Ulanguzi tiketi wapamba moto kwa abiria

Dar es Salaam. Wingi wa abiria wanaosafiri kutoka Stendi Kuu ya Mabasi ya Magufuli kuelekea mikoa mbalimbali nchini umeibua mianya ya ulanguzi wa tiketi, hali inayowalazimu baadhi ya wasafiri kulipa nauli za juu kupita viwango halali.

Ongezeko hili la mapema la abiria linachochewa na tetesi za maandamano yanayodaiwa kupangwa kufanyika Desemba 9. Kwa kawaida, changamoto za usafiri huanza kuonekana kuanzia Desemba 20, lakini mwaka huu zimejitokeza mapema.

Hofu hiyo inajengwa na kumbukumbu za maisha magumu waliyopitia wakazi wa Dar es Salaam baada ya matukio ya Oktoba 29, yaliyosababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali za umma na binafsi.

Kufuatia matukio hayo, Polisi ilitoa amri ya wananchi kutotoka nje kuanzia saa 12 jioni, iliyodumu kwa takriban siku tano, hivyo safari hii baadhi ya wananchi wakaona waondoke mapema kuepuka adha hiyo.

Desemba 2, Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na wazee wa Dar es Salaam, alitangaza hakikisho la usalama katika jiji hilo na maeneo mengine, akisema Serikali imejipanga kudhibiti matukio yoyote wakati wowote.

Maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam yameshuhudia ulinzi ukianza kuimarishwa chini ya Polisi na vikosi vingine vya ulinzi na usalama, hasa askari wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi Tanzania (JWTZ).

Kutokana na hali hiyo inayoshuhudiwa, nafasi kwenye mabasi mengi yanayoenda mikoani zimejaa kuanzia Desemba mosi hadi Desemba 8, 2025, kwa mujibu wa mfumo wa ukataji tiketi mtandaoni.

Hata hivyo, kinachoonekana ni kuwa kuna baadhi ya watu waliokata tiketi tiketi kwa kuziuza kwa wasafiri waliozikosa kwa bei wanayofikiria wao, wakati tiketi unayouziwa inakuwa imeandikwa kiwango halali cha nauli.

Mchezo huo unadaiwa kuchezwa na baadhi ya wamiliki wa mabasi kwa kushirikiana na vijana hao ili kutumia uhitaji uliopo kujinufaisha.

Ingawa vitendo hivyo vinanufaisha wachache, walanguzi na uwezo wa kulipa zaidi, umegeuka shubiri na mzigo kwa abiria wengi wa kipato cha chini, hasa wanaohitaji kusafiri haraka.

Kwa mfano, nauli ya Dar es Salaam kwenda Njombe imepandishwa hadi Sh65, 000 kutoka Sh48,000; Dar–Iringa Sh55,000 badala ya Sh35,000 na Dar–Mtwara kufika Sh55,000 kutoka Sh40,000.

Mwananchi imezungumza na mmoja wa vijana wanaouzaji tiketi hizo, ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema ongezeko la abiria ni sababu ya wao kutumia mbinu hiyo.

“Unajua ni mpango ambao unasukwa na wenye mabasi wenyewe, mfano mimi nauza tiketi katika kila tiketi za kwenda Njombe, nauli halali ni Sh48, 000, nauza kwa 65,000 mwenyewe nachukua Sh10,000 mwenye basi anapewa chake,” amesema.

Amesema kulingana na hali ilivyo, abiria hawezi kuacha kusafiri na ikizingatiwa walio wengi wana presha ya kuondoka kwenda mkoani na kila basi limejaa.

“Kama hawawezi kulipia, anabaki na wenye fedha wanaosafiri,” amesema.

‘Abiria wanalazimisha’

Alipoulizwa kuhusu madai hayo, Mkurugenzi wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Mustapha Mwalongo amekiri kuwepo kwa viwango hivyo kwa baadhi ya vijana wasiokuwa waaminifu, lakini akasema hali hiyo husababishwa na abiria wanaolazimisha kusafiri.

“Ni kweli kuna vitendo hivyo vinafanyika lakini kwa kificho, abiria wenyewe wanalazimisha hali hiyo. Abiria anaambiwa basi limejaa lakini analazimisha kusafiri siku hiyo hiyo, ni chanzo cha yote hayo,” amesema.

Pia, Mwalongo ametoa tahadhari kwa abiria, akiwataka kutokata tiketi kwa watu wasiofahamika, ili kuepuka kulanguliwa au kutapeliwa kutokana na msongamano wa abiria uliopo.

Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Usafiri Ardhini (Latra) Kituo cha Magufuli, Rukia Kibwana alipoulizwa kuhusu hali hiyo, amesema wanafuatilia na wanaobainika kufanya mchezo huo wanawapeleka Polisi ili wachukuliwe hatua za kisheria.

“Ushauri wetu wananchi wakate tiketi kwa njia mtandao ili walipe bei halali, na wakiona zimejaa wasilazimishe kusafiri siku hiyo hiyo, wawe na subira waangalie siku zinazofuata,” amesema.

Amesema ili kukabiliana na wingi huo wa abiria, Latra wameanza kutoa vibali vya muda mfupi kwa wasafirishaji wa mabasi kwa maeneo yenye uhitaji mkubwa kama Iringa, Dodoma, Tanga na Morogoro.

“Tumetoa ruhusu kwa wenye mabasi yenye sifa kufanya safari kwenda maeneo hayo na zaidi ya vibali 12 vimeshatolewa kuanzia juzi, lengo wananchi wapate huduma nzuri,” amesema.

Baadhi ya abiria waliozungumza na Mwananchi wamedai wakiangalia kwenye mifumo ya tiketi mtandaoni, tiketi zimeisha lakini wanapofika stendi hukuta vijana wakitembea na tiketi mkononi, wakiziuza.

Sabina Milinga, abiria aliyekuja kutafuta tiketi ya kuelekea Njombe, amesema imelazimu alinunue tiketi kwa Sh65, 000 badala ya Sh48, 000 ziliyopangwa na Latra.

Amesema licha ya usafiri kuwa mgumu, mawakala wameongeza ugumu zaidi kwa kuuza tiketi kwa bei ya juu.

“Usafiri hakuna, lakini ukiwafuata mawakala wanakwambia tiketi zipo lakini bei tunayouza unaweza kulipia? Ukikubali wanakutajia bei. Nimeilipa na nasubiri safari; basi linaondoka saa 10 jioni,” amesema Sabina.

Amesema licha ya hali hiyo anashukuru kwani amekuwa akihangaika kutafuta tiketi tangu Novemba 30 bila mafanikio.

Kwa upande mwingine, Herman Gerald anayesafiri kwenda Iringa, amesema amejikuta kwenye mazingira magumu baada ya kutozwa Sh55, 000 badala ya Sh35,000.

 “Nimeongea na wakala lakini hanielewi. Naenda Iringa kikazi, ni lazima nipate tiketi iliyo na kiwango halali ili nikifika ofisini fedha zangu nirudishiwe, hali imekuwa ngumu,” amesema Helman.

Kwa upande wake Meshack Mbangula amelazimika kuhairisha safari ya kwenda Tanga baada ya kukosa fedha ya kuongezea ili apate tiketi.

“Nimefika tangu alfajiri nimezunguka kutafuta usafiri kila gari imejaa lakini madalali wanauza tiketi kwa bei yao, nimeongea nao kiasi nilichonacho hawanielewi, tumezoea kwenda Tanga Sh 17,000 lakini sasa wanataka Sh30,000, nimeshindwa narudi nyumbani kwenda kuongezea,” amesema Meshack.

Katika hatua nyingine, Kibwana wa Latra amewashauri abiria wanaohitaji kusafiri kwenda Kaskazini kutumia usafiri wa treni, akisema kuna inayoondoka Jumatatu na Ijumaa, ili kuepuka adha ya usafiri wa mabasi.

Kwa upande wa kwenda Zanzibar, Mwananchi limefika bandarini na kukuta umati wa watu katika ofisi za kukata tiketi na wengine maeneo ya kusubiri abiria.

Akizungumza na Mwananchi mmoja wa abiria aliyekuwa anaelekea Zanzibar, Jasmine Hashimu amesema ni wakati wa likizo kwa wanafunzi na baadhi ya wafanyakazi, hivyo wengi huitaji kusafiri kuwatembelea ndugu na jamaa.

“Shule nyingi tayari zimeshafungwa, hivyo baadhi yao wanarudi nyumbani na wengine kwenda kusalimia ndugu, jamaa na marafiki wanaoishi visiwani,” amesema.

Naye Khalfan Ahmad ambaye amesafiri kutoka Zanzibar kwenda Dar es Salaam, amesema wasafiri wengine wanakwenda vyuoni kwa kuwa tayari vimeshafunguliwa tangu wiki iliyopita.

“Vyuo vingi hapa Dar es Salaam kwa wanafunzi wanaoendelea, vimefunguliwa tangu wiki iliyopita wachelewaji kama mimi ndo tunaripoti,” amesema.

Msafiri mwingine ambaye hakutaka kutajwa jina lake amesema uhitaji wa watu kusafiri mapema tofauti na sikuuu za mwisho wa mwaka ni baadhi ya shule kuwahi kufungwa.

“Baadhi ya shule zimefungwa tangu mwishoni mwa mwezi Novemba, hivyo likizo nayo imeanza mapema,” amesema.

Kwa upande wake, mfanyabiashara ya chakula katika eneo hilo aliyejitambulisha kwa jina moja la Mariam amesema tangu kuanza kwa wiki hii, kumekuwa na ongezeko la watu wanaokwenda kupata huduma ya chakula tofauti na siku za kawaida.

“Kuna wakati haswa asubuhi na jioni watu wanakuwa wengi hadi kukosa eneo la kukaa, tunashukuru tunapata riziki,” amesema.