Joseph Guede anahesabu siku Singida Black Stars

MSHAMBULIAJI  wa zamani wa Yanga, Joseph Guede anahesabu siku tu kabla ya kurejea tena Singida Black Stars, inayoelezwa imeshamalizana naye na kumsainisha mkataba wa kuitumika kuanzia dirisha dogo la usajili wa ligi hiyo.

Guede aliitumikia timu hiyo msimu uliopita  kabla ya kuondoka mapema kutokana na kuwa na majeraha na sasa inadaiwa kila kitu kimekaa sawa kabla ya kuingia Singida BS katika mfumo rasmi na kutambulika baada ya dirisha dogo la usajili litakalofunguliwa mwanzoni Januari mwakani.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga, klabu yake imetangaza kumrejesha tena kikosini kuongeza nguvu safu ya ushambuliaji ambayo inaongozwa na Mkenya Elvis Rupia, Horso Muaku, Andrew Phiri raia wa Zambiani na Mishamo Daudi ni mara yake ya pili kuichezea timu hiyo kabla ya kuondolewa akiwa  amehudumu kwa miezi mitano pekee.

Chanzo cha kuaminika kutoka Singida BS, kimeliambia Mwanaspoti mshambuliaji huyo tayari amesaini mkataba baada ya Kocha Miguel Gamondi kuridhishwa na kiwango chake hivyo kuanzia Januari ataanza kuitumikia timu hiyo.

GUE 01

“Ni kweli Guede tumemalizana naye na ataungana na washambuliaji wengine ambao tayari wapo kikosini japo kuna dalili kubwa wawili miongoni mwao wakatemwa ili kupisha sajili nyingine akiwemo Guede ambaye kila kitu kimekamilika,” amesema mtoa taarifa huyo na kuongeza;

“Usajili wake ni mapendekezo ya benchi la ufundi na tunaamini ataongeza kitu kwenye safu yetu ya ushambuliaji ambayo kwa sasa inategemewa zaidi na viungo bora washambuliaji tulionao.”

Guede hakuwa na miezi mitano mizuri ndani ya Singida baada ya kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara huku akiwa pia hajafunga bao lolote mpaka uongozi ulipofanya uamuzi wa kuachana naye.

Kabla ya hapo akiwa Yanga ndani ya miezi sita aliifungia timu hiyo mabao 10 kwenye mashindano yote aliyocheza lakini Mabingwa hao wa soka wakagoma kumuongezea mkataba.