ACHANA na rekodi iliyoandikwa na Azam FC kutinga makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini kikosi hicho chini ya kocha mwenye uzoefu Afrika, Florent Ibenge kinapitia wakati mgumu kutokana na namba kukikataa.
Ipo hivi. Azam inapitia nyakati ngumi kupata matokeo ya ushindi kwani mara ya mwisho furaha ya ushindi ni pale ilipofuzu hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuifunga KMKM 7-0.
Baada ya ushindi huo Ibenge na timu yake hawajaonja ushindi zaidi ya kuambulia sare mbili za mechi ya ligi na vipigo viwili Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi.
Licha ya kukosa furaha ya ushindi timu hiyo kwenye ligi haijapoteza mechi kwani ilianza na ushindi dhidi ya Mbeya City kisha sare ya 1-1 dhidi ya JKT Tanzania na baadaye Namungo Novemba 9 kabla ya majuzi suluhu na Singida Black Stars.
Suluhu ya Singida ilikuja baada ya kuchapika mechi mbili mfululizo za Kundi B la Kombe la Shirikisho Afrika ikianza kulala 2-0 ugenini mbele ya AS Maniema ya DR Congo kisha nyumbani 1-0 kwa Wydad Casablanca ya Morocco.
Katika mechi hizo nne zilizopita Azam timu hiyo imefunga bao moja pekee, huku ikiruhusu nyavu zake kutikishwa mara nne.
Bao pekee ambalo azam ilifunga ni dhidi ya Namungo ikitoka sare ya bao 1-1 na baada ya hapo ikafuatiwa na vichapo viwili na suluhu ya ligi dhidi ya Singida, na kuifanya katika mechi hizo kufungwa mabao matatu ikiwa na wastani wa kuruhusu kila mechi bao moja.
Tofauti na matarajio ya wengi kwa Azam ya Ibenge, hasa kutokana na kuwa na washambuliaji hodari kama Japhte Kitambala, Nassor Saadun na kiungo Feisal Salum ambaye misimu miwili iliyopita tangu alipojiunga na timu hiyo alihusika na zaidi ya mabao 40, akifunga 23 na kuasisti 20, haipo vizuri mbele ya lango la wapinzani.
Fei Toto alifunga mabao 19 msimu wa 2023-2024 na uliopita alifunga manne na kuasisti 13 akiwa ndiye kinara wa pasi za mwisho za mabao katika ligi ya msimu huo, lakini huu amefunga mabao mawili na kuasisti moja.
Akizungumza Ibenge amelia na washambuliaji akisisitiza kufanyia kazi zaidi eneo hilo ambalo limekuwa likikosa umakini hasa wachezaji wakiwa ndani ya 18 kushindwa kufanya uamuzi sahihi.
“Tulikuwa na shida ya kutotengeneza kabisa nafasi. Sasa tunatengeneza, jana (juzi) tumetengeneza nafasi zaidi ya tatu, lakini wachezaji hawajazifanyia kazi. Ninachoweza kusema narudi uwanja wa mazoezi kufanyia kazi hilo,” amesema Ibenge wakati Kitambala akisema makosa yamekuwa mengi eneo hilo kama mshambuliaji atafanyia kazi ili kuisaidia timu iweze kufikia mafanikio huku akidai Ligi Kuu Bara ni ngumu.
“Kazi yangu ni kufunga nimeajiriwa hapa kwa kazi hiyo. Mambo yanayoendelea ni sehemu ya changamoto nitarudi imara na kutumia kila nafasi nitakayotengenezewa ili tuipambanie Azam ifikie malengo. Kuhusu ligi ni ngumu sana,” amesema Kitambala asiye na bao lolote katika Ligi Kuu.
Azam inajiandaa kushuka uwanjani kesho Jumapili kukabiliana na Simba katika Dabi ya Mzizima itakayokuwa mechi ya kwanza kubwa kwa Ibenge katika Ligi Kuu Bara itakayopigwa kwa Mkapa kuanzia saa 11:00 jioni.
