Unguja. Meya wa Jiji la Zanzibar, Kamal Abdulsatar Haji amesema atahakikisha anatunza siri za serikali katika utekelezaji wa majukumu yake ili kulinda maadili ya utumishi wa umma huku akisisitiza suala la kuvunja makundi.
Hayo ameyasema jana Desemba 4, 2025 katika hafla ya kuwaapisha madiwani wateule uliombatana na uchaguzi wa kumchangua Meya na Naibu wake iliyofanyika katika Ofisi za Baraza la Jiji Michenzani Unguja.
Amesema, si jambo la kujivunia kwa mtendaji kusambaza au kuzungumzia taarifa ambazo zipo katika mazingira ya kikazi, bila kuzingatia taratibu za serikali.
Haji amewasisitiza watendaji wa baraza hilo kuhakikisha vikao vyao vinakuwa vya siri na kushuka kwa wananchi kusikiliza changamoto zao na kuzitatua kwa haraka.
“Nahitaji tufanye kazi kwa ushirikiano na kuvunja makundi kwani hayawezi kutusaidia katika utekelezaji wa majukumu yetu,” amesema
Naye aliyekuwa Meya wa Jiji hilo, Mahmoud Mohammed Mussa amesema ni jambo la msingi viongozi hao kuona umuhimu wa kuwa na ustahamilivu na uadilifu wanapotekeleza majukumu yao.
Amesema, kiongozi mwenye dhamana anapaswa kuwa makini kwa kauli na matendo yake ili kulinda heshima ya ofisi pamoja na maslahi ya wananchi.
“Kiongozi anapokula kiapo tayari ametoa uhalali wa kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ikiwa atakiuka maagizo yote aliyopewa hivyo kila mmoja atekeleze majukumu yake kwa mujibu wa sheria,” amesema
Naye, Naibu Meya, Haitham Muhidini Khamis amewapongeza wajumbe kwa kumchagua kwa kura za ndio na kuwaomba kushirikiana na upendo ili kufanya kazi kwa ufanisi kwani bila ya ushirikiano hawawezi kufikia lengo lililokusudiwa na serikali.
Kwa upande wake, Hakimu Mkoa wa Mjini, Mummin Ali Juma ameeleza, imani yake kwa viongozi hao akisema bila shaka watatekeleza majukumu yao ipasavyo kwa mujibu wa sheria na watambue kuwa kiapo hicho wamejikubalisha na kutoa uhalali wa kuchukuliwa hatua wakati wowote endapo watakwenda kinyume.