Ligi ya Vijana Magharibi A yarejea baada ya kusimama miaka miwili 

TIMU 20 zimejitokeza kushiriki Ligi ya Vijana chini ya miaka 20 na 15 katika Wilaya ya Magharibi A baada ya ligi hiyo kusimama kwa kipindi cha miaka miwili. 

Akifungua ligi hiyo leo Jumamosi Desemba 6, 2025, Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya Magharibi A, Yussuf Ali Kessi, amesema changamoto ya kukosekana viwanja vyenye ubora wilayani humo ilichangia kusimama kwa ligi hiyo. 

Amesema wamefikia hatua ya kuirudisha ligi hiyo baada ya kuona viwanja vya michezo vinajengwa katika kila wilaya, huku akifichua kwamba kusimama kwa miaka miwili vijana wao walikosa fursa ya kuonyesha vipaji vyao.

“Kila kitu kwenye michezo kinawezekana, tulikuwa tunakwamishwa na viwanja vya kuchezea kwani vilivyopo havina ubora,” amesema.

Mbali na hilo, amezipongeza klabu kushiriki kwa lengo la kuinua ligi ya wilaya hiyo na kutambulika kama ilivyo kwa wengine.

Naye Mwenyekiti wa kamati ya ligi ya U20, Jaffar Ramadhan Jaffar, amesema awali klabu nyingi zilishindwa kushiriki kwani hazikuwa na uwezo wa fedha kuchagia gharama.

Timu zilizojitokeza kushiriki ni New Kids, New City, Panama Academy, Taifa Jipya FC, Kikaangoni City, Amsadam FC, Beach Villa, Bumbwisudi, Kitundu FC, Yough Legends FC, Kisongoni City, Bumbwisudi, Kitundu FC, Scud SC, Mbuzini, African lions, Alwadady, Amsadam FC, Kisongoni, Chuini, Chivere na Kitundu.