Unguja. Zanzibar inatarajia kupata mfutiko mkubwa katika sekta ya nishati kufuatia kutiwa saini kwa mradi wa uimarishaji wa miundombinu ya umeme wenye thamani ya Sh385 bilioni, baina ya Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco) na kampuni ya Elecmech Switchgears kutoka Dubai.
Hafla ya utiaji saini imefanyika leo Ijumaa, Desemba 5, 2025, katika viwanja vya Maisara, Mjini Unguja.
Mradi huo, ambao utatekelezwa kwa kipindi cha miaka saba, unalenga kuongeza uwezo wa usambazaji wa umeme, kuimarisha uhifadhi wa nishati na kuwezesha utambuzi wa hitilafu kwa haraka ili kupunguza adha za kukatika kwa umeme kisiwani.
Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja Mkuu wa Zeco, Haji Haji, amesema mradi huo utabadilisha kwa kiwango kikubwa miundombinu chakavu ya umeme iliyopo sasa na kuweka mifumo ya kisasa yenye uwezo mkubwa wa kusafirisha umeme.
“Mradi huu utaondoa njia za umeme zilizopo zenye uwezo mdogo wa milimita 50 na kuweka zile zenye uwezo wa milimita 150. Hii itatuwezesha kusafirisha umeme mwingi zaidi kutokana na ongezeko la matumizi,” amesema Haji.
Ameeleza kuwa ukomo wa uwezo wa njia za sasa umekuwa ukilazimu Zeco kukata umeme mara kwa mara ili kuepusha athari kwenye mfumo, jambo ambalo mradi huu utalimaliza kwa kuongeza uwezo wa kuhifadhi nishati na kuifanya ipatikane hata wakati kunapotokea upungufu kwenye gridi.
Haji alisisitiza kuwa Zanzibar itaondokana na mfumo wa zima washa unaosababishwa na uchakavu wa miundombinu, kwani vifaa vipya vya kuhifadhia umeme vitahakikisha huduma inapatikana bila kukatika kirahisi.
Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Nadir Abdullatif akizungumza baada ya kushuhudia utiaji saini mkataba wa uimarishaji miundombinu ya umeme baina ya Shirika la Umeme Zanzibar na Kampuni ya Elecmech Switchgears ya Dubai.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu katika Wizara ya Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Joseph Kilangi, alifafanua maeneo manne muhimu ya utekelezaji wa mradi huo ikiwemo ufungaji wa vifaa vya kuhifadhi umeme vyenye uwezo wa megawati 20 na ujenzi wa kituo cha uzalishaji umeme wa jua chenye uwezo wa megawati 30.
Kadhali amesema mradi huo utahusisha ufungaji wa vifaa vya kisasa vitakavyowezesha kugundua hitilafu pindi zinapojitokeza na ubadilishaji wa njia na mfumo wa kusafirisha umeme kwa umbali wa kilomita 210.
Kilangi amesema mradi huo utagharimu dola za Marekani milioni 159, sawa na Sh385 bilioni, ambazo zote zitalipwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
“Kukamilika kwa mkataba huu kutapunguza muda wanaotumia mafundi wetu kugundua hitilafu kwa kuwa hatutategemea tena uchunguzi wa kutembea kwa miguu. Teknolojia itafanya kazi hiyo kwa haraka,” amesema.
Waziri wa Wizara ya Maji, Nishati na Madini, Nadir Abdullatif, alisema mradi huo ni hatua muhimu kwa Zanzibar kwani unapeleka shirika hilo kwenye teknolojia za kisasa zitakazorahisisha utendaji kazi na kupunguza changamoto za mara kwa mara za umeme.
Akizungumza kwa niaba ya kampuni ya Elecmech Switchgears, Nimish Patel alimshukuru Rais na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuwamini na kuahidi kwamba watautekeleza mradi huo kwa uaminifu, weledi na ubora wa kiwango cha juu.