Sambo, Meya mpya Kigamboni | Mwananchi

Dar es Salaam. Madiwani 14 wa Halmashauri ya Kigamboni wamemchagua Diwani wa Kata ya Kibada, Amani Mzuri Sambo, kuwa Meya wa Halmashauri hiyo, akichukua nafasi iliyoachwa na Ernest Mafimbo aliyemaliza muda wake wa uongozi.

Katika uchaguzi huo uliofanyika leo Desemba 5, 2025, Sambo ambaye alikuwa mgombea pekee, alipata kura 13 za ndiyo na mojawapo ya hapana, kati ya jumla ya kura 14 zilizopigwa.

Kwa upande wa Unaibu Meya, Elizabeth Edith Kimambo aliibuka mshindi baada ya kupata kura 14 kati ya 14, ikiwa ni kura zote za madiwani waliopiga kura.

Uchaguzi huo umeenda sambamba na kuapishwa kwa madiwani na uundwaji wa kamati mbalimbali za kudumu za Halmashauri, katika mchakato uliofanyika mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Pendo Mahalu.

Ikumbukwe kuwa uchaguzi wa kura za maoni ndani ya CCM kwa ajili ya kumpata mgombea wa nafasi ya Meya na Naibu Meya ulifanyika Desemba 1, 2025, ambapo Sambo na Kimambo walishinda nafasi hizo mtawalia.

Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi, Sambo amesema aliomba ridhaa ya kuwania nafasi hiyo kwa sababu anaamini ana uwezo wa kusimamia maslahi ya wananchi na madiwani, na kuongeza kasi ya maendeleo ndani ya Halmashauri ya Kigamboni, hususan kwenye sekta ya elimu.

Huku akisema wapo baadhi ya walimu Wilayani humo hawafundishi ipasavyo huku kazi yao kubwa ni kwenda Kariakoo kuchukua mitihani na kuwapa wanafunzi wafanya.

“Nashukuru mchakato ulienda vizuri na hatimaye nimeibuka mshindi. Napenda kuwaambia madiwani kwamba nitatoa ushirikiano muda wowote kwa ajili ya kuijenga wilaya hii. Tuende na kasi ya maendeleo ambayo jamii inaitaka, maana bila ushirikiano hatuwezi kusonga mbele,” amesema Sambo.

Amesisitiza umuhimu wa madiwani kujibu hoja zinapojitokeza, na kushauri changamoto zinazoweza kutatuliwa ndani ya baraza zifanyiwe kazi mapema ili kuepusha kupelekwa mpaka Bungeni.

Naibu Meya mpya, Elizabeth Edith Kimambo, aliwashukuru madiwani kwa kumchagua na kuahidi kufanya kazi kwa bidii, kwa ushirikiano na viongozi wengine ndani ya Halmashauri.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sudi Mpili aliwataka madiwani kuthamini imani waliyopewa na wananchi, akisisitiza umuhimu wa kusimamia mapato ya Halmashauri.

“Tunawaomba madiwani mfuate sheria na kanuni, na msisahau kusimamia mapato. Kupitia kodi ndipo tunaweza kuleta maendeleo bila migogoro kati yenu na watumishi,” amesema Mpili.

Kwa upande wake, Katibu wa CCM Wilaya ya Kigamboni, Dailo Otanga, aliwahimiza madiwani kutekeleza Ilani ya CCM kwa uadilifu, akiwakumbusha kuwa wote wanatoka chama kimoja.

“Mkifanya kazi vizuri na kuleta maendeleo, hiyo ndiyo njia ya kuhakikisha ushindi kwenye uchaguzi ujao. Ninyi ni kama mkataba wetu na wananchi hivyo nendeni mkafanye kazi,” amesema Dailo.

Diwani wa Kata ya Kisarawe, Issa Hemedi Zahoro, amesema kiapo alichokula ni dhamana muhimu na atahakikisha anatekeleza mahitaji ya wananchi kupitia Ilani ya CCM.

“Wananchi wakae mkao wa kula. Hawajakosea kunichagua, nitafanya yale wanayoyataka kwa kipindi changu cha uongozi,” amesema Zahoro.

Baada ya uchaguzi wa viongozi hao wakuu, baraza pia limeunda kamati mbalimbali za kudumu kwa mujibu wa sheria, zikiwemo kamati ya malezi, kamati ya Mipango Miji, kamati ya huduma za jamii na kamati ya utawala bora.