Dar es Salaam. Jeshi la Polisi nchini, limepiga marufuku maandamano yanayodaiwa kupangwa Desemba 9,2025 nchi nzima, likisema yamekosa sifa za kisheria ya kuruhusiwa kufanyika.
Kwa mujibu wa polisi, hadi sasa hakuna barua yoyote iliyofikishwa au kupokelewa na ofisi yoyote ile ya Mkuu wa Polisi Wilaya nchini ya kutoa taarifa kuhusu kufanyika kwa maandamano hayo.
Uamuzi huo wa polisi umekuja, baada ya kuwepo kwa taarifa zinazodai uwepo wa maandamano ya amani yasiyokuwa na kikomo yanayohamasishwa kupitia mitandao ya kijamii.
Hata hivyo, Desemba 2,2025 polisi ilibainisha mambo 12 ikidai yanaendelea kupangwa mitandaoni kuelekea Desemba 9, 2025, huku likiwaonya wanaopanga na kuhamasisha vitendo vya uvunjifu wa amani siku hiyo kuachana navyo, la sivyo watashughulikiwa.
Msisitizo huo wa mara kwa mara kwa polisi wa kutaka wananchi kutojihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani, umekuja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kulihutubia taifa na kueleza jinsi Serikali ilivyojipanga wakati wote kudhibiti vitendo vya kihalifu.
Desemba 2,2025 Rais Samia alitoa kauli hiyo kufuatia kilichotokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025 yalipofanyika maandamano yaliyozaa vurugu katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, Mwanza, Mara, Mbeya, Geita, Dodoma na Arusha.
Vurugu hizo zilisababisha vifo, majeruhi, uharibifu wa mali za umma na binafsi. Miongoni mwa mali zilizoathirika zaidi ni kuchomwa moto vituo vya polisi, ofisi za serikali za mitaa, vituo vya mafuta na mabasi yaendayo haraka na nyumba za watu kadhaa.
Hii ni mara ya pili ndani siku tano, polisi ikiwataka Watanzania kutojihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani.
Mara kwanza polisi ilieleza kile lilichoita njama zinazoratibiwa kupitia mitandao ya kijamii na makundi mbalimbali ya sogozi, zenye lengo la kuvuruga amani nchini.
Jeshi hilo lilidai kumekuwepo na mfululizo wa ujumbe katika mitandao ya kijamii unaohamasisha vitendo 12 vinavyoashiria uvunjifu wa amani, ikiwemo kuzuia shughuli za kiuchumi na kuvuruga miundombinu muhimu ya mawasiliano.
Leo Ijumaa Desemba 5, 2025 Taarifa ya Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamanda David Misime, imeeleza kuwa wanaodaiwa kupanga maandamano hayo, wameongeza jambo jingine la kuhamasisha kubeba petroli kwenye chupa siku hiyo.
“Kulingana na Sheria ya Polisi na Polisi Wasaidizi inayotoa maelekezo na masharti ya kufanya, kukusanya, kuunda au kufanya mkusanyiko au maandamano na kutokana na mbinu za kihalifu zilizobainika wakihamasishana kuzitumia Desemba 9, maandamano hayo yamekosa sifa kisheria,”
“Maandamano yanayopewa jina la maandamano ya amani na yasiyo na kikomo yamekosa sifa za kisheria za kuyaruhusu kufanyika, Jeshi la Polisi lapiga marufuku maandamano,” amesema Misime.
Aidha Misime amefafanua kuwa, maandamano hayo yaliyopangwa kufanyika nchi nzima yasifanyike, akisema wanaohamasisha hawana anuani maalumu zaidi ya kuona namba nyingi za simu za mataifa ya nje ya Tanzania na ndani ya Tanzania.
Pia, Misime amedai kuwa hata akaunti za mitandaoni ni za nje na ndani ya nchi, ambazo wamiliki wake ndio wanaohamasisha maandamano hayo.
“Jeshi la Polisi linapiga marufuku maandamano hayo yaliyopewa jina la maandamano ya amani yasiyo na kikomo yasifanyike.Polisi inatoa wito kwa Watanzania na wasio Watanzania waliopo ndani na nje yan chi kuyakataa,” amesema Misime.
