Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ameielekeza TANESCO kuchukua hatua na kuchunguza kwa kina kauli iliyotolewa na Padri Dk. Charles Kitima akidai kuwa shirika hilo lilizima umeme ili kurahisisha shambulio dhidi yake katika makazi ya maaskofu.
Akizungumza leo katika hafla ya uzinduzi wa mita janja kwa wateja wa TANESCO jijini Dar es Salaam, Chalamila alisema madai hayo ni mazito na yanagusa moja kwa moja taswira ya shirika hilo muhimu la umma, hivyo hayawezi kupuuzwa.
Chalamila alieleza kuwa alimsikia Padri Kitima akitamka hadharani kuwa siku ya tukio la uvamizi kulikuwa na mpango kati ya wahalifu na TANESCO, kwa madai kwamba umeme umezimwa kwa makusudi ili kuwapa nafasi wavamizi kumdhuru.
Amesema tayari amezungumza na Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Lazaro Twange, na wamekubaliana kuwa kauli kama hizo zinahitaji uthibitisho wa kina na hatua stahiki, ili kulinda heshima na uaminifu wa shirika hilo mbele ya wananchi.
Chalamila ameongeza kuwa kama kuna ukweli wowote, uchunguzi utafichua; na kama ni taarifa zisizo sahihi, hatua zitachukuliwa kwa mujibu wa taratibu.
Related
