Zikibaki siku 26, Mukoko, Yacouba, Inonga wapo Dar

HAKUNA anayejua nini kinachoendelea wakati dirisha dogo la usajili likitarajiwa kufunguliwa Januari mwakani, lakini ni kwamba kama hujui nyota wa zamani wa Simba na Yanga Mukoko Tonombe, Yacouba Songne na Henock Inonga wapo Dar wakisikilizia dili jipya.

Mukoko na Yacouba waliwahi kuitumikia Yanga wakati Inonga alikipiga Simba inayoelezwa ilimbeba juu kwa juu wakati akiwa njiani kutua Jangwani na kuupiga mwingi akishirikiana na Pascal Wawa, Joash Onyango na Fondoh Che Malone.

Mwanaspoti limeshuhudia mastaa hao watatu wakijitokeza katika viwanja viwili tofauti katika mechi za Ligi Kuu ambazo timu zao za zamani zilicheza dhidi ya Fountain Gate na Mbeya City.

Yanga ndio ilikuwa ya kwanza kucheza mapema dhidi ya Fountain Gate kwenye Uwanja wa KMC Complex ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0 na jukwaani walionekana kiungo mkabaji Mukoko na mshambuliaji Yacouba waliokuwa sambamba na kipa wa Yanga, Djigui Diarra na Clement Mzize ambao hawakuwa sehemu ya kikosi kilichocheza mechi hiyo.

Kwa upande wa Mukoko katika kikosi cha Yanga alicheza misimu ya 2020/21 na 2021/22 akicheza sambamba na Feisal Salum ‘Fei Toto’ kabla ya kupandishwa kucheza kiungo mshambuliaji chini ya Nasreddine Nabi.

Msimu wa kwanza ndani ya Yanga alikuwa panga pangua, lakini mara baada ya Yanga kuongeza nguvu eneo la kiungo kwa kumsajili Khalid Aucho na Yanick Bangala huo ndio ukawa mwisho wake Yanga. Wakati Yacouba alijiunga na Yanga, Agosti 11, 2020 alihudumu klabuni hapo hadi  Julai 15, 2022 akipishana na Stephane Aziz Ki kutokana na kukosa nafasi ya kucheza akiwa nje ya uwanja kuuguza jeraha la goti.

Kwa upande wa Simba iliyokuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo na kushinda 3-0 mbele y Mbeya City, jukwaani alionekana beki wa kati wa zamani wa timu hiyo Henock Inonga ambaye aliuzwa FAR Rabat  ya Ligi Kuu ya Morocco. Beki huyo alishaondolewa katika kikosi cha FAR Rabat na opengine ujio huo una lengo la kusikilizia dili jipya dirisha dogo, japo mwenyewe hakupata nafasi ya kuliweka hilo wazi licha ya kwamba dirisha lililopita alikuwa akihusishwa sana na Yanga kabla ya dili kuishia njiani.