Dar es Salaam. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), limezindua mita janja za umeme ambazo zitamwezesha mtumiaji anaponunua umeme unaingia moja kwa moja.
Ilivyo sasa baada ya kununua umeme unalazimika kuingiza tokeni kwenye mita au kwa kutumia rimoti.
Mita mpya za kielektroniki zina uwezo wa kuwasiliana kimfumo, hivyo kumwezesha mteja kulipia na kuingiza umeme kwenye mita moja kwa moja kama ilivyo kwenye ving’amuzi.
Hatua hiyo imefikiwa wakati ambao baadhi ya wateja wa shirika hilo kwa nyakati tofauti wamekuwa wakilalamika kupata changamoto ya kushindwa kuingiza umeme kutokana na rimoti kuharibika au kuwa na hitilafu.
Akizungumza na Mwananchi, Husna Hassan, mkazi wa Kimara jijini Dar es Salaam amesema amefarijika kuhusu ujio wa mita janja akitaka imfikie mapema kwani amechoka kupanda ukutani kuingiza umeme.
“Umeme ukiisha tunaanza kuwaza nani achukue ngazi aweke umeme kwa kuwa rimoti yetu imeharibika. Natamani nipate mita hii mpya,” amesema.
Kwa upande wake, Donald Mgaya, mkazi wa Mbezi amesema anatarajia urahisi wa upatikanaji wa mita hizo, akieleza amechoshwa na kero za kuharibika kwa rimoti.
“Nyumbani tumeshabadilisha rimoti hadi tumechoka, wakianza kubadilisha tupate wote wenye changamoto kama hii,” amesema.
Mteja anayebadilishaji rimoti iliyoharibika anapaswa kulipia gharama kuanzia Sh50,000.
Uzinduzi wa mita janja umefanyika leo Ijumaa Desemba 5, 2025 kwenye ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Lazaro Twange amesema mita hizo zina faida, ikiwamo kutunza kumbukumbu kwa muda mrefu, zina suluhisho endapo mteja akinunua umeme kwa bahati mbaya.
“Zina taarifa zote juu ya mwenendo wa umeme hivyo zutapunguza mawasiliano ya huduma kwa wateja. Zina mifumo ya kiusalama pia na kulinda udhibiti wa mapato,” amesema.
Twange amesema habari ya kutumia rimoti au kusumbua majirani zimefikia mwisho kwa kuwa mita hizo zimekuja na suluhisho, ikiwemo kuokoa muda.
Akitoa ushuhuda kwenye mkutano huo kuhusu matumizi ya mita janja, mmoja wa watumiaji wake, Emmanuel Mgaya maarufu Mpoki, amesema hazisumbui na ni za uhakika.
Akizungumza na Mwananchi, Meneja Kitengo cha Mita Tanesco, Mhandisi Nyanda Busumabu, amesema hakuna gharama za kubadilisha mita ya zamani ili kupata janja.
“Kwa sasa hakuna gharama ambayo mteja atatozwa. Ni programu inayokwenda kwa awamu ya maeneo, lengo ni kufika nchi nzima. Tutawafikia wateja kwa namna hiyo. Wateja wapya wanaoomba wanafungiwa kulingana na maeneo hayohayo hadi tuwamalize,” amesema.
Amesema: “Hii ni programu inayotekelezwa hatua kwa hatua na mwisho tutafikia wateja wote. Hata sisi tunatamani hata kesho tuamke watu wote wawe wamefungiwa lakini kwa sababu ya utendaji ulivyo lazima twende hatua kwa hatua.”
Kuhusu watu wenye haraka ya kufungiwa mita hizo, amesema wanapaswa kuwasiliana na ofisi za maeneo husika kama Tanesco wilaya au mkoa.
“Unaweza kukuta mtu ana haraka anataka kufungiwa leo kumbe mpango ni kufika kwake kesho. Kwa hiyo mkiwasiliana na ofisi zetu mtapata mipango iliyopo kwamba wataanza awamu kwa eneo gani,” amesema na kuongeza:
“Wakipokea maombi wataona mipango yao ikoje, hivyo itakuwa rahisi kuona namna ya kuitekeleza.”
Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi amesema lengo ni kuhakikisha Tanzania inakuwa na mfumo madhuhuti wa kisasa na kiteknolojia wa huduma na usimamizi wa umeme wenye tija.
Ameiagiza Tanesco kuanzisha aplikesheni itakayorahisha mwingiliano kati ya shirika na wateja wake, ikiwa ni mwendelezo wa kuendana na kasi na mapinduzi ya teknolojia ya sasa.
Ndejembi amelitaka Tanesco kuendelea kuboresha mawasiliano ya mara kwa mara na wateja ili kuimarisha utoaji huduma wa kisasa.
“Kuhusu matengenezo, tujitahidi kuyafanya muda watu wamekwenda kwenye shughuli za utafutaji siyo watu wamerejea nyumbani ndipo mnafanya matengenezo,” amesema.
Ameagiza mita janja zisambazwe nchi nzima kwa kuzingatia usalama wa wananchi, huku wateja wapya wafungiwe mita hizo.
Amesema wenye nia ovu kutaka kujifanya wao ndio wanauza mita hizo amewaonya akisema asitokee mtu wa nje ya Tanesco akajifanya ndiye muuzaji.
“Asije akatijitokeza mtu kwenda kwa wananchi akajifanya yeye ametoka Tanesco, huduma hii itatolewa na Tanesco wenyewe,” amesema.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, amesema sekta ya nishati inakua kwa teknolojia na huwezi kutenganisha vitu hivyo viwili, hivyo mita hizo ni moja ya matokeo yake.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema hali ya ulinzi wa miundombinu ya umeme kwa sasa ipo shwari kutokana na ushirikiano uliopo kati ya serikali ya mkoa na Tanesco.
Amesema kwa sasa wizi wa miundombinu kama nyaya umepungua kwa kiasi kikubwa, hivyo miundombinu ya umeme ipo katika hali nzuri.
“Miezi michache iliyopita kulikuwa na wizi mkubwa wa transfoma, pamoja na ukataji wa miundombinu mingine ya Tanesco, lakini tumeshirikiana kudhibiti kadhia hiyo,” amesema.
