Dar es Salaam. Siku moja baada ya Marekani kueleza azma yake ya kutathmini uhusiano wake na Tanzania, mataifa mbalimbali ya Ulaya na Scandinavia, yenye balozi zake nchini, yamelaani mauaji ya raia katika maandamano ya Oktoba 29, 2025 huku wakizitaka mamlaka kukabidhi miili ya marehemu ili wakazike.
Kupitia tamko lao la pamoja, balozi za Uingereza, Canada, Norway, Uswisi, Ubelgiji, Denmark, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi, Poland, Slovakia, Hispania, Uswiswi na Ujumbe wa Umoja wa Ulaya (EU), zimeeleza kuhuzunishwa na vifo vilivyotokana vurugu za Oktoba 29.
Tamko hilo la balozi hizo, limekuja siku moja baada ya Serikali ya Marekani kueleza kuwa inatathmini kwa kina uhusiano wake na Tanzania, kwa kile inachodai kutoridhishwa na matukio ya ukandamizwaji wa uhuru wa dini na uhuru wa kujieleza nchini unaofanywa na Serikali.
Mbali na hilo, Marekani pia imedai kwamba kumekuwapo na vikwazo vya mara kwa mara dhidi ya uwekezaji wa nchi hiyo na ukatili dhidi ya raia kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Katika tamko hilo, balozi hizo zilianza kwa kurejea tamko la Mwakilishi Mkuu wa Umoja wa Ulaya (EU) lililotolewa Novemba 2, 2025 na tamko la pamoja la mawaziri wa mambo ya nje wa Canada, Norway na Uingereza la Oktoba 31, 2025 kuhusu uchaguzi wa Tanzania.
“Tumehuzunishwa sana kwa vifo na majeruhi wengi waliotokana na matukio ya wakati wa uchaguzi. Tunatambua azma ya Serikali ya kudumisha amani na utulivu, tunasisitiza umuhimu wa vyombo vya ulinzi kutekeleza majukumu yao kwa uangalifu mkubwa,” wameeleza.
Katika tamko hilo, balozi hizo zimejerea wito wake wa kuitaka Serikali ya Tanzania kutekeleza ahadi zake za kimataifa za kulinda haki za msingi, ikiwemo, haki za kikatiba za kupata taarifa na uhuru wa kujieleza kwa Watanzania wote.
“Taarifa za kuaminika kutoka mashirika ya kitaifa na kimataifa zinaonyesha ushahidi wa mauaji nje ya utaratibu wa kisheria, kupotea kwa watu, ukamataji wa watu kiholela na ufichaji wa miili ya waliopoteza maisha.
“Tunatoa wito kwa mamlaka husika kukabidhi miili ya marehemu kwa familia zao haraka iwezekanavyo, kuwaachia huru wafungwa wote wa kisiasa na kuhakikisha waliokamatwa wanapata misaada ya kisheria na matibabu,” limeeleza tamko hilo.
Hata hivyo, Desemba 2, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan alisema Serikali anayoiongoza haitakubali kupangiwa cha kufanya, wala kupewa masharti na yeyote, badala yake ataongoza kwa misingi ya Katiba.
Katika maelezo yake, Rais Samia alisema kumeibuka wadau wa kimataifa wanaoipangia Tanzania mambo ya kufanya, akihoji wao ni kina nani hasa hadi waipangie nchi huru.
Mkuu huyo wa nchi, alieleza kuwa Tanzania ni nchi huru na sio koloni la yeyote kwa sasa. Mataifa yanayoipangia nchi cha kufanya yenyewe mara kadhaa yanakumbwa na hali kama hiyo lakini hayapangiwi cha kufanya.
Balozi hizo pia zimetoa wito kwa Serikali kushughulikia mapendekezo yaliyotolewa katika ripoti za awali za waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) zilizoweka bayana mapungufu yaliyojiri wakati wa uchaguzi.
“Tunakaribisha hatua ya Serikali ya kutambua kwamba kuelewa kiini na mazingira yaliyopelekea vurugu, ikiwemo vifo, ni hatua muhimu kuelekea upatikanaji wa haki na maridhiano,” wameeleza.
“Uchunguzi wowote lazima uwe huru, wazi na shirikishi ukijumuisha asasi za kiraia, taasisi za kidini na wadau wote wa kisiasa,” wameeleza.
Akizungumzia matamko hayo, mchambuzi wa siasa za kimataifa na diplomasia, Deus Kibamba amesema matamko hayo yanaashiria Tanzania imekalia kuti kavu kwa siku zijazo, kwa sababu uchumi wa nchi si mkubwa, lakini umekuwa na mwenendo mzuri kutokana na msaada wa kibajeti na mikopo inayotolewa Marekani na EU.
“Kama Marekani ana ‘review’ uhusiano wake na Tanzania ni kauli tata na nzito kidiplomasia, sio kwamba haieleweki bali inaashiria kitu kibaya kwa nchi. Nilivyoisikia nimesononeka sana, maana hali yetu si nzuri, kama bajeti sapoti hakuna ya Marekani na EU, naona ndoto hali haitakuwa nzuri,” ameeleza Kibamba.
Kibamba amesema Marekani imeeleza kuthamini upya uhusiano wake na Tanzania, kwa sababu mbalimbali walizozitoa ikiwemo kutoridhishwa na uhuru wa kujieleza ndani ya nchi, ukizingatia taifa hilo linaheshimu haki za binadamu.
Mtaalamu mwingine wa diplomasia, Innocent Shoo amesema tamko la Marekani linamaanisha hawakuridhishwa na mwenendo wa uchaguzi, kiasiasa kidemokrasia, haki za binadamu na haki za raia nchini.
“Maana yake wanataka tujirekebishe ili kuendana na viwango vya ubora wa kimataifa kwa sababu wao (Marekani na EU), hawajafurahia mchakato mzima wa mwenendo wa Tanzania na wamesema tunawabughi watu wa Marekani wanaowekeza,” amesema.
