NAIBU Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini mkoani Manyara, Daniel Sillo amesema serikali itaendelea kuwekeza katika sekta ya michezo ili kuhakikisha nchi inawakilishwa vyema Kimataifa.
Ameyasema hayo katika mashindano ya mbio za Nyika za Madunga msimu wa pili zilizofanyika leo Desemba 6, 2025 wilayani Babati mkoani Manyara, yaliyoandaliwa na bingwa wa marathoni Tanzania, Gabriel Geay kwa kushirikiana na kampuni inayomsimamia ya Pososo Sports na kampuni ya vifaa kutoka nchini Japan ya Asics.
Amempongeza Geay kwa kuanzisha mashindano hayo ambayo yameshirikisha vijana wa umri mbalimbali katika mbio za kilometa 2 wanafunzi wa sekondari, kilometa 4 wanafunzi wa sekondari, kilometa 6 vijana wadogo, kilometa 8 wanawake na kilometa 10 wanaume.
Amesema kupitia mashindano hayo, vipaji vingi vitaibuliwa ambavyo vitakuja kuwa faida kwa nchi hapo baadae, pia serikali itaendelea kuongeza bajeti ya michezo ambayo itatoa nafasi kwa vipaji mbalimbali kuibuliwa na kutoa fursa kwa wanamichezo kuiwakilisha nchi vyema kimataifa.
“Nichukue nafasi hii kuwapongeza waanzilishi wa mashindano haya kwa vijana wetu kwa umri mbalimbali, tunaona vijana wadogo kabisa na umri wa kati pamoja na wale wazoefu, niwapongeze kwa sababu yanaibua vipaji.
“Tunafahamu michezo ni ajira na kupitia michezo hii naamini sasa vipaji vipya wakike na wakiume vitaibuliwa ambao watakuja kuiwakilisha nchi Kimataifa na kufanya vizuri kama Geay na Simbu,” amesema Sillo.
Ameongeza wao kama wawakilishi wa wananchi wataendelea kuisemea michezo na hata ikiwezekana kuongeza bajeti ili kuendelea kuibua vipaji mbali mbali.
Kwa upande wake meneja wa wanariadha Gabriel Geay na Alphonce Simbu, Luis Filipe Posso, ameweka wazi ataendelea kuhakikisha vipaji vingi vinaibuliwa katika mashindano hayo ya Madunga pamoja na zile za Mampando, zinazofanyika Ikungi mkoani Singida ambazo zinaadaliwa na Simbu ili kuwashika mkono vijana ambao wanatamani kutimiza ndoto zao kupitia mchezo wa riadha.
Naye Gabriel Geay amesema kwake ni furaha kuona kile ambacho anafanya kınafanikiwa kwa maana kuandaa mashindano ambayo yanalenga kuibua vipaji vijijini ambapo miongoni mwa matunda hayo ni moja kati ya vijana kutoka katika klabu yake, Benjamin Ferdinand alivunja rekodi yake ya taifa kilometa 15 wanaume, hivyo anafarijika kuona vijana wake ambao anawalea wanavunja rekodi yake.
Kwa upande wake Simbu, amempongeza Geay kwa kuanzisha mashindano ambayo yameonyesha nia ya kuibua vipaji, hivyo amefarijika na anamini kupitia wanariadha hao miaka ya mbele Tanzania itaenda kuwakilishwa vyema kimataifa.
Mbio hizo pia zimetumika kuchagua timu ya Taifa ya mbio za Nyika ambayo itakwenda kuiwakilisha nchi katika mashindano ya Dunia zitakazofanyika Januari 2026 nchini Marekani, ambapo Afisa Michezo wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Charles Maguzu amethibitisha timu hiyo itakwenda kushiriki na kurudi na medali.
Zawadi za fedha, vifaa vya michezo na medali vilitolewa kwa washindi.