Pointi moja yamliza kipa Prisons, Baraza achekelea Sokoine akitaja usajili

Pamoja na kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mechi, Kipa wa Tanzania Prisons, Mussa Mbisa amesema haikuwa bahati kwao kushinda dhidi ya Pamba Jiji, huku akimuachia jukumu Kocha Mkuu, Zedekia Otieno.

Mbisa ameibuka mchezaji bora wa mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa leo Desemba 6, 2025 kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, baada ya kuonesha kiwango bora kwa kuokoa hatari nyingi na kufanya dakika 90 kumalizika bila ya kufungana.

Katika mechi hiyo iliyopigwa saa 8 mchana, Tanzania Prisons ndio ilikuwa na uchu zaidi ya kukusanya pointi tatu kufuatia matokeo ya kupoteza mechi mbili ugenini dhidi ya Fountain Gate na TRA United ikiruhusu mabao mawili.

Mechi hiyo ilionekana kuwa na ushindani ambapo Pamba Jiji ilihitaji kuendeleza rekodi ya kutopoteza mechi saba saba mfululizo na kufanikiwa kupata pointi moja iliyowafanya kuchumpa nafasi ya pili kwa pointi 16 baada ya mechi tisa.

Mbisa amesema licha ya matokeo hayo kutokuwa mabaya sana, lakini walihitaji pointi tatu ambazo zingewaweka nafasi nzuri katika msimamo.

Amesema sehemu ya makosa yaliyoonekana kiufundi, kocha mkuu ndiye atajua namna ya kuyafanyia kazi akieleza kuwa bado wanayo nafasi ya kufanya vizuri.

“Haikuwa bahati yetu, ila hatujacheza vibaya, tulihitaji ushindi zaidi ya wapinzani ila tunashukuru kwa pointi moja, sehemu ya makosa kocha ataona,” amesema Mbisa.

Kocha Mkuu wa Pamba Jiji, Francis Baraza amesema pamoja na matokeo hayo, lakini anayo kazi kubwa kuwaweka vijana kutobweteka akiahidi kusahihisha sehemu ya makosa.

Kuhusu dirisha dogo, kocha huyo raia wa Kenya, amesema haoni sababu ya kupangua timu badala yake akiona uhitaji hawatazidi watatu wapya kutokana na waliopo kuonesha kitu uwanjani.

“Pointi moja siyo mbaya, wapinzani walikuwa na ushindani, sitaki kuwaambia wanafanya vizuri kwa kuwa wanaweza kubweteka, bado kazi ni ngumu ila tunapambana,” amesema Baraza.