Hekaya za Mlevi: Mitandao iwe chachu ya mafanikio

Dar es Salaam. Kila jambo lina umri wake wa kulifanya. Kama vile mtoto anavyoanza kukaa, kutambaa, kusimama, kutembea hadi kukimbia, maishani mwetu pia kuna mambo mengi yanayofanyika kulingana na wakati husika. Kwa mfano ni lazima uwe na umri fulani ili uweze kuendesha gari.

Kuendesha gari na kuoa kunafanana kwenye mambo kadhaa: Ni lazima uwe umetosha kufanya mambo hayo. Huwezi kuendesha gari ukiwa na miaka minane kwani hutakuwa na urefu wa kuona kinachokuja mbele yako. Hata ukipandishwa juu ya mito, miguu yako itashindwa kukanyaga pedeli za chini. Kadhalika huwezi kuoa kwenye umri huo kwa sababu mwili wako hautakuwa tayari kuleta familia.

Kuendesha gari kunahusiana uelewa wa akili ya dereva. Anaweza kuwa na mwili wa kutosha kuvifikia viungo vya gari kama klachi, usukani, gia na kuweza kuona vema kupitia kioo cha mbele. Lakini kama hajatimiza umri tajwa basi akili yake haijakomaa. Hiki ndicho kinachopelekea masomo ya elimu ya udereva, kwani dereva anajengwa kimwili na kisaikolojia.

Hili linafanana sana na kumiliki silaha. Baadhi ya vigezo vya kumiliki ni uraia, akili timamu na umri. Kigezo cha umri kinamhakikisha mmiliki wa silaha kutumia silaha yake kwa maamuzi ya kiutu uzima. Hata kama atachokozwa, mtu mzima anaweza kutotumia silaha aliyonayo kwa kuhofu usalama wa silaha hiyo. Pia anaweza kutoitumia kuepusha madhara kwa wengine wasio na hatia. 

Vilevile mtoto akishika silaha anaweza kuitumia kwa kujifurahisha. Anaweza kukesha akiwatungua kunguru na popo. Yupo mtoto mmoja wa Kimarekani aliyefanikiwa kuingia shuleni akiwa na silaha ya baba yake. Iliripotiwa kuwa kijana huyu alisimama kwenye lango la ofisi za walimu na kuwaamuru wabusu viatu vyake kwa zamu. Hii ndio akili ya kitoto punguwani anaweza kuchomoa mkwaju akidai chenji yake baa.

Hata matumizi ya mtandao yanapaswa kuangaliwa kwa umakini. Kwenye maeneo mengi mtu mwenye akili timamu anajiuliza iwapo watupiaji wa mada wametimu japo miaka minane. Kazi inakuja kwa watupiaji wa picha utajiuliza kama wana akili timamu. Labda awali ya yote tuelewane ni nini wasomaji wa mitandao ya kijamii wanachohitaji. Ni habari na elimu, mikwatuo na mashauzi, au vyote?

Jibu rahisi “Ni vyote” kwa sababu dunia ina watu wa kila aina. Wapo wapenda maendeleo lakini pia wapo wanaopenda ujinga. Na ikumbukwe kuwa magwiji wa mitandao wanajua mbinu za kila aina za kuwavuta mashabiki. Anaweza kukuvuta kutoka nchi kavu akakutosa baharini. Anakutoa mpirani na kukudondoshea dansini. Lazima utakubali tu.

Baadhi ya wafuatiliaji wanadhani watu hupendezwa zaidi na mambo mapya au ya kipekee. Wakati fulani watu hupenda picha za watu walio kwenye mazingira maalum kama milimani, mabondeni, misituni au kwenye barafu. Waharibifu wa maudhui nao wakaja na mbinu mpya. Leo anatupia akiteleza kwenye barafu, kesho akiogelea kwenye mto, na keshokutwa anaharibu kwa kutupia mambo ya hovyo. 

Kwa kuwa mtu huyu alishakutegea ndoano ukanasa, unaweza ukajikuta ukitembelea ukurasa wake kwa bahati mbaya. Jambo la kwanza ukiona mtu wa aina hiyo, mwondoe kwenye orodha ya wale unaowafuatilia. Aidha anataka kukupiga, au kukupotosha. Na hakuna mtu anayefurahia kugeuzwa zuzu kuna mtu alitaka kumchoma kibaka aliyemdhulumu buku tu. 
Shida siyo buku, bali kufanywa mjinga. Ni afadhali yule mrembo aliyewalaghai washabiki wake kwa picha ya yai. Yai kama lilivyo halijachemshwa wala kukaangwa. Yai hilo lilivunja rekodi baada ya kufuatiliwa na zaidi ya watu milioni 26! Kumbe halikuwa na maudhui ya maana, lakini iliwajengea maswali kama “kuna nini kwenye yai hilo” Wengine wakafikia kujiuliza “au anatuambia kisanii kuwa kapata ujauzito?” 
Mitandao ya kijamii inapaswa kutumika kuziba mapengo tuliyonayo. Kwa mfano mtu anaweza kukosa elimu ya darasani, lakini akawa na ufundi wa kurithi.

Anaweza kuonesha kazi zake na zikawapendeza wengine. Ni bahati mbaya sana wengi hawazingatii kuwa mitandao ya kijamii inafuatiliwa na wengi. Unapotupia picha yako ujue tayari imeshasambaa duniani.

Chukua mfano mdogo tu wa wazee wa “tuma kwenye namba hii”. Hawa hawana mtu waliye na ahadi naye, lakini wanaposema hivyo, wanakutana na watu wenye kujiuliza “nitume kwa namba ipi?” Katika watu mia, wawili wakinasa yeye huwa amefaidika. Huu si mfano wa kuuiga, lakini ukituma kazi yako ya ufundi duniani inaweza kupendwa na angalau mtu mmoja.

Unapotuma picha ukiwa kwenye mbuga za wanyama, hakika ni lazima ipendwe duniani kote. Dunia ya leo imejawa na misongo ya kila aina. Watu wanatafuta dawa ya kujifurahisha, hivyo si ajabu mgonjwa akapata nafuu iwapo atajichukulia yeye ndiye aliye mbugani. Ni kama vile tunavyoangalia filamu, hatukawi kuhamisha nafsi zetu kwa wale mashujaa tunaowatazama.

Tujifunze kuleta maudhui yanayoakisi mila na tamaduni zetu. Magwiji wetu wa mitandao wangetusaidia sana kama wangeitumia fursa hii kukumbusha historia inayopotea, kutangaza rasilimali zetu na kadhalika. Fursa ya utalii ipo wazi sana, inavutia dunia nzima. Na kwa bahati nzuri hakuna yeyote anayekatazwa kuishiriki. Sio kutupia picha zinazotulazimisha kuhoji utimamu wa akili zao.