Dar es Salaam. Meya mpya wa Jiji la Dar es Salaam, Nurdin Juma, maarufu Shetta amesema katika uongozi wake atahakikisha kila mmoja anapata haki yake inayostahiki na hakuna atakayependelewa.
Diwani huyo wa Mchikichini katika kuhakikisha hilo amesema yeye siyo meya wa mtu bali ni wa Jiji la Dar es Salaam.
Shetta amesema hayo leo Desemba 4, 2025 katika ukumbi wa Karimjee baada ya kushinda nafasi hiyo kwa madiwani kumchagua kuwa Meya wa jiji hilo.
Shetta anakuwa meya wa Jiji hilo akichukua nafasi ya Omary Kumbilamoto aliyehudumu kuanzia mwaka 2021 hadi 2025.
“Tuwe watu wamoja tusiwe na makundi tunapopata kitu tunakwenda pamoja, hakuna mtu kupendelewa haya mambo katika uongozi wangu sitataka kuyaona.”
“Ofisi yangu iko wazi mnakaribishwa. Nasema hivi kwa sababu wapo watu wanaoweza kujimilikisha meya. Nitoe rai mimi sio meya wa mtu,” amesema.
Amesema anachotamani Shetta ni umoja na si mgawanyiko na manenomaneno huku akiahidi kuwaunganisha watu wote madiwani na watumishi.
Shetta ameshukuru kuchaguliwa kwa kishindo huku akiahidi kutekeleza dhamana hiyo kwa uadilifu bila kuchoka.
Amesema kwa umoja wao watahakikisha mapato yanaongezeka zaidi kutoka Sh132 bilioni za sasa.
Akizungumza kwa mara ya kwanza katika baraza hilo la madiwani kama Meya, ameshukuru kwa kuchaguliwa kwa kishindo, huku akiahidi kushikamana na uongozi uliopita.
“Nakuomba Kumbilamoto uwe mwalimu wangu ili niweze kufanikisha kazi kubwa iliyopo mbele yangu,” amesema.
Ameomba watumishi na viongozi wote wa jiji kufanya kazi kwa pamoja kusimamia sheria, kanuni na taratibu zote zilizopo.
Awali, katika uchaguzi huo wajumbe 51 waliopiga kura walimchagua Shetta kwa kura 48 huku mbili zikiwa za hapana moja ikiharibika. Kwa upande wake John Mrema ambaye ni Naibu Meya amepata kura za ndiyo 49.
Katika mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM kumpata mgombea wa Umeya wa Jiji katika uchaguzi uliofanyika Ukumbi wa CCM Wilaya ya Ilala, Shetta aliibuka mshindi baada ya kupata kura 25, akimshinda Diwani wa Segerea, Robert Manangwa, aliyepata kura 21.
Ushindi huo ulifikiwa baada ya mchakato wa kura kurudiwa kwa mara ya pili kufuatia duru ya awali kufutwa kutokana na mgombea aliyekuwa anaongoza kushindwa kufikisha nusu ya kura halali 52 zilizopigwa.
Aliyekuwa anatetea nafasi hiyo, Omary Kumbilamoto aliondolewa mapema baada ya kupata kura nne tu katika duru ya kwanza.
Amesema vijana ndio wenye kujenga nchi hivyo fedha za mikopo ya asilimia 10 atahakikisha wanazipata ili kujikwamua kiuchumi.
“Tuwape vipaumbele vijana wapate fedha hizi ili kujikwamua kiuchumi, tulinde amani yetu, tusishawishike vijana wenzangu,” amesema Shetta.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya amesema wananchi wa jiji hilo asilimia kubwa ni wafanyabiashara hivyo kwa kushirikiana na uongozi watahakikisha wanafanya kazi na biashara kama inavyotakiwa.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amesema bajeti iliyopendekezwa na kupitishwa ya Sh152 bilioni katika mwaka huu wa fedha ni wajibu wa timu nzima ya Ilala kuisimamia kwa kushirikiana.
“Meya ndiyo taa ya jiji lazima tumpe ushirikiano katika kutimiza majukumu yote,” amesema.
Kwa upande wake Naibu Meya Mrema amesema anatarajia kufanya kazi kwa kuheshimiana na watumishi wa Serikali. “Tufanye kasi kwa kusimamia masilahi ya wananchi,” amesema.
Diwani Buyuni, Jesca Msola amesema atahakikisha miradi ya barabara, afya, elimu, miundombinu na yote inayohusu maendeleo ya wananchi inasimamiwa utekelezwaji wake vyema.
