizungumzia siri ya mafanikio, Dk Sambu amesema katika huduma za ulinzi wamewawezesha wafanyakazi kuwahudumia wateja vizuri na kampuni imewekeza sana katika kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa ngazi zote, hasa juu ya mienendo, vitendo vinavyojitokeza Β na hatari ya vitisho.
Tuzo ya Chaguo la Mtumiaji Afrika inayotolewa kila mwaka, inalolenga kutoa tuzo kwa kampuni, mashirika na taasisi barani Afrika katika sekta mbalimbali za uchumi kupitia maoni ya umma yanayokusanywa kama kura za mtandaoni kupitia tovuti hii, iliyoanzishwa mwaka 2019 jijini Dar es Salaam.