Dk Mwigulu awaambia wananchi wasihofu misaada ilikuwa miaka ya 90

Mwanza. Wakati baadhi ya wananchi wakihofia kusitishwa kwa misaada nchini kufuatia matamko mbalimbali ya kimataifa, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amewatoa hofu wanaohofia kusitishwa kwa misaada nchini, akisema misaada ilikuwa miaka ya ’90’ (1990).

Akizungumza na wakazi wa jijini Mwanza katika uwanja wa Nyamagana leo Ijumaa Desemba 5, 2025, Dk Mwigulu amewataka wasihofie misaada kwakuwa wanaochochea vurugu nchini, wanafanya hivyo kwakuwa wanatolea macho madini yanayopatikana nchini.

“Kuna wengine wanalilia misaada tu kwamba unajua ikienda hivi sasa … ee … misaada sasa misaada, fuatilieni rekodi za misaada ilikuwa miaka ya 90 ndiyo kulikuwepo na misaada wewe unalilia misaada mwenzako analilia urani wako,” amesema

Amewataka watanzania wakiwemo viongozi wa dini, vijana, viongozi wa kimila na sekta binafsi kulinda nchi na kuwa Serikali itayashughulikia magumu yote yanayoonwa na Watanzania na kuyafanya mepesi ili nchi iendelee kuwa na amani na kufurahiwa na wananchi.

“Msimpe mwanya adui kupitia kwenye haya mavugu vugu, mimi nawajua sana hawa watu wanataka yatokee mavugu vugu wao wapitishie ajenda yao pale nawajua … na sisi hatutoruhusu vuguvugu hatutoruhusu vurugu kwa sababu tunajua ajenda zao … tena nimnukuu Rais Magufuli alisema anayetaka kufanya fujo asimtangulize mtoto wa mtu aje yeye mwenyewe,” amesema Dk Mwigulu

Amesema baada ya vijana kufutiwa makosa, Serikali haitarajii wafuate tena mkumbo wa kushiriki kwenye vurugu kama zilizotokea Oktoba 29, mwaka huu.

“Mheshimiwa Rais akatoa msamaha kwa wale waliofuata mkumbo, hatutarajii huko tunapokwenda kwamba patakuwepo na kijana  atafuata mkumbo, hatutarajii na wala hatutoruhusu fujo itawale kwenye nchi yetu. Tumekubaliana kuendesha nchi kwa mujibu wa katiba na sheria kila mmoja ana wajibu wa kutimiza kwenye hili,”

Amesema kwenye nchi yeyote hakuna haki inayokwenda bila wajibu, akisema kila mtu ana haki yake na wajibu wa kutimiza na kusisitiza kwa sababu yoyote  ile Mtanzania asije kusukumwa kwenda kuchoma nchi yake.

Amewataka wananchi kuheshimu sekta binafsi na kuacha kuichukia ili kupambana na umasikini kwakuwa inatengeneza na kutoa ajira kwa vijana.

Katika hatua nyingine, Dk Mwigulu amemtaka mkandarasi Jasco.Co.Ltd kumaliza ujenzi wa Daraja la Mkuyuni lililoanza kujengwa Novemba, 2024 na kutarajiwa kukamilika Novemba mwaka huu ili kumaliza adha ya wakazi wa jijini Mwanza kupita ndani ya maji machafu daraja hilo linapofurika mvua zikinyesha.

Dk Mwigulu amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega kufika kwenye daraja hilo linalounganisha barabara kuu ya Mwanza-Shinyanga kisha amuulize mkandarasi ana maliza lini ujenzi huo.

“Wale wakandarasi wote, yeyote aliyepokea pesa ya mradi ahakikishe kazi ambayo imeshafanyika inalingana na pesa aliyopokea na hapa nimeambiwa kuna  eneo kwenye daraja linaenda lina suasua ni elekeze Waziri wa ujenzi pamoja na huyo mkandarasi … waziri afike kwenye daraja hilo na mkandarasi awepo site aseme anakamilisha lini kazi hiyo,” ameagiza Dk Mwigulu.

Nakuongeza, “Nitakapokuja ziara ya kikazi nikute kazi hiyo imepiga hatua … maeneo ambayo fedha ya walipa kodi imeshatolewa lazima wapate matunda ya fedha yao, tunataka wananchi wasipate kero eneo ambalo Serikali imeshachukua hatua”.

Akitoa taarifa kwa Dk Nchemba, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema mkoa huo umeimarisha ulinzi na usalama si tu kwaajili ya Desemba 9, 2025 bali utakuwa endelevu huku, Naibu Waziri Mambo ya Ndani ya Nchi, Denis Londo akisema jukumu lao ni kuhakikisha wanalinda usalama wa raia na mali zao na kuwa wamejipanga vilivyo kutekeleza jukumu hilo.

Naye, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Michael Lushinge amesema baadhi ya ofisi za chama hicho za wilaya na kata ni miongoni mwa ofisi zilizoathirika kutokana na vurugu zilizotokea wakati wa uchaguzi mkuu huku, Mbunge wa Ilemela, William Kafiti akisema ofisi za kata zaidi ya nane za wilaya hiyo zilichomwa moto.

“Vurugu zilizotokea ziendelee kuwa funzo kwa nchi yetu.. hakuna mtu mwingine wa kuweza kuilinda bali ni sisi tuliepo hapa. Sisi vijana wa nchi hii hatuna budi kuwa tayari kuilinda nchi hii, na hatupo tayari kwa wakati mwingine kushiriki ghasia zilizojitokeza,” amesema Kafiti.

Mbunge wa Nyamagana, John Nzilanyingi amesema, “Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Mkuyuni imechomwa wananchi wanapitia changamoto kubwa sana ya kupata huduma za kiserikali. Niwaombe wana Mwanza wenzangu ilindeni nchi yetu  kwa wivu mkubwa sana,” amesema.