Simba, Yanga zarudi mzigoni kukipiga leo

LIGI Kuu Bara inaendelea leo Alhamisi kwa mechi mbili vinazohusisha vigogo Simba na Yanga zinazokabiliana na Fountain Gate na Mbeya City zikitoka katika majukumu ya mechi za kimataifa za Ligi ya Mabingwa Afrika ugenini.

Yanga yenyewe itaanza kazi saa 10 jioni kuikaribisha Fountain Gate kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge jijini Dar es Salaam kabla ya saa 1:00 usiku Simba itakuwa mwenyeji wa Mbeya City kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Mbweni, Dar es Salaam.

Yanga imekuwa na mwenendo mzuri ikionyesha ubora katika kila eneo la uwanja, imefanya hivyo msimu huu katika mashindano yote inayoshiriki wakati wapinzani wao wakitoka kuchapwa 2-0 nyumbani na JKT Tanzania.

Mara ya mwisho dhidi ya Fountain Gate, Yanga ilishinda kwa mabao 4–0, huku msimu uliopita, Yanga iliitandika Fountain Gate mabao 9-0 katika mechi zote mbili walizokutana katika ligi.

Wale nyota waliofunga katika ushindi wa 4-0, wote hawapo katika mechi ya leo akiwamo Clement Mzize aliyefunga mawili anayeuguza majeraha, wakati Stephanie Aziz Ki na Clatous Chama wapo na timu nyingine. Aziz KI amejiunga na Wydad ya Morocco, Chama akiitumikia Singida Black Stars.

Kikosi cha Yanga kina ubora katika maeneo mengi ukilinganisha na Fountain Gate, ikiwamo aina ya uchezaji wenye kasi na kupiga pasi fupi.

Yanga inatumia mfumo wa kuanzisha mashambulizi nyuma kwa utulivu, kisha kuyapandisha kwa kasi kupitia viungo wao wabunifu Maxi Nzengeli, Duke Abuya  na Celestine Ecua. Pia ina mabeki wenye nidhamu wakiongozwa na Dickson Job, Ibrahim Bacca na Bakari Mwamnyeto wenye kujiamini na mawasiliano mazuri, ukiachilia uzoefu walionao. Katika mechi tatu ilizocheza, imeruhusu bao moja tu, huku ikifunga mabao tisa.

Ubora wa wachezaji wa pembeni ilionao Yanga, ni hatari kwa wapinzani kwani timu hiyo inajulikana kwa kutumia vizuri udhaifu wa beki za pembeni za wapinzani.

Kwa upande wa Fountain Gate, changamoto kubwa imekuwa kukosa uzoefu dhidi ya timu kubwa, jambo linalosababisha kupoteza umakini dakika muhimu za mchezo.

Timu imekuwa ikipoteza mipira kirahisi katikati ya uwanja na kuruhusu presha isiyo ya lazima katika eneo lao la hatari.

Hivyo italazimika kuboresha ulinzi hasa katika dakika 20 za mwanzo ambazo Yanga mara nyingi hutumia kutafuta bao la mapema.

Ikiwa Fountain itadhibiti presha ya mwanzo, mechi inaweza kuwa mgumu zaidi kuliko wengi wanavyotarajia.

Katika mechi tisa za ligi ilizocheza Fountain, imeshinda tatu, sare moja na kupoteza tano huku ikionekana kuwa na tatizo la ufungaji na ulinzi kwani imefunga mabao manne na kuruhusu kumi.

Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves, alisema licha ya kuwa na changamoto ya fatiki kutokana na kucheza mfululizo, lakini bado wanataka alama tatu.

“Diarra (Djigui) na Pacome (Zouzoua) hawako sawa kiafya, lakini tunaamini waliopo wana uwezo wa kufanya vyema kwenye mechi iliyopo mbele yetu.

“Tutakwenda kutengeneza nafasi na kuzifanyia kazi, lakini kuhakikisha haturudii makosa ambayo tuliyafanya kwenye mechi zilizopita,” alisema kocha huyo, huku kocha wa Fountain, Mohamed Ismail ‘Laizer’ alisema: “Mchezo ujao dhidi ya Yanga hautakuwa mgumu kwetu wala mrahisi kwa wapinzani wetu kwa kuwa tumejipanga kutoa ushindani mkubwa, najua wametoka kucheza kimataifa hivyo wako vizuri.”

Simba imecheza mechi tatu, imefunga mabao manane, hivyo Wekundu hao wana uwezo wa kufunga mabao mawili kila mechi. Mbeya City iliyorejea Ligi Kuu msimu huu, imeshuka dimbani mara tisa, imefunga mabao saba na kuruhusu 10. Ina tatizo la kujilinda huku ikijitahidi katika kushambulia.

Timu hizi zinakwenda kukutana zote zikiwa zina mabadiliko ya mabenchi ya ufundi. Mbeya City ikiwa imeachana kocha mkuu, Malale Hamsini, wakati Simba ikiachana na Dimitar Pantev ambaye kwa kiasi kikubwa alikuwa anaongoza benchi hilo la ufundi.

Simba imeendelea kuwa moja ya timu zenye kiwango cha juu nchini, ingawa msimu huu imekuwa na vikwazo kadhaa vinavyohitaji suluhisho la haraka.

Katika mechi ya mwisho dhidi ya Mbeya City, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3–1, ikiwa ni mechi ya Kombe la FA msimu uliopita. Katika Ligi, mara ya mwisho zilikutana Januari 18, 2023, Simba ikashinda 3-2.

Simba ina safu ya ushambuliaji inayotegemewa, ingawa mara kadhaa imeshindwa kutumia nafasi muhimu wanazotengeneza. Hata hivyo, timu hii inapocheza mechi kubwa, mara nyingi huonekana kubadilika na kucheza kwa kasi, mashambulizi kwa wingi, ambayo huwafanya wapinzani kushindwa kuunganisha pasi.

Rekodi zinaonyesha katika mechi kumi baina ya timu hizo, Simba imepata ushindi mara nane, Mbeya City ikishinda moja huku pia sare ikiwa moja.

Moja ya tabia kubwa ya Mbeya City ni pale inapokuwa nyumbani huwa na moto tofauti kabisa na ikicheza ugenini. Ni timu inayocheza kwa kasi, wana mashabiki wanaowapa nguvu, na mara nyingi wachezaji wao wa pembeni hutoa changamoto kubwa kwa mabeki.

Lakini inapokuwa ugenini, imeonyesha udhaifu kwa kiasi fulani ingawa pia imepambana na kushinda mechi mbili kati ya tano, ikipoteza tatu msimu huu.

Mbeya City kinachowatesa sana ni uzoefu na ubora wa kikosi, mara nyingi wamekuwa na rekodi duni dhidi ya timu kubwa kama Simba.

Rekodi zinaonyesha katika mechi 19 dhidi ya Simba, Mbeya City imeshinda mara tatu, imepoteza 12.

Kocha wa Simba, Selemani Matola, alisema kwa sasa wanawaza mechi za ligi na wameachana na kimataifa, kwa sababu hata upande wa ndani ni kugumu.

“Sisi tunaipa umakini mkubwa Mbeya City kwa sababu na wao ni wagumu licha ya kwamba tuna rekodi ya kuwafunga mechi za karibuni ila lazima tuwe na nidhamu,” alisema Matola.

Kocha wa Mbeya City, Patrick Mwangata alisema: “Hatutarajii kupoteza mchezo wa kesho (leo) na sina hofu kwa sababu tumejipanga vyema na tumeshaangusha alama tatu kwenye mechi tatu zilizopita, hivyo tunataka kufanya vizuri.”