Dar es Salaam. Wahitimu wamehimizwa kuendeleza nidhamu, ustahimilivu na kujituma baada ya kupitia safari yenye changamoto nyingi lakini walidumu katika misingi hiyo.
Wito huo umetolewa leo Desemba 4, 2025 na Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dk Ali Mohamed Shein katika mahafari ya 24 ya chuo hicho tawi la Dar es Salaam yaliyofanyika Mlimani City.
Amesema maarifa waliyopata hayana maana kama hayataongozwa na uadilifu. Taifa linawahitaji kama watu wa kusimamia ukweli na kusisitiza mchango wao katika jamii ni muhimu kuliko shahada wanazopokea leo.
Dk Shein amesema mafanikio yao yanatokana na misingi thabiti ya maadili na uwajibikaji waliouonyesha katika kipindi chote cha masomo. Pia wanapaswa kutambua kuwa mafanikio yao ni matokeo ya juhudi binafsi na mchango wa wale waliowasimamia katika safari ya kitaaluma.
βNyuso zenu leo zinaonyesha faraja na matumaini mapya, Mmeweka bidii, mmevumilia na sasa mko tayari kuanza awamu mpya yenye majukumu makubwa zaidi. Nawapongeza kwa hatua hii muhimu,” amesema Dk Shein ambaye ni Rais mstaafu wa Zanzibar.
Amesema wahitimu watumie maarifa yao kwa uadilifu na ubunifu, akisema dunia ya sasa inahitaji watu wanaoweza kutatua matatizo kwa njia bunifu na zenye tija na ana imani wahitimu wa Mzumbe wataendelea kuwa chachu ya maendeleo katika jamii wanazokwenda kutumikia.
Hivyo, amesema Mzumbe itaendelea kuwekeza katika kutoa elimu yenye kuzingatia ushindani wa kitaifa na kimataifa, kwani mahitaji ya wataalamu nchini yanaongezeka katika fani za sheria, usimamizi, uchumi na sekta mbalimbali za kijamii kwani ongezeko la matokeo mazuri kwa wahitimu zaidi ya asilimia 23 mwaka huu ni ishara kuwa chuo kinasonga mbele kitaaluma.
Katika mahafari hayo ya 24 tawi la Dar es Salaam jumla ya wahitimu 752 wametunukiwa stahiki zao katika ngazi mbalimbali. Katika hao 560 wametunukiwa shahada ya umahiri na kati yao wanaume ni 251 sawa na asilimia 44.8 na wanawake 309 sawa na asilimia 55.18.
Wahitimu 192 wametunukiwa shahada ya kwanza kati ya hao 82 sawa na asilimia 43 ni wanawake na 110 sawa na asilimia 57 ni wanaume.
Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa William Mwegoha amewataka wahitimu kutumia elimu waliyoipata kwa uadilifu, uvumilivu, na ari ya kuleta maendeleo katika maisha yao na jamii.
Amesema mafanikio ya kumaliza masomo si mwisho wa safari ya elimu, bali ni mwanzo wa changamoto mpya za maisha: βElimu mliyoipata hapa ni silaha yenye nguvu inayoweza kubadilisha maisha yenu na ya jamii mnayoihudumia. Ni jukumu lenu kuitumia kwa uelewa na uadilifu.β
Amesema wahitimu wanapaswa kutumia teknolojia kwa uwazi, uwajibikaji na maadili mema, huku wakijenga miradi inayoongeza tija na kuboresha huduma kwa jamii. Kila mradi unaotumia AI kwa uadilifu na weledi unaweza kuchangia maendeleo ya taifa na jamii.
Pia, amewahimiza wahitimu kuangalia elimu yao kama msingi wa kuunda ajira na kuanzisha biashara.
Β βTumia ujuzi wenu kuanzisha biashara ndogo au kubwa, kuongeza ajira, na kusaidia wengine kupata fursa za maendeleo. Kuwa wabunifu, wavumilivu na waadilifu katika kila hatua mnayochukua,β amesisitiza.
Kwa upande wake, mwananfunzi bora wa shahada uhasibu na fedha katika Sekta ya Biashara, Anold Ngoli aliyepata alama ya 4.7 na kufanya vizuri kwenye andiko la mafunzo amewataka wanafunzi wajikite katika nidhamu, bidii, uadilifu na kujituma badala ya kutegemea alama pekee kama kipimo cha mafanikio.
“Matumizi sahihi ya teknolojia, ikiwemo akili bandia (AI), yanaweza kuongeza ufanisi katika masomo na kuwaandaa wanafunzi kutengeneza ubunifu badala ya kuitumia vibaya,” amesema Ngoli.
