Serikali yajibu matamko ya EU, Marekani na mashirika ya kimataifa

Dar es Salaam. Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika taarifa kwa vyombo vya habari imesema Serikali imepokea taarifa na matamko kwa umma yaliyotolewa kwa nyakati tofauti na washirika wa maendeleo na Serikali za mataifa mbalimbali kuhusu matukio ya Oktoba 29, 2025.

Wakati na baada ya uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025 yalifanyika maandamano yaliyozaa vurugu katika mikoa mbalimbali, ikiwemo Dar es Salaam, Mwanza, Mara, Mbeya, Geita, Dodoma, Songwe na Arusha.

Vurugu hizo zilisababisha vifo, majeruhi, uharibifu wa mali za umma na binafsi. Miongoni mwa mali zilizoathirika zaidi ni kuchomwa moto vituo vya polisi, ofisi za serikali za mitaa, vituo vya mafuta na mabasi yaendayo haraka na nyumba za watu kadhaa.

Taarifa iliyotolewa leo Desemba 5, 2025 na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini cha wizara hiyo imesema taarifa na matamko hayo yanajumuisha yaliyotolewa na Ubelgiji, Canada, Denmark, Umoja wa Ulaya, Finland, Ufaransa, Ghana, Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi, Norway, Poland, Slovakia, Hispania, Sweden, Uswisi, Uingereza, Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, Marekani na Taasisi ya Thabo Mbeki.

Wizara imesema Tanzania imeguswa hususani na maudhui ya matamko hayo, licha ya mazungumzo ya wazi kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na wanadiplomasia wanaoziwakilisha nchi zao Tanzania, yaliyofanyika Novemba 28, 2025.

Taarifa imesema ingawa inatambua mchango wa jumuiya ya kimataifa katika kukuza demokrasia na maendeleo ya kijamii na kisiasa nchini, ni muhimu pia kutambua kuanzishwa kwa Tume ya Uchunguzi ambayo itachunguza ghasia za baada ya uchaguzi na kuwasilisha ripoti.

Wizara imesema matokeo ya ripoti hiyo yataleta uelewa wa matukio yasiyofurahisha yaliyotokea na kuwa msingi wa ushirikiano wa kujenga katika siku za usoni.

“Tanzania itaendelea kuwa na dhamira ya ushirikiano wa kimataifa kwa ajili ya amani na maendeleo. Inatoa wito kwa wadau wote kuruhusu mifumo ya kitaifa kutekeleza hatua na mikakati iliyochukuliwa na Serikali,” imesema taarifa hiyo.

Wizara imesema Serikali inaihakikishia jumuiya ya kimataifa na washirika wa maendeleo utayari na dhamira yake ya kuendeleza ushirikiano katika masuala yote ya manufaa ya pande zote, kama washirika walio sawa.