…………
Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi
amewasihi watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira kufanya
kazi kwa weledi kwa kuzingatia dhamana kubwa waliyopewa ya kusimamia suala la
Mazingira na Muungano hapa nchini.
Makamu wa
Rais amesema hayo wakati akizungumza na watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano
na Mazingira katika kikao kazi kilichofanyika mkoani Dodoma. Amewataka kutambua
na kuchukulia kwa uzito suala la uhifadhi na usimamizi wa mazingira kwani
linabeba mustakabali wa vizazi vya sasa na baadaye.
Aidha
amewataka kuwa na utaratibu wa upimaji wa malengo yaliyowekwa katika Wizara
hiyo ikiwemo upandaji wa miti ili kuhakikisha utekelezaji wa mipango na malengo
ya uhifadhi mazingira yanakuwa na matokeo mazuri na yenye manufaa.
Makamu wa
Rais, amesema ni lazima Wizara hiyo kutambua umuhimu wa suala la Muungano kwa
kuhakikisha elimu inatolewa vya kutosha kwa wananchi hususani vijana kwa
kuhusianisha maendeleo na mafanikio ya Taifa yanategemea uimara wa Muungano.
Ameongeza
kwamba, kutokana na idadi kubwa ya wananchi waliozaliwa baada ya Muungano mwaka
1964, ni vema kutoa elimu ya kuwafahamisha umuhimu na uzuri wa Muungano ili
kuweza kuendeleza yale ya Serikali zilizopita na kuwa na Taifa zuri zaidi
kwenda mbele.
Halikadhalika,
Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa Wizara hiyo kujipanga kuhakikisha
inatekeleza hapa nchini, maazimio na mipango ya kulinda mazingira yanayofikiwa
katika mikutano ya kimataifa ambayo Tanzania inashiriki.
Vilevile,
Makamu wa Rais amewataka watumishi wa Wizara hiyo kuzingatia ahadi za
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan, alizotoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, kwa kubainisha yale
yanayohusu Wizara hiyo na yatekelezwe kwa ufanisi.
Makamu wa
Rais amewasihi watumishi hao, kuisoma na kuelewa vema Dira ya Taifa ya Maendeleo
2050 ili kubaini maeneo ambayo Wizara inahusika zaidi na kuhakikisha
yanatekelezwa. Pia amewaagiza kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi
2025 – 2030 na kutekelezaa yale ambayo Wizara inahusika moja kwa moja.
Makamu wa
Rais amewahimiza kuzingatia mafunzo kazini ili kuweza kuenda sambamba na
mabadiliko yanayojitokeza pamoja na kufanya kazi kwa bidii na nidhamu na kuwa
mfano mzuri katika Serikali.
Awali Makamu
wa Rais, alitembelea na kukagua jengo la Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na
Mazingira linalojengwa katika Mji wa Serikali Mtumba mkoani Dodoma, na kupongeza
hatua kubwa iliyofikiwa katika ujenzi huo na kuwasihi wakandarasi kuhakikisha
wanatimiza ahadi ya kukamilisha jengo hilo ifikapo mwezi Machi 2026.


