Moshi. Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA) Mkoa wa Kilimanjaro imewataka watoa huduma za usafiri kuepuka upandishaji wa nauli holela na matumizi ya magari mabovu, hasa katika msimu huu wa kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka ambapo mahitaji ya usafiri huwa makubwa.
Ofisa Mfawidhi wa LATRA mkoani hapa, Paulo Nyello, amesema mamlaka hiyo imejipanga kikamilifu kuhakikisha wasafiri wote ndani ya mkoa huo wanakuwa salama wawapo safarini na wanalipa nauli zilizopo kwa mujibu wa sheria ili wananchi na wageni wanaoingia mkoani hapa wasipate usumbufu.
“Hali ya usafiri ni shwari, huduma zinaendelea vizuri ndani na nje ya Mkoa. Kama tunavyofahamu, Desemba Kilimanjaro hupokea wageni wengi wanaokuja kwenye shughuli za sikukuu. Tunawahakikishia wenyeji na wageni wote kuwa haki yao ya usafiri italindwa,” amesema Nyello.
Ameongeza kuwa” LATRA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani imeimarisha doria katika maeneo yenye wingi wa wasafiri, ikiwamo Rombo, Machame na Bomang’ombe, ili kuhakikisha kunakuwa na usalama kwa wasafiri na wanapata huduma stahiki.
Amesema Wilaya ya Rombo ndiyo hupokea wasafiri wengi zaidi katika sikukuu za mwisho wa mwaka, hivyo magari mapya yenye uwezo wa kubeba abiria 25 yameongezwa ili kupunguza msongamano wa abiria.
“Pia tumejipanga kutoa vibali maalumu kwa magari yatakayohitajika kulingana na mahitaji na wingi wa watu, mradi yakidhi vigezo vya usalama wa abiria,” amesema.
Nyello ametoa angalizo kwa madereva na watoa huduma wanaopanga kutumia magari mabovu au kupandisha nauli bila ruhusa kuacha tabia hiyo kwa kuwa mamlaka itachukua hatua kali kwa watakaobainika.
“Matumizi ya magari mabovu ni kosa kisheria. Tutachukua hatua kwa yeyote atakayebainika kufanya hivyo. Timu zetu za ukaguzi ziko kazini kudhibiti hali hiyo,” amesisitiza.
Kuhusu makosa ya kupandisha nauli au kuzidisha abiria, Nyello amesema adhabu ya papo kwa papo ni Sh250,000, na wahusika wanaweza kufikishwa mahakamani, kufungiwa leseni au kusitishiwa kibali cha usafirishaji.
“Nawaomba watoa huduma wafuate sheria na masharti ya leseni zao bila kushurutishwa. Hudumieni wananchi kwa usalama na uadilifu,” amesema.
Ashura Elias, mmoja wa wananchi wa mkoa huo wameiomba Mamlaka hiyo kuhakikisha hakuna uongezwaji wa nauli kiholela kwani wananchi wa hali ya chini ndio wanaoumizwa.
“Tunaziomba mamlaka husika hasa kipindi hiki kuhakikisha abiria hawatozwi nauli kiholela, lakini pia usafiri wa uhakika uwepo, maana kusipokuwepo na magari ya kutosha madereva wanajipangia nauli wanavyotaka
Naye John Kombe mkazi wa Moshi, amesema udhibiti wa nauli ufanywe maeneo yote hadi vijijini, ili kudhibiti madereva wote ambao wamekuwa na tamaa ya kupandisha nauli katika msimu wa sikukuu.
“Zipo nauli ambazo zimepitishwa na Latra ambazo ndizo zinatambulika, tuombe hizo zizingatiwe na wale watakaokiuka taratibu hatua kali zichukuliwe ili kuwa fundisho kwa wengine,” amesema Kombe.
