Simba yajipigia Mbeya City, Bajaber atupia

SIMBA kama kawaida imeendeleza moto wake kwenye Ligi Kuu Bara, baada ya kuichapa Mbeya City mabao 3-0, lakini utamu wa ushindi huo ni kiungo Mohammed Bajaber.

Ushindi huo wa nne kwenye mechi nne za Ligi Kuu Bara unaifanya Simba kufikisha pointi 12 ikipaa kutoka nafasi ya nane mpaka ya tano.

Mapema tu Mbeya City iliilainisha mechi baada ya mshambuliaji wake Vitalis Mayanga kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja na mwamuzi Nassoro Mwinchui dakika ya 23 baada ya kumpiga kiwiko beki wa Simba, Antony Mligo.

SIMB 02

Kadi hiyo ikafungulia mabao ambapo kiungo Morice Abraham akaanza kutikisa nyavu dakika ya 27 akimalizia kazi nzuri ya Ellie Mpanzu.

Wakati Mbeya City inatafuta utulivu ikajikuta inaruhusu bao la pili dakika ya 37 mfungaji akiwa Jonathan Sowah akifunga kirahisi akinufaika na makosa ya mabeki wa wageni waliokuwa wanagongeana pasi eneo la nyuma na mshambuliaji huyo kwenda kumfunga kipa Benno Kakolanya.

Mabao hayo yakadumu mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika huku Simba ikiongozwa na Seleman Matola ikionekana kutulia na kucheza kwa kasi.

Kipindi cha pili Simba kama ingetulia ingeongeza mabao mengi lakini washambuliaji wake wakajikuta wanapoteza nafasi nyingi.

SIMB 01

Majukwaa ya Uwanja wa Meja Jeneali Isamuhyo yakalipuka kwa furaha dakika ya 84 wakati kiungo Mkenya, Mohamed Bajaber akiingia uwanjani ikiwa ni mechi yake ya kwanza tangu asajiliwe na wekundu hao akitokea Kenya Police, akichukua nafasi ya Mpanzu.

Mapokezi hayo yakalipa dakika ya 85 baada ya Bajaber mpira wake wa kwanza kugusa tangu aingie uwanjani akaifungia Simba bao la tatu akipokea pasi ya Steven Mukwala.

Bao hilo likaimaliza mechi hiyo ikiisha kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 huku Mbeya City ikizidi kuandamwa na matokeo mabaya, ikipoteza mechi nne mfululizo.