KMC yaachana na Maximo baada ya siku 131

SIKU 131 zimetosha kwa Marcio Maximo kuwa Kocha wa KMC, baada ya klabu hiyo leo Desemba 6, 2025 kutangaza kusitisha mkataba wake.

Mbrazili huyo alitambulishwa kuwa kocha wa KMC Julai 28, 2025, amefanikiwa kuongoza timu hiyo katika mechi tisa za Ligi Kuu Bara na kuambulia ushindi mara moja, huku vipigo vikiwa saba na sare moja.

Taarifa iliyotolewa na uongozi wa KMC leo Desemba 6, 2025, imesema: “Tumefikia makubaliano ya kusitisha mkataba na Kocha Maximo pamoja na benchi lake la ufundi.

“Tunatambua na kuthamini jitihada walizofanya katika kuboresha utendaji wa timu, ndani na nje ya uwanja, kwa ngazi ya mchezaji mmoja mmoja na timu kwa ujumla.

“Hata hivyo, mabadiliko hayo hayakuweza kuleta matokeo ya haraka, kwani yanahitaji muda wa kutosha ili kuzaa matokeo yanayotarajiwa.

“Tunamtakia Kocha Maximo na timu yake kila la heri, na tunabaki wazi kuwatumia tena pindi fursa itakapojitokeza siku za usoni.”

Wakati Maximo anaondoka akiiacha KMC ikiwa mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara, taarifa zinabainisha huenda Malale Hamsini akarithi mikoba yake. Kumbuka Malale hivi karibuni alikuwa akiinoa Mbeya City iliyoamua kuachana naye kutokana na mwenendo usioridhisha kwenye Ligi Kuu msimu huu.