Tanzania inavyoweza kujitegemea, kujitosheleza kiuchumi bila misaada

Tanzania inaweza kujitegemea kwa kutumia makusanyo ya ndani yanayo Mamlaka ya Mapao Tanzania (TRA) Pamoja na yale yasiyo ya kikodi yanayokusanywa na mamlaka nyingine ikiwemo Serikali za mitaa.

Ili hilo lifanikiwe wadau wanashauri kuongeza ufanisi wa ukusanyaji kodi, kupanua wigo wa walipa kodi, kupambana na ukwepaji kodi pamoja na kutumia mapato hayo kuboresha huduma za jamii na kuchochea uchumi.

Haya yanasemwa wakati ambao Rais Samia Suluhu Hassan ametaka nchi kusimama imara na kujitegemea kwa kiasi kikubwa kwa kutumia fedha za ndani wakati akizundua Bunge na kuwaapisha mawaziri.

Rais Samia alisema mikopo na misaada inaweza kupungua kutokana na yale yaliyotokea Oktoba 29, 2025 siku ya uchaguzi ambayo alisema yaliiitia doa Tanzania ambayo kwa miaka minne iliyopita ilivutia mikopo na misaada kutoka kwa wafadhiri wa kimataifa.

Siku chache baada ya Rais Samia kutoa kauli hiyo Bunge la Umoja wa Ulaya (EU) lilitangaza kupitisha azimio lake leo Novemba 27, 2025 la kuzuia zaidi ya Euro 150 milioni (zaidi ya Sh400 bilioni) zilizopangwa kutolewa kwa Tanzania mwaka 2026 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambapo imeeleza wasiwasi wake kuzorota kwa hali ya haki za binadamu na utawala wa sheria nchini Tanzania.

Hata hivyo, kauli hizi zinakuja wakati Tanzania ikishuhudia kwa vipindi tofauti ukuaji wa ukusanyaji wa mapato unaofanywa na TRA hali inayofanya wadau kukiri kuwa nchi inaweza kujitegemea ikiwa itabana matumizi na kutanua wogo wa kodi.

Taarifa za hivi karibuni zinaonyesha kuwa TRA ilifanikiwa kukusanya Sh8.97 trilioni kati ya Julai hadi Septemba 2025 Ikiwa ni ongezeko la asilimia 15.1 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliotangulia.

Makusanyo hayo ni sawa na ufanisi wa asilimia 106.3 ya lengo lililokuwa limewekwa la kukusanya Sh8.43 trilioni.

Taarifa iliyotolewa na TRA Oktoba 2, 2025 ilieleza kuwa, makusanyo yaliyokusanywa kwenye robo ya Julai hadi Septemba 2025 ni sawa na ukuaji wa asilimia 104 ukilinganisha na Sh4.40 trilioni zilizokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka 2020/2021.

Pia, taarifa hiyo inaeleza kuwa, wastani wa makusanyo kwa mwezi pia umeongezeka kutoka cha Sh1.47 trilioni kwa mwezi, mwaka 2021/22 mpaka Sh2.99 trilioni kwa mwezi kwa mwaka 2025/26.

“Ili tuweze kujitegema ni vyema kuangalia maeneo ambayo unaweza kubana matumizi kuboresha, kupunguza au vingine kuachana navyo,” anasema Dk Lutengano Mwinuka ambaye ni mtaalamu na mchambuzi wa masuala ya uchumi.

Kuangalia vipaumbekle kwani kulikuwa na fedha zilitegemea fedha za wahisani, vipaumbele viuwiane na uhalisia jisni ulivyo, kinachopatikana kipatikane wapi

Anasema suala hilo liende sambamba na kuangalia vipengele vilivyokuwa vimewekwa katiba bajeti kwani baadhi ya fedha zilikuwa zinategemea fedha za wahisani ili kuhakikisha vinavyobakia vinauwiana na uhalisia ulivyo kwani fedha itakuwa inajulikana inakotoka.

“Pia kutanua wigo wa kukusanya kodi, kutumia teknlojia ili upate mapato zaidi, kuhakikisha wote wanaopaswa kulipa kodi wanalipa. Pia kutumia nguvu za ndani, mikopo ya ndani na hata ubia una maana kubwa katika serikali kuokoa fedha kwani watatekeleza miradi kwa mikopo yao wenyewe,” anasema.

Mtaalamu wa uchumi kutoka chou kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Dk Felix Nandonde nchi kuwa na uwezo wa kujitegemea imekuwa ni kiu ya muda mrefu lakini bado haijafanikiwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo pesa nyingi kutoingizwa katika mfumo kama ambavyo ripoti za CAG zimekuwa zikieleza.

“Huenda tumeanza kutembea kwa vitendo kwa maelekezo ya wakuu wetu kwa kuzuia mianya hii hasa kwa watumishi wasiokuwa na weledi ila tunahitaji kuongeza nguvu,” anasema Dk Nandonde.

Ili hilo lifanikiwe alitaka kuwekwa kwa mpango unaosaidia kuzuia upotevu wa mapato kama ambavyo hutajwa katika Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) hasa yanayokusanywa na halmashauri na hata TRA yenyewe.

Hata hivyo, Dk Nandonde anasema kuongezeka kwa mapato yanayokusanywa TRA inaweza kuonyesha kuwa watu wameelimishwa vya kutosha na kulipa kodi ipasavyo au huenda urasimishaji shughuli za kiuchumi umeimarika ikilinganishwa na miaka ya nyuma ambayo kulikuwa na maeneo ambayo yalikuwa hayatozwi

“Kama TRA wanafanya kazi kwa kiasi hicho ni sehemu inayotupa nafasi kujitathmini zaidi kuhakikisha tunapata kodi katika maeneo ambayo hatupati ili kuweza kuendesha shughuli zetu za ndani,” amesema.

Alitumia nafasi hiyo kutaka kutanuliwa zaidi kwa wigo wa kodi kwani bado wanaolipa ni wachache ikilinganishwa na wanaopaswa kulipa.

Wafanyabiashara wazungumza

Mwenyekiti wa Jumuiya ya wafanyabiashara Tanzania (JWT), Khamisi Livembe alitoa angalizo kuwa wakati nchi ikilenga kujitegemea ni vyema kutoongeza viwango vya kodi na ushuru ili kufiidia pengo linaloachwa.

“Kodi kubwa haizalishi mapato ya kudumu huwa ni ya muda mfupi na baadaye hupotea kabisa. Ni kama ng’ombe wa maziwa ukiamua kumchinja nyama utakula nyama siku moja itaisha na mwisho wa siku hutakuwa na nyama wala maziwa,” anasema Livembe.

Anasema huu ni wakati wa serikali kuangalia sehemu ambayo inaweza kuwekwa nafuu ili ikusanye zaidi na kuweka kodi katika maeneo ambayo yanawezekana kutozwa.

Lakini zipo njia nyingi za kuongeza kodi alizoshauri ikiwemo kuongeza wingi wa bandari kavu (ICD’s) ili zisaidie kurahisisha upakuaji wa mizigo bandarini kwa kile alichobainisha kuwa ufanisi wa bandari unavyozidi kuongezeka unaongeza uhitaji wa sehemu za kuhifadhi mizigo ili kuzirahisishia meli kushusha mizigo.

Pia alitaka kuangaliwa kwa namna bora ya uondoshaji wa mizigo bandarini kwenda maeneo mbalimbali nchi nan je ya nchi kwa kile alichokisema kuwa sasa barabara inayotegemewa ni ile ya Morogoro na Mandela kwa kiasi kikubwa.

“Tuangalie namna ya kutoa mizigo kwa kasi kulingana na ushushaji, kufanya hivikuitaweza kusaidia kuziba pengo linalotokana na kupungua ufadhili. Ile reli ya SGR ikamilishwe haraka ili isaidie kutoa mizigo bandarini,” anasema.

Hata yote yafanyike wakati ambao anapendekeza kama nchi iongee nan chi wahisani ili waweze kuongeza muda wa kulipa madeni kwa masharti nafuu ili isaidie kushusha kiwango cha fedha zinazolipwa kila mwaka.

Kuhusu hofu ya kuongezwa kodi alilokusema Livembe, kulijibiwa siku chache zilizopita na Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda ambapo alisema Tanzania kujitegemea kwa mapato ya ndani haimaanishi kuwaongeza Wananchi Viwango vya ulipaji kodi bali ni kuongeza ufanisi kwa kutanua wigo wa kodi na kuzuia ukwepaji kodi.

Badala yake Mwenda alisema katika kufanikisha hilo watazia mianya ya ukwepaji kodi, kuweka mazingira mazuri kwa wanaolipa kodi vizuri na kuongeza wigo wa kodi na siyo kuongeza Viwango vya kodi inayolipwa.